Dodoma. Katika miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia matumizi ya teknolojia ya akili mnemba [AI] yakishika kasi katika sekta mbalimbali, na tasnia ya habari ikiwemo. Katika tasnia ya habari tumeona waandishi wa habari wakitumia AI kutafuta mawazo ya habari, kuchakata taarifa, kutengeneza sauti na picha.
Ingawa teknolojia imeonekana kuwa na manufaa, wadau wa habari wanaonya waandishi wa habari kutotumia teknolojia hiyo kama nyenzo pekee ya kufanya kila kitu.
Mtaalamu wa Dijitali na Usalama Mtandaoni [Digital and Cyber Expert] kutoka Jamii Forums Emmanuel Mkojera anasema, katika kipindi hiki akili mnemba imerahisisha kazi za waandishi wa habari, wanatumia AI katika masuala mbalimbali ikiwemo kupata mawazo ya habari, kufupisha taarifa, kutengeneza picha zinazo endana na maudhui bila kuwa na picha halisi za tukio.
“Kikubwa zaidi AI inawasaidia waandishi katika kukabiliana na masuala ya Mis- and Disinformation [Maudhui ghushi] hususani kwa zile taarifa zinazosambaa kwa njia ya picha au video,” Mkojera anaiambia The Chanzo.
“Mfano, kwa sasa ‘business insider’ wanatengeneza AI iitwayo SAGA REACT. Hii itasaidia mwandishi kuweza kutabiri kwa namna gani andiko lake linaweza kupokelewa na jamii anayoiandikia. Inaweza isiwe sahihi, ila kwa namna moja itampa mwanga namna ya kuandika andiko lake,” anaongeza Mkojera.
Kuwe na angalizo
Mkojera anasema, mbali na AI kurahisisha yote hayo, kunatakiwa kuwe na angalizo kwa waandishi wa habari.
“Waandishi wanapaswa kutumia AI kama msaidizi, ila sio nyenzo pekee ya kufanya kila kitu,” anasisitiza. “ Hili litapelekea AI kuchukua nafasi ya mwandishi katika kazi yake. Waandishi wa habari wanatakiwa wasiogope AI, ila wawe makini katika matumizi yake.”
Mwandishi wa Habari na Mtetezi wa Haki za Kidijitali Imani Luvanga anasema, licha ya AI kuleta mawazo mapya, kuokoa muda vyombo vya habari vinapaswa kuwa na Sera madhubuti ya matumizi ya AI, kuhakikisha kwamba inatumika kwa uangalifu na kwa kuzingatia maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.
“Kufahamu namna bora ya kutumia akili mnemba ni jambo muhimu sana,” anasema Imani. “Lakini vyombo vya habari ni muhimu kuwa na Sera ambayo inatoa miongozo ya matumizi ya AI. Vikiwa na Sera nzuri, vikiwa na programu za kufundisha waandishi wao namna bora ya kutumia AI. Ni kitu ambacho kinakwenda kuleta mapinduzi makubwa kwenye tasnia ya habari.”
Akizungumzia mchakato wa ukusanyaji wa data, Imani anasema kuna taarifa ambazo ni za siri na za faragha. Hali hii inaweza kupelekea kutoa taarifa ambazo ni hatari, kwa kuwa hakuna uhakika wa kiwango cha usalama kinachotumika kuzilinda.
“Hatuna uhakika kwamba ni kwa namna gani hizi mashine zinatunza na kuchakata taarifa zetu,” anasema Imani.
Ingawa AI ina uwezo wa kufanya kazi kwa muda mfupi, kwenye kuchakata wazo la habari akitolea mfano kutoka dakika 30 hadi chini ya dakika moja, anasema lugha inayotumiwa ni ya mashine . Hivyo, ni muhimu kuhakikisha taarifa zinazo patikana.
“Sisi kama wanahabari tunapaswa kuwa na uelewa mpana juu ya mambo ambayo tunapaswa kufanya, au juu ya habari ambazo tunapaswa kufanya kwa msaada wa AI,” anasisitiza imani.
Irahisisha kazi bila kuharibu taaluma
Victor Maleko ambaye ni Afrisa Programu wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania UTPC anasema, anaiona AI kama nyenzo muhimu katika taaluma mbalimbali ikiwemo uandishi wa habari. Kwa kuwa, inarahisisha utendaji kazi bila kuharibu taaluma ya mwandishi wa habari kama ilivyo.
“Kwa mfano, naiona AI imesaidia kuzuia taarifa potofu, uhakiki wa taarifa [fact checking],” anasema Victor. “Unapokuwa na data ambazo huna uhakika nazo kama mwandishi wa habari, ama unataka kufanya uthibitisho wa taarifa fulani hizi zana za AI [tools] zinaweza zikakusaidia kuhakikisha data zako kwa maana ya kujua nini kilitokea.”
Victor anasema, AI ni nyenzo muhimu inapohitajika kuchakata data. akitolea mfano wa matokeo ya uchaguzi au takwimu michezo AI inaweza kusaidia kupanga na kuchambua data kwa urahisi kuonyesha ni mgombea gani anaongoza, mikoa iliyopata kura nyingi zaidi, au timu zilizo fanya vizuri kwenye ligi .
Anaongeza kuwa, kwenye eneo la uzalishaji wa maudhui ya vyombo vya habari, AI imerahisisha kazi kama vile uhariri wa video na tafsiri za lugha.
“Lazima [pia] tuitumie AI kwa tahadhari hizi ni mashine zina kosea. Kwa hiyo, akili ya mwandishi wa habari, utashi wa mwandishi wa habari na taaluma yenyewe lazima ihusike wakati wa kutumia AI. Kwa sababu hatuwezi kuzitumia kwa asilimia 100 uhakika kwamba AI ziko sahihi.”
Kuna mabadiliko na changamoto
Mhariri wa chombo cha habari cha Clouds Joyce Shebe, anakiri AI kuleta mabadiliko kwenye sekta ya habari, huku akisema wakati mwingine huleta changamoto.
“Ndani ya hiyo teknolojia ya AI inaweza ikatengeneza taarifa ambayo si sahihi. Inaweza ikapotosha maana nzima ya kinachotakiwa kuzungumzwa. Wakati huo huo AI ni kama mifumo ambayo inakuwa na upendeleo fulani. Haiwezi kuwa na mizania. Kama unavyo jua vyombo vya habari katika misingi yetu tunapaswa kuweka mizania kuhakikisha taarifa inajieleza vizuri.”
Joyce, anasema AI haina ladha ya kibinadamu kwenye utafutaji wa taarifa. “Bado jicho la binadamu linahitajika kuangalia kwamba hii taarifa salama kiasi, ni uhakika kiasi, na maadili yamezingatiwa kwa kiasi gani. Mwisho wa siku tutakubaliana kwamba sawa imekuja na changamoto zake na fursa zake,” anasema Joyce.
“Lakini mwisho wa siku wana habari lazima tujiongeze tukasome tuijue AI. Tujue matumizi yake, tuitumie kwa ufasaha. Tusipo tumia kwa ufasaha tutajikuta tumeingia kwenye changamoto za kitaaluma.”
Kwa upande wa Mwandishi wa Habari Florence Majani anasema, anaona AI imeongeza hali ya kutojituma na kufikiri kwa waandishi wa habari. Anasema, mwandishi mzuri ni yule anayefanya utafiti, akazitengeneza vizuri na baadae ajaribu kutafuta kwa upana kwa anacho kifanya.
“Lakini waandishi wengi wanatumia AI anaiuliza chart GBT Florence Majani ni nani? anacho kipata ndicho anacho kiandika. Hasa huo ni uandishi au uzembe. Akitumia kifaa kinachompa taarifa zozote bila yeye kujishughulisha, kusoma kwa kweli tunategeneza kizazi cha waandishi wa habari ambao ni wavivu kupindukia.”
Ametoa rai kwa waandishi wa habari kuitumia AI kwa manufaa, na wasibweteke ili kutosababisha kushindwa kufanya majukumu yao.
“Kwa sababu, majukumu ya mwandishi wa habari ni kusoma, kutafiti, kufikiri kuchambua ndiyo aweze kutumia maudhui kwenye chombo chake. Sasa wanahabari wengi sasa hivi hatufanyi hivyo. Tunategemea teknolojia itufanyie kila kitu. Ikikudanganya, ikikupata taarifa ambazo siyo za kweli umepotea.”
Ni kitu kipya
Mkurugenzi wa Ubunifu [creative director ] Warda Mansour anasema, hawezi kusema imeleta mabadiliko kwa kiasi kikubwa, kwa kuwa ni kitu kipya ambacho kimeanza hivi karibuni.
“AI kwa sasa ina sababisha kutengenezwa kwa maudhui ambayo yanawezekana siyo ya kweli. Ambayo pia yanaonekana ni ya kweli,” anasema Warda. “ Kwa hiyo, yana athiri kwa kiasi kikubwa taarifa wanazo pokea watu hususan kwenye mitandao ya kijamii. Na hii tunaweza tukaona hata siyo nchi yetu inaathirika pekee hata nchi za nje.”
Warda anasisitiza waandishi wa habari, kujifunza teknolojia hii kabla ya kuanza kuitumia, akiwa na maana ya kuwa bila kujifunza itakuwa ngumu kujua madhara yake na faida yake.
“ Tujifunze kuthibitisha [taarifa] tusitegemee AI peke yake,” anasisitiza Warda. “AI ni roboti haina hisia za kibinadamu . Hata kwenye uelezaji wa habari siku zote mimi huwa nasema AI imetengenezwa kujibu kile ambacho inaulizwa. Tofauti na sisi binadamu unaweza ukaripoti habari kwa huruma na hisia.”
“Kwa hiyo, tunapoenda kutumia hii teknolojia mpya tunajitaji kujua wapi kuna changamoto na wapi kuna faida. Kwenye faida tuchukue, faida tutumie kwenye changamoto kuhakikisha kwamba haitupi nafasi ya kutengeneza makosa. Au kutengeneza madhara yoyote kwenye jamii,” anaongeza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA Dk Rose Reuben anasema, AI itawaacha nyuma wale ambao hawataki kuitumia, kwa kuwa ni teknolojia inayo endelea kukua kwa kasi.
“Wale ambao watapitwa inawezekana kabisa ikawatoa nje ya wigo wa uandishi wa habari. Ni vyema waandishi wengi waanze kujifunza ni namna gani wanavyoweza kutumia AI na kurahisisha kazi zao. Imekuwa ni nyenzo muhimu inayo rahisisha kazi. Na nyezo muhimu inayo fanya maisha yawe mepesi kwa uandishi wa habari.”
Jackline uwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana mkoani Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jaquelinevictor88@gmail.com