The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Tunawezaje Kuzungumza na Watoto Wetu Kuhusu Suala la Mahusiano?

Lengo si kuwahamasisha waingie kwenye mahusiano mapema, bali ni kuwapatia mwongozo wa kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi yenye heshima na usalama.

subscribe to our newsletter!

Kuzungumza na watoto kuhusu mahusiano huwa ni jambo gumu kwa wazazi wengi wa Kitanzania. Utamaduni wetu unahimiza heshima na maadili ya kifamilia, jambo linalosababisha mazungumzo kati ya wazazi na watoto kuhusu mapenzi na hisia kuwa gumu. 

Hata hivyo, watoto wanapokua, wanapata hisia na shauku ya kuelewa mahusiano, na ni muhimu kwa wazazi kuwa sehemu ya safari hii kwa kuwapa mwongozo mzuri. Wataalamu wa saikolojia na malezi, makuzi na maendeleo ya watoto wanasisitiza umuhimu wa kuwa na mawasiliano ya wazi ili kuwasaidia watoto kufanya maamuzi sahihi kuhusu mahusiano.

Watoto wanahitaji kujisikia huru na kujiamini kuzungumza na wazazi wao kuhusu mahusiano.   Dk Jean Twenge, mtaalamu wa saikolojia ya watoto, anadhihirisha kuwa, “Wazazi wanapojenga mazingira ya usikivu na kuelewa hisia za watoto wao, inakuwa rahisi kwao kufunguka.” 

Tunaweza kulifanikisha hili kwa kutumia mbinu mbalimbali, ikiwemo kuepuka kushtuka, au kuwa mkali, mtoto anapoonesha, au kusema kuwa anampenda mtu, au anapendwa na mtu.

Tunaweza pia kuonesha usikivu na kuuliza maswali muhimu ili tuweze kufahamu kwa kina badala ya kuwahukumu.

SOMA ZAIDI: Tunawezaje Kuwalinda Watoto Wetu Mtandaoni?

Pia, tunaweza kuhakikisha watoto wetu wanaelewa kuwa ni jambo la kawaida kuwa na hisia za kupenda na ni jambo lisiloepukika, yeye kupendwa na mtu na kwamba anaweza kuzungumza na mzazi wake kwa uhuru na kujiamini ili mzazi aweze kumpa ushauri na muongozo sahihi.

Tusikaripie, tuulize maswali

Lakini, tunawezaje kujibu pale mtoto akisema ana mpenzi, amempenda au kapendwa na mtu? Wazazi wengi huwa tunapata mshtuko mtoto, hasa wa  kike, anaposema ana mpenzi, au anampenda mtu au kapendwa, au katongozwa, na mtu. 

Badala ya kukataa au kumkaripia, ni muhimu kumuuliza maswali kama vile, “Unampenda mtu huyu kwa sababu gani?” ili kuona mtazamo wake. Mazungumzo haya pia ni  fursa ya kumuelimisha kuhusu mahusiano yenye heshima na maadili mazuri na kuwaeleza watoto wetu umuhimu wa kujitambua na kujiendeleza kimaisha kabla ya kuingia katika mahusiano. 

Dk Lisa Damour, mwanasaikolojia, anasema, “Wazazi wanapotoa mwongozo badala ya kuonesha ukali, watoto hujifunza kufanya maamuzi bora kuhusu mahusiano yao.”

Katika jamii ya Kitanzania, wazazi mara nyingi hukazia umuhimu wa kuepuka mahusiano kabla ya kukamilisha mipango yao ya maendeleo kama elimu, ajira n.k, na hasa kabla ya ndoa.

SOMA ZAIDI: Usalama wa Mtoto wa Kike Dhidi ya Ukatili wa Kinjinsia ni Jukumu la Nani?

Hata hivyo, watoto wa kizazi cha sasa wanakua katika ulimwengu unaoathiriwa na mitandao ya kijamii, maendeleo ya kiteknolojia na mabadiliko ya kijamii na kutokana na matakwa ya kielimu wengi huondoka majumbani mwao katika umri mdogo, hivyo hukumbwa na ushauri na ushawishi wa makundi rika na kupata taarifa kirahisi ukilinganisha na zamani.

Tunapaswa kuwafundisha kuelewa mipaka kwa kuzungumza nao kuhusu maadili ya familia na maadili ya mtu binafsi ndani ya familia na jamii, ili kuwaelewesha madhara na faida za mahusiano katika wakati muafaka, huku tukiwawekea mwongozo unaowapa muelekeo sahihi. Mwandishi Chimamanda Ngozi Adichie anasema, “Mila zetu zinapaswa kuwa mwongozo wa mazungumzo ya wazi, si vizuizi vya maendeleo ya watoto.”

Badala ya kuwaonya watoto  kwa makaripio na mafumbo tu  kuhusu hatari za mahusiano, tunapaswa kuwafundisha watoto misingi ya mahusiano mazuri na namna ya kujisimamia. 

Mfano, heshima na mipaka, kwamba mahusiano bora yanapaswa kujengwa kwa heshima. Ustawi wa kihisia, kwamba watu ambao wapo kwenye mahusiano wanapaswa kuelewa thamani yao na kuepuka mahusiano yanayoweza kuwaletea madhara. Uwezo wa kufanya maamuzi, kujitathmini na kufanya maamuzi ya busara anapojikuta ana hisia za kumpenda mtu au kupendwa na mtu. 

Dk John Gottman, mtaalamu wa saikolojia ya mahusiano, anasisitiza kuwa “Watoto wanaofunzwa ujuzi wa kukabiliana na hisia za  mahusiano na mahusiano halisi mapema, huwa na maisha ya baadaye yenye furaha na utulivu.”

SOMA ZAIDI: Uelewa wa Kisayansi na Kimila Unavyoweza Kusaidia Kuelewa Uotaji Meno wa Watoto

Ili watoto wetu waweze kuzungumza nasi bila woga, ni muhimu kuwashirikisha uzoefu wetu wa maisha na mahusiano kulingana na umri wao. Tunaweza kutumia mifano kutoka vitabu,  hadithi za jamii, au filamu kuwafundisha masuala ya mahusiano. 

Pia, tuwape nafasi ya kuzungumzia changamoto wanazopitia bila kuhisi kwamba tunawahukumu. Mwandishi bell hooks anasema, “Upendo ni vitendo, si hisia pekee. Kufundisha watoto kuhusu upendo kunahitaji uwazi na ukaribu wa kudumu kati ya mzazi na mtoto.”

Tuna nafasi kubwa ya kuwasaidia watoto kuelewa suala zima la mahusiano kwa njia iliyo salama. Lengo si kuwahamasisha waingie kwenye mahusiano mapema, bali ni kuwapatia mwongozo wa kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi yenye heshima na usalama. 

Watoto wanapojua kuwa wazazi wao ni sehemu salama, na wanaweza kuwa na mazungumzo kama haya, wanakuwa na ujasiri wa kufanya maamuzi bora kuhusu mahusiano na ukuaji wao binafsi.

Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×