The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Nukuu Muhimu Kutoka Kwenye Mahojiano Maalum Kati ya The Chanzo na Ally Salum Hapi, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi, CCM

Kada huyo wa CCM anatetea demokrasia ndani ya chama hicho kikongwe barani Afrika, uteuzi wa Rais Samia kama mgombea wa CCM kwa nafasi ya urais kwenye uchaguzi ujao, na madai ya CCM kutumia vyombo vya dola kubakia madarakani.

subscribe to our newsletter!

Ally Salum Hapi, kiongozi mwandamizi wa chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM), amefanya mahojiano maalum na mwandishi wa The Chanzo, Khalifa Said, na kufafanua mambo mbalimbali yanayohusiana na chama hicho tawala nchini, Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2025, na mwelekeo wa jumla wa nchi, ikiwemo siasa, maendeleo na ustawi wa wananchi.

Kwenye mahojiano hayo ya takriban saa moja, Hapi, ambaye ni Katibu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, alitetea demokrasia ndani ya chama hicho kikongwe barani Afrika, uteuzi wa Rais Samia kama mgombea wa CCM kwa nafasi ya urais kwenye uchaguzi ujao, na madai ya CCM kutumia vyombo vya dola kubakia madarakani.

Hapa tunakuwekea baadhi ya nukuu muhimu zinazoangazia maeneo hayo zinazotoka kwenye mahojiano hayo:

Demokrasia ndani ya chama

“Kuhusu demokrasia, chama chetu [cha CCM] kina demokrasia ya kutosha kabisa, demokrasia pana kabisa, na wapi unaweza kuiona demokrasia [ndani ya chama] ni katika namna ya upatikanaji wa viongozi ndani ya chama chetu, unaweza kuiona kwenye namna ya uwajibishwaji wa viongozi, maana demokrasia siyo tu kupata viongozi, au kutoa mawazo, hata mfumo wenyewe wa kuwajibishana ndani ya chama unapokuwa wa uwazi na unafanya kazi, nayo ni demokrasia hiyo. Lakini tunaweza kuiona [demokrasia] pia kwenye upatikanaji wa viongozi wanaokiwakilisha chama ndani ya vyombo vya dola, Wabunge, Madiwani, tunayo demokrasia ya kutosha sana.”

“Si kweli kwamba CCM hakiruhusu wanachama wake kutoa mawazo [kinzani]. Kuna kitu kinaitwa maamuzi ya chama. Maoni yanaruhusiwa, yanatolewa wakati mnakwenda kufikia uamuzi. Lakini chama kikishafikia uamuzi uliofanywa na vikao halali, kuna jambo linaitwa uwajibikaji wa pamoja; mnapokuwa mmefanya kikao, kwenye [ngazi ya] kata, mmekubaliana kwamba huu ndiyo uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Chama ya Kata, anapotoka mtu mmoja katika kikao kile halali, cha Kikatiba, akaenda kuyabagaza maamuzi ya kikao, huyu sasa hajatoa maoni; huyu ameenda kinyume na kanuni na taratibu za chama.”

“Tunao wanachama wa Chama cha Mapinduzi, mashuhuri kabisa, [wenye mawazo kinzani na hawajafukuzwa]. Chama cha Mapinduzi chenyewe kinaamini katika muundo wa Serikali [ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania] wa Serikali Mbili; lakini wako wanachama wa CCM ambao wao wanaamini kwamba Serikali Tatu ndiyo jibu [la changamoto za Muungano], akiwemo, kwa mfano, mzee wangu [Joseph] Warioba. Lakini [Warioba] hajawahi kufukuzwa uanachama. Kwa hiyo, maoni yanatolewa. Ninachosema hapa ni kwamba ni lazima chama kiwe na mfumo wa ndani wa kudhibiti nidhamu. Ukiacha kila mwanachama, chama kimefanya maoni, watu wametoa maoni yao kwenye vikao, vikao vimeamua, halafu ukaruhusu kukawa tena kuna watu, wanachama na viongozi, wanapinga maamuzi ya vikao, hiyo inaingia kwenye taratibu za kinidhamu za kuwajibishana.”

Uteuzi wa Rais Samia

“Uteuzi [wa Rais Samia Suluhu Hassan kama mgombea wa CCM kwa nafasi ya urais] umefanywa kwa kuzingatia Katiba ya CCM. Katiba yetu inasema, chombo cha juu kabisa chenye mamlaka, ambacho kikiamua hakuna chombo kingine kinaweza kutengua maamuzi hayo isipokuwa chombo hicho hicho chenyewe, ni Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, au CCM Congress, ndiyo chombo cha juu kabisa. Leo hii Kamati Kuu [ya CCM] inaweza kufanya maamuzi, au Halmashauri Kuu, au Sekretarieti, na maamuzi yale yakatenguliwa na Mkutano Mkuu wa Chama.”

Kumnadi Rais Samia

“Rais Samia amefanya kazi kubwa sana, amefanya kazi kubwa katika miaka yake minne. Unapozungumza kuhusu uchumi, Taarifa ya Robo ya Kwanza ya Mwaka 2025 ya Benki Kuu [inaonesha] uchumi unakuwa kwa asilimia 5.7. Ukienda kwenye mfumuko wa bei, mfumuko wa bei umebaki kwenye single digit, asilimia isiyozidi tano. 

“Ukienda katika sekta ya kilimo, nchi yetu inajitosheleza kwa chakula, na imepata mazao mengi inauza mpaka nje ya nchi. Na katika msimu uliopita, korosho, peke yake, imeiingizia nchi yetu takriban Shilingi trilioni moja. Wakulima wamepata bei haijapata kutokea. Huduma za maji zimepelekwa kwa wananchi. Rais juzi ametoka kuzindua mradi mkubwa wa kihistoria wa maji, Same, Mwanga na Korogwe, Shilingi bilioni 600 zimewekezwa pale. 

“Mradi ambao unakwenda kunufaisha vijiji takriban 38. Mradi huu umekuwepo katika makaratasi kwa miaka 20 iliyopita, leo Rais Samia amekwenda kuuzindua, na umetoa maji kwa asilimia 60, imekwenda mpaka asilimia 90. Maji vijijini, zaidi ya miradi 1,000 imetekelezwa katika vijiji vya Tanzania. Rais amejenga madarasa zaidi ya 34,000, mapya, nchi nzima. Leo hatukamati tena kuku wa Watanzania kugharamia ujenzi wa madarasa ya Kidato cha Kwanza. Leo hatutozi michango kwa ajili ya madawati. Kazi kubwa imefanyika. 

“Shule mpya zimejengwa. Zahanati zimejengwa kila kijiji. Rais amejenga vituo vya afya 485, kwenye kata mbalimbali za Tanzania. Vituo vya afya vina uwezo wa kufanya upasuaji, vina uwezo kwa akina mama kujifungua kwa njia ya operesheni. Hospitali za wilaya, magari ya ‘ambulance.’ Unasemaje kwamba Chama cha Mapinduzi, chini ya Dk Samia, hakina hoja za kwenda kwa wananchi? Sisi tunasema tunazo hoja za kutosha.”

Rais Samia ni “asset”

“Rais Samia ni ‘asset,’ na sisi kama Chama cha Mapinduzi, na kama vijana, tunasema Rais ni ‘asset’ kwa sababu gani? Kwanza, amethibitisha pasi na shaka uwezo wake wa kuongoza nchi yetu. Mazingira ambayo ambayo Rais Samia ameipokea nchi hii ni mazingira magumu hayajawahi kutokea katika historia; ni mazingira ambayo Watanzania wote walikuwa na majonzi hawajuwi nini kitatokea kesho. 

“Kwa sababu tukio lile lililotokea, la kufariki kwa Rais aliyeko madarakani, ndiyo tukio la kwanza kwa Rais kufariki akiwa madarakani katika historia ya nchi yetu. Lakini [Rais Samia] amekuwa imara, amekuwa mtulivu. Hatujasikia nchi ikipata mitikisiko. Ametuvusha salama katika kipindi hichi. Jambo la pili, nchi yetu imeendelea kuwa na amani na utulivu, watu wanafanya shughuli zao. Sisi tuko hapa tunajadiliana. Si nchi zote ambazo zinafurahia amani na usalama kama Tanzania, na hili linatokana na uongozi mzuri wa Rais ambaye yuko madarakani. 

“La tatu, tunazungumza kuhusu afya za wananchi. Rais amefanya kazi kubwa ya kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za afya, na huduma zinawafikia kule vijijini, kwa kujenga zahanati, kwa kujenga vituo vya afya vya kisasa, kwa kupeleka ‘ambulance,’ kila halmashauri imepelekewa ‘ambulance,’ kwa kupunguza vifo. Kulikuwa na vifo kwa miaka kadhaa iliyopita, Watanzania 556 walikuwa wanafariki kutokana na matatizo ya uzazi, kati ya Watanzania 100,000. 

“Leo hii Tanzania imepunguza vifo vinavyotokana na uzazi kwa asilimia 80, na Tanzania imepata tuzo ya Bill & Melinda Gates ya the Goalkeepers, ambayo kwa mara ya kwanza katika historia ya tuzo hiyo ndiyo imetoka nje ya Marekani na imekuja Tanzania, kuenzi kazi kubwa iliyofanywa na Dk Samia Suluhu Hassan. 

“Sasa, ukigusa afya, ukaguza maji, ukatoa elimu bila ada mpaka Kidato cha Sita, watoto wa Watanzania masikini wakasoma, ukajenga madarasa, ukawaondolea Watanzania adha ya kukamatiwa kuku na mbuzi zao kuchangia ujenzi wa madarasa, umegusa maisha ya Watanzania kwa zaidi ya asilimia 90.”

Matumizi ya vyombo vya dola

“Chama cha Mapinduzi ndiyo chama chenye wanachama wengi kuliko vyama vyote Tanzania. Na juzi, Katibu wetu Mkuu, Balozi Dk Emmanuel Nchimbi, ameeleza kwa Watanzania [kwamba] tuna wanachama wa kielektroniki, tuliowasajili, zaidi ya milioni 12 na laki moja na ushee. Katika uchaguzi wa mwaka 2025, wapiga kura wanaokadiriwa kwamba watakwenda kupiga kura ni milioni 31. CCM tayari tuna mtaji wa milioni 12, wa wanachama peke yake; acha wakereketwa, mashabiki na wapenzi, wanachama peke yake, milioni 12! Ukitoa katika kura milioni 31, unabaki na kama milioni 19. 

“Kwa hiyo, tuna mtaji wetu. La kwanza. La pili, sisi hatutegemei dola kushinda. Chama kinachaguliwa kwa sababu ya mambo makubwa mawili. La kwanza, nini kimefanywa, kilipopewa dhamana, na ndiyo maana nasema sisi tumefanya, tumefanya [kwenye] maji, umeme, elimu, huduma za afya, mikopo kwa vijana, tumepandisha madaraja, Rais kapandisha madaraja watumishi wa umma. Haya ni yale tuliyoyafanya, ya utekelezaji wa Ilani, ambayo tulikubaliana na Watanzania mwaka 2020. 

“La tatu, tunapeleka nini kwa wananchi kama matumaini katika miaka mitano ijayo? Mtaona Ilani yetu. Tunakwenda kufanya mambo makubwa zaidi kuliko haya ambayo tumeyafanya katika miaka hii mitano inayokwisha. Kwa hiyo, nataka kukuthibitishia hatutumii dola, wala hatuhitaji dola kushinda uchaguzi.”

‘Kazi na Utu, Tunasonga Mbele’

“Kauli mbiu ya ‘Kazi na Utu, Tunasonga Mbele,’ kipande cha ‘Kazi,’ kinasadifu kwamba [CCM] tunataka kujenga taifa la aina gani? Tunataka kujenga taifa la watu wanaofanya kazi. Tunataka kujenga taifa ambalo kazi ndiyo msingi wa utu wetu, wa uhuru wetu, na kauli mbiu hii ni kauli mbiu kama watu hawafahamu, wakati tunapigania ukombozi wa nchi yetu, ilikuwa ‘Uhuru na Kazi,’ ni kauli mbiu ambayo ilitumika wakati wa TANU na wakati wa Baba wa Taifa [Julius Kambarage Nyerere]. Kwa hiyo neno ‘Kazi’ limeendelea kujitokeza sana katika awamu mbalimbali kama kielelezo cha kwamba sisi ni taifa la watu wanaoamini katika kuchapa kazi.

“‘Utu,’ nayo inakurudisha kule kule, kwamba Chama cha Mapinduzi kinaamini kila Mtanzania, kila mtu, anastahili kuthaminiwa utu wake, bila kujali makabila yetu, hadhi za uchumi, vyama vyetu vya siasa, Utu ndiyo kitu kikubwa ambacho sisi tunataka kujenga. Kwa hiyo, ‘Kazi na Utu’ inaweza kuunganishwa katika namna hiyo. Lakini la pili, ni haiba ya Rais wetu na mgombea wetu mteule. Ni mtu ana haiba ya utu, anapenda watu, ni mtu ambaye anajali haki za watu, anajali usawa. Kwa hiyo, tumedhani kwamba ‘Kazi na Utu’ ni mambo ambayo yanakwenda pamoja, lakini yanasadifu yale ambayo tunataka tuyafanye kwa Watanzania – maji yanahusu watu, afya zinahusu watu. Unapowasaidia akina mama wajawazito wajifungue kwa usalama, wapate huduma nzuri, huo ndiyo utu wenyewe. ‘Tunasonga Mbele’ kazi inaendelea.” 

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×