Ni kawaida yetu kwamba hatuwezi kujadili jambo hadi yatokee matatizo, au mtu mmoja aibuke na kuanza kuulizia mwenendo wake. Bila ya hivyo, jambo linaweza kwenda miaka na miaka likiwa na kasoro ambayo iliwahi kuibuliwa na kutolewa majibu ya ‘bora liende’.
Kwa sasa, mjadala wa Zanzibar na Muungano umepoa kidogo, na hata ukiwa moto huwa haugusi sana huku kwenye michezo kwa kuwa kuna majibu ya haraka; kwamba suala la michezo si la Muungano.
Majibu mengine, kama huku kwenye mpira wa miguu ni “kama ni ruzuku zinazotoka [Shirikisho la Kimataifa la Soka] FIFA, Zanzibar hunufaika” kwa vitu kama mafunzo ya kiufundi, miradi kama nyasi bandia na vitu vingine.
Jibu jingine ni kwamba kama ni uteuzi wa timu za taifa, kinachoangaliwa si mchezaji ametopa upande gani wa Muungano, bali kiwango na uwezo wake.
Ni kweli kwamba mafunzo ya walimu, waamuzi, viongozi, madaktari na wengine, na kwamba uteuzi wa timu za taifa hutegemea na kiwango cha mchezaji na si uwiano wa wachezaji kutoka Bara na Visiwani.
SOMA ZAIDI: Jamii Haina Budi Kumlinda Ladack Chassambi
Lakini uendeshaji wa michezo kitaifa hujumuisha Wazanzibari kikamilifu? Na kama haushirikishi Wazanzibari kikamilifu, basi hata hizo ruzuku kutoka FIFA huhusisha Zanzibar kama hiari, au utashi binafsi wa viongozi wa wakati huo lakini si kwa utashi wa Zanzibar.
Ukiangalia muundo wa vyama vyote vya michezo, utaona havina uwakilishi wa Zanzibar isipokuwa Kamati ya Olimpiki (TOC) ambayo muundo wake huruhusu wagombea na wapigakura kutoka Zanzibar kushiriki kikamilifu. Ndiyo maana mara kadhaa kunakuwa na viongozi wakuu wa kamati hiyo wanaotokea Zanzibar.
Leo hii useme Wazanzibari wajitokeze kugombea nafasi, hata ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), sijui kama watapata hata kura moja pamoja na kwamba TFF ndiye mwakilishi wa nchi kimataifa. Hii ni kwa sababu wajumbe wote wa mkutano mkuu wa TFF ni kutoka Bara pekee.
Kwa hiyo, muda mwingi shirikisho linakuwa linafanya kazi kama Chama cha Soka cha Tanzania Bara pekee kumbe kimsingi kinawakilisha nchi nzima. Ungetegemea shirikisho lishirikishe vyama vya pande zote mbili za Muungano, lakini linashirikisha Bara pekee.
Ni kweli kwamba masuala ya michezo si ya Muungano, lakini inapofikia uwakilishi wa nchi, masuala ya michezo yanakuwa ya Muungano. Hivyo, ni muhimu kwa vyombo vinavyopewa majukumu ya uwakilishi viwe na sura hiyo ya Muungano kimuundo.
SOMA ZAIDI: Ifike Wakati Maofisa Habari wa Klabu Waache Kupumbaza Mashabiki wa Soka
Bila shaka kuunda chama kingine kitakachokuwa na muundo huo wa Muungano, itakuwa ni kuongeza gharama za uendeshaji, huku suala la mapato likiwa ni tatizo gumu. Lakini nini kinafanyika ili Zanzibar ishiriki kikamilifu katika uendeshaji wa shughuli za michezo na kuweka sura ya kitaifa?
Kuna mambo mengi yanaweza kufanyika, lakini kwa sasa ninaona kuna haja ya vyombo vya juu katika vyama vya michezo kujumuisha wawakilishi japo watatu kutoka Zanzibar. Yaani kama TFF ina kamati ya utendaji ambacho ndicho chombo kinachotoa miongozo ya utendaji, basi chombo hicho kiwe na uwakilishi wa Zanzibar.
Yaani, rais wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), makamu wake na katibu mkuu wawe wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF ili kila masuala yanayoamuliwa kuhusu nchi nao washiriki. Kila inapojadiliwa mikakati ya maendeleo ya soka Tanzania, basin a wajumbe hao kutoka Zanzibar wahusike.
Hii itaisaidia kamati ya utendaji ya chama chochote kuwa na taarifa pana zaidi kuliko zile za kutoka kwa wajumbe wa Bara pekee, hasa inapojadili masuala ya maendeleo ya mchezo husika, kama vile miradi inayofadhiliwa na mashirikisho ya kimataifa ya ujenzi wa vituo vya ufundi, programu kama za Talent Development Scheme (TDS) na mingine mingi inayobuniwa na shirikisho hilo la kimataifa la soka.
Bila ushiriki wa Wazanzibari kwenye vikao vya juu vya vyama vya michezo, ni vigumu kwa viongozi kutoka Bara kujua hasa program hizo zielekezwe wapi linapofikia suala la maendeleo ya nchi nzima.
SOMA ZAIDI: Uraia kwa Viungo Watatu wa Singida Big Stars Haukidhi Maslahi Yoyote ya Kisoka au Kitaifa. Ubatilishwe
Wakati mwingine tunaona Wazanzibari wanadai vikubwa kupita kiasi, lakini kumbe kuna vitu hawajavipata vizuri kama sehemu ya Muungano. Tunahitaji viongozi wenye maono na busara kuliona suala hili katika picha kubwa zaidi ili nchi iwe na uwezo wa kuwaibua akina Feisal Salim wengi zaidi kutoka upande huo wa Muungano.
Baadhi wanaweza kusema Wazanzibari watashiriki kuamua mambo yetu Wabara kama wataingia kwenye kamati za utendaji, lakini midhari tumeshasema kwamba hivi vyama ni vya kitaifa, basi ni lazima ushiriki wa wote sit u uonekane, bali uwe halisi.
Kanuni zinaweza kuwekwa kuwa Wazanzibari wasishiriki kuchangia ajenda ambazo zinahusu uendeshaji wa mchezo wa Bara, lakini masuala mengine yote ya kitaifa, wapewe haki yao.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.