The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

CCM Imeongeza Wapigakura Kuzuia Rushwa, Kwa Nini TFF Imewapunguza?

Kitendo cha kupunguza idadi ya wajumbe wa mkutano mkuu kinaweza kuunufaisha uongozi wa sasa, lakini kinaweza kuwa chanzo cha migogoro mingine mikubwa hapo baadaye.

subscribe to our newsletter!

Moja ya matukio makubwa katika mkutano mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika jijini Dodoma mapema mwaka huu ilikuwa ni kufanya marekebisho katika katiba yake kwa kuongeza idadi ya wapiga kura kuanzia katika uteuzi wa wagombea.

Na lengo kubwa la kuongeza idadi ya wajumbe wanaoruhusiwa kupiga kura ni kujaribu kupambana na rushwa ya uchaguzi ambayo husababisha wasio nacho kutopata fursa ya kuongoza hata kama wana sifa na uwezo mkubwa.

Kwa kawaida unapokuwa na wajumbe wachache ni rahisi kwa mgombea mwenye uwezo mzuri kifedha kurubuni wajumbe wengi, kama si wote, na kushinda kirahisi.

Ni rahisi pia kwa mtetezi wa nafasi inayogombewa kutumia wadhifa wake kurubuni wajumbe, na hivyo kuzuia wengine kuingia.

Na kwa kuwa hao wapigakura ndio wajumbe wa chombo muhimu cha maamuzi katika chama au taasisi, inakuwa rahisi kwa kiongozi kuendesha chama au taasisi atakavyo kwa kuwa anawamudu watu wachache walio katika chombo kikuu cha maamuzi katika ngazi fulani.

Enzi za FAT

Hii ndiyo hali iliyosumbua sana mpira wa miguu Tanzania wakati ukiongozwa na chombo kilichoitwa FAT, au Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania, ambacho baadaye kiligeuzwa na kuitwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya vyama vya mikoa kupewa uhuru kamili wa kujiendesha.

SOMA ZAIDI: Kufuta Kadi Nyekundu Haitoshi, Tuanzie Uchunguzi kwa Refa Japhert Smarti

Mkutano mkuu wa TFF ulikuwa na wajumbe takriban 70 tu. Ilikuwa ni ngumu kwa mtu kutoka nje kujaribu kuwaondoa viongozi walioko madarakani, hasa mwenyekiti, kwa kuwa alidiriki kutumia rasilimali zote za chama kurubuni wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi.

Na juhudi za kumuondoa kwa kutumia mkono wa Serikali zilikuwa zikigonga mwamba kwa kuwa Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) haliruhusu Serikali kuingilia masuala ya uendeshaji wa mpira wa miguu.

Na kwa kuwa wakati huo watu wengi waliokuwa karibu na viongozi wa Serikali hawakuwa wakiwashauri vizuri zaidi ya kuwasifia kuwa Serikali inaweza kufanya lolote, kila mara waziri alichukua uamuzi wa kuwaondoa viongozi na kuunda uongozi wa muda, kitu ambacho FIFA ilikikataa na kutishia kuzitoa timu za Tanzania katika mashindano ya kimataifa.

Lakini watu walipochoka na uongozi huo wa kiimla, vuguvugu la mabadiliko likaanza. Wimbi likazagaa kila sehemu, kiasi cha wajumbe wa mkutano mkuu kuonekana kuwa ndio wasaliti wa maendeleo ya mpira wa miguu. Vuguvugu hilo likasababisha FIFA kuja kutaka kujua chanzo cha matatizo.

Ndipo mapendekezo kadhaa yakatolewa, ikiwemo kuondoa nafasi ya Katibu Mkuu na viongozi wengine wa kuchaguliwa, na hivyo uchaguzi ukahusu Mwenyekiti au Rais kwa sasa na wajumbe wa kamati ya utendaji tu.

SOMA ZAIDI: Uwakilishi wa Wazanzibari Unahitajika Uongozi wa Michezo Kitaifa

Baadhi ya viongozi walipinga, lakini wadau wakafungua kesi kuwashtaki waliopinga maelekezo ya FIFA hadi suala hilo lilipopatiwa ufumbuzi.

Kampeni zikawa kali za kutaka kuingiza viongozi wapya ambao wangeleta mabadiliko katika mfumo wa uendeshaji mpira wa miguu na uchaguzi ulipofanyika pale Golden Tulip, mwenyekiti wa wakati huo akatolewa mapema na katika marudio Leodegar Tenga akashinda uenyekiti.

Uongozi mpya ukajikita katika kuifanya FAT na sasa TFF ijiendeshe kitaasisi badala ya hali ilivyokuwa mwanzo wakati mwenyekiti aliweza hata kusema kuwa mchezaji fulani hatachezea timu ya taifa au yeye afe. Yaani ahakikishe Mohamed Mwameja hateuliwi timu ya taifa hadi Muhidin Ndolanga afe!

Idadi ya wajumbe

Lakini tatizo moja kubwa lililoonekana kuwa ndio lilisababisha viongozi kuwa na kiburi, ni idadi ndogo ya wajumbe wa mkutano mkuu. Ndipo vyama shiriki kama cha waamuzi, makocha, wachezaji, cha soka la wanawake na cha madaktari vikapewa nafasi tatu kwenye mkutano mkuu na kila nafasi ilikuwa na haki ya kupiga kura.

Kila mkoa ukaongezewa idadi ya wajumbe wa mkutano mkuu kwa kuweka nafasi ya wachezaji na wanawake, huku viongozi wote watatu wa juu wa mkoa wakiwa na haki sawa ya kupiga kura.

SOMA ZAIDI: Jamii Haina Budi Kumlinda Ladack Chassambi

Mabadiliko hayo yaliongeza idadi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wenye haki ya kupiga kura na hivyo kuweka ugumu kwa wagombea kurubuni wajumbe wengi kirahisi.

Maana yake, ili mgombea akubalike kwa wajumbe wa mkutano wa uchaguzi, ni lazima awe na sera za kueleweka, awe na rekodi nzuri na mambo mengine yanayoweza kumpa sifa za kupigiwa kura.

Na ili mtetezi wa nafasi ya uongozi aendelee kubaki madarakani ni lazima awe amefanya mambo makubwa ya maendeleo yanayoonekana na si ya kutumia tochi kuyajua.

Lakini Mkutano Mkuu wa mwaka 2020 ukaenda kufanya mabadiliko yaliyoturudisha enzi za FAT. Yaani, idadi ya wajumbe wa mkutano mkuu ikapunguzwa kwa kiwango kikubwa. Mbali na kupunguza idadi ya wajumbe, mabadiliko hayo yakapunguza pia idadi ya wajumbe wenye haki ya kupiga kura.

Kwa hiyo, kuna ubaguzi wa wajumbe; kwamba wako wanaoingia Mkutano Mkuu kama maboya na wako wenye haki ya kupiga kura na hawa ndio wanaopewa kipaumbele katika mambo mengi, au kwa maneno mengine, rushwa.

SOMA ZAIDI: Ifike Wakati Maofisa Habari wa Klabu Waache Kupumbaza Mashabiki wa Soka

Tulitegemea katika kipindi hiki, TFF ifanye kazi kubwa ya kuweka mazingira ya kudhibiti rushwa, kumbe ndio imeenda kuweka mazingira rahisi ya rushwa. Kitendo cha kupunguza idadi ya wajumbe wa mkutano mkuu kinaweza kuunufaisha uongozi wa sasa, lakini kinaweza kuwa chanzo cha migogoro mingine mikubwa hapo baadaye.

Kwa sasa inaonekana mambo yanakwenda vizuri kutokana na njia za kufuzu mashindano makubwa kurahisishwa na ndio maana timu zetu zinafuzu fainali za Afrika, huku uwezo wa kifedha wa klabu ukiziwezesha kusajili nyota kutoka kila kona ya Afrika na hivyo kujijengea uwezo wa kupambana na vigogo wa Afrika Kaskazini na Magharibi.

Lakini haya si mabadiliko yanayotuhakikishia maendeleo endelevu, bali yanayojenga mazingira ya rushwa za fedha na hisani kwa wajumbe.

Ni muhimu wajumbe wa Mkutano Mkuu wakaliona hili na kulipigia kelele ili rushwa izuiwe kutoka mbali.

Kama CCM, chama ambacho kinatawala taifa hili, imeona njia nzuri ya kudhibiti rushwa ni kuongeza idadi ya wapigakura, TFF imeona nini hadi ikapunguza idadi ya wapigakura?

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×