Kadri teknolojia ya mtandao inavyoendelea kukua ndivyo watoto wetu nao wanavyozidi kuutumia. Tafiti zinaonesha kwamba watoto wengi wa Tanzania, hasa wa umri wa miaka 12 hadi 17, wanatumia mtandao kupitia simu zao za mkononi kwa lengo la kutembelea mitandao ya kijamii, kujifunza, na kucheza michezo ya mtandaoni.
Ingawa majukwaa haya yanatoa nafasi ya kujifunza na kuburudika, pia yanawaweka karibu na hatari kama vile unyanyasaji wa kingono, uonevu wa mtandaoni, na ukiukaji wa faragha. Hali hii inaonesha umuhimu wa kuchukua hatua madhubuti ili watoto waweze kutumia mtandao kwa usalama na uhuru.
Siku ya Usalama Mtandaoni mwaka huu ilikuwa fursa ya kuhamasisha wazazi, waalimu, watunga sera, na jamii kushirikiana kuimarisha usalama wa watoto mtandaoni.
Kama tulivyosema hapo awali, hatari kubwa zinazowakumba watoto mtandaoni ni pamoja na unyanyasaji wa kingono. Tatizo hili linaongezeka kwa kasi. Tafiti zinaonesha kuwa baadhi ya watoto wa Tanzania wanaongea na watu wasiowajua mtandaoni kwa lengo la kujenga uaminifu kabla ya kuwashawishi kufanya vitendo visivyofaa. Mitandao ya kijamii na programu za ujumbe mfupi, au messaging apps, ni maeneo ya kawaida ya vitendo hivi.
Mfano, mtoto wa miaka 14 alishawishiwa kupitia mchezo wa mtandaoni hadi kufikia hatua ya kutumiwa maombi ya picha za utupu.
SOMA ZAIDI: Usalama wa Mtoto wa Kike Dhidi ya Ukatili wa Kinjinsia ni Jukumu la Nani?
Pia, kuna unyanyasaji na uonevu wa mtandaoni, au Cyberbullying. Hili ni tatizo lingine linaloathiri watoto kisaikolojia. Watoto wengi wanakumbana na dhihaka, matusi, au kutengwa kwenye mitandao ya kijamii. Mara nyingi, unyanyasaji huu huchochewa na uwezo wa mtu kuficha utambulisho wake mtandaoni.
Wazazi na walimu wanapaswa kuwa macho kwa dalili za mabadiliko ya kitabia yanayoweza kuonesha mtoto anayefanyiwa vitendo hivyo mtandaoni. Mazungumzo ya mara kwa mara yenye upendo ni muhimu katika kuwasaidia watoto wanaokumbana na hali hizi.
Watoto pia wanakutana na maudhui ya vurugu, ngono, au yenye chuki mtandaoni. Bila udhibiti, yanaweza kuwa na athari mbaya kwa afya yao ya akili. Mipangilio ya udhibiti na uchujaji wa maudhui ni hatua muhimu za kuzuia maudhui yasiyofaa.
Kwa sababu hawajui madhara yake, watoto mara nyingi hutoa taarifa binafsi kama jina, anwani, au picha zao bila kufahamu hatari zinazoweza kutokea. Hatua za kuwalinda watoto zinapaswa kujumuisha elimu kuhusu matumizi salama ya taarifa kibinafsi.
Je, lipi jukumu la wazazi, walimu na jamii katika ulinzi na usalama wa watoto mtandaoni?
SOMA ZAIDI: Uelewa wa Kisayansi na Kimila Unavyoweza Kusaidia Kuelewa Uotaji Meno wa Watoto
Wazazi tunapaswa kuhakikisha tunawasaidia watoto kuutumia mtandao kwa usalama. Hii inajumuisha kutumia vichujio vya maudhui, kuweka mipaka ya muda wa matumizi ya mtandao, na kufuatilia tabia za watoto mtandaoni. Pia, ni muhimu kuwa na mazungumzo ya wazi kuhusu hatari za mtandaoni.
Walimu wanapaswa kuwa sehemu ya kuelimisha watoto kuhusu usalama wa mtandao. Ujumuishaji wa masomo ya usalama wa kidijitali kwenye mitaala ya shule inapendekezwa pia ili kuwapa watoto maarifa ya kutambua hatari na kuchukua hatua sahihi. Walimu pia wawezeshwe kutoa elimu hio.
Kwa upande wa jamii, sote tunapaswa kujitolea kuhamasisha usalama wa watoto, tukiona mtoto wa mwenzetu ananyanyaswa mtandaoni tusikae kimya bali tuwe mstari wa mbele wa kuhakikisha mtoto huyo yuko salama. Ushirikiano wa kijamii ni muhimu katika kuunda mazingira salama kwa watoto wetu.
Kwa watoto chini ya miaka 10, tuchunge wanachotazama kila mara, tunaweza kutumia vichujio vya maudhui na tuwaeleze hatari za kubofya viungo, au link, au tovuti zisizojulikana.
Kwa vijana wadogo wa kuanzia umri wa miaka 10 hadi 14, tujitahidi kuwa na mazungumzo nao mara kwa mara kuhusu hatari zilizopo mtandaoni na namna ya kutoa taarifa juu ya matukio ya hatari mtandaoni. Tuwahimize kutumia akaunti binafsi, au private profile, kwenye mitandao ya kijamii na kuwakumbusha kutokutoa taarifa binafsi kwa watu wasiowajua.
Vijana wa umri kati ya miaka 15 hadi 18 tayari wanakuwa na uelewa na ujanja wa kuutumia mtandao. Hivyo tuwape maarifa ya kutambua mbinu za ulaghai na udanganyifu mtandaoni.
Tuwahimize kutoa taarifa kwetu wazazi au walezi au kupiga namba 116 ambayo ni Huduma ya Simu kwa Mtoro ikiwa wamekutana na hali hatarishi mtandaoni na pia tuwafundishe kutumia mipangilio ya faragha kwa usahihi.
Kuhakikisha usalama wa watoto mtandaoni ni jukumu la pamoja. Elimu, usimamizi wa sera, na kampeni za kuhamasisha ni hatua muhimu katika kuimarisha usalama wa watoto.
Kwa kushirikiana, tunaweza kuboresha mazingira ya kidijitali na kuhakikisha watoto wanatumia mtandao kwa usalama. Wazazi, walimu, serikali, na watoto wenyewe sote tuna jukumu la kuhakikisha tunatumia mitandao kwa usalama.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.