The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Waliovurunda ‘Dabi ya Kariakoo’ Walazimishwe Kuomba Radhi Hadharani

Wenzetu wanatunga sheria zaidi ili kulinda mashabiki ambao ndio nguzo kubwa ya michezo duniani, lakini huku watu wanatoa taarifa ya kuahirisha mechi kiholela bila ya kuonyesha kujali athari ambazo mashabiki wamezipata

subscribe to our newsletter!

Waziri wa Utamaduni,  Sanaa na Michezo, Profesa Palamaganda Kabudi, amekutana na viongozi wa klabu za Yanga, Simba, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi (TPLB) kujadili sakata la uahirishaji tata wa mechi ya klabu hizo mbili iliyokuwa ifanyike Machi 8, 2025.

Siku moja kabla ya mechi, Simba ilizuiwa kutumia Uwanja wa Benjamin Mkapa na mamlaka za uwanja huo na watu wanaosadikiwa kuwa ni walinzi wa Yanga, kitendo ambacho ni kukiuka kanuni ya ligi inayoipa timu ambayo siku hiyo ni mgeni kufanya mazoezi uwanja utakaotumika kwa muda ule wa mechi.

Simba ilisema haingecheza mechi hiyo hadi waliohusika wote wapatikane na kuchukuliwa hatua, kitu ambacho pia ni kinyume na kanuni za ligi zilizoweka adhabu kwa yeyote anayehusika kuzuia timu kufanya mazoezi lakini haitoi haki kwa timu hiyo kutocheza mechi siku inayofuata kwa kisingizio hicho.

Lakini Yanga ikasisitiza kuwa itapeleka timu uwanjani kwa kuwa hakuna kanuni inayoruhusu mechi kuahirishwa kwa sababu hizo na tamko la Yanga likafuatiwa na taarifa ya Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi ya TPLB ambayo iliweka msisitizo kuwa mechi ipo kama ilivyopangwa na waliohusika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni.

Lakini saa mbili kabla ya mechi, kamati hiyohiyo ikatoa taarifa nyingine kuwa mechi imeahirishwa kwa madai kuwa imeona viashiria vya vurugu na rushwa, hivyo mechi itapangiwa siku nyingine.

SOMA ZAIDI: Kwa Kuifokea Yanga, Karia Ameonesha Upande Kwenye Sakata Kati ya Klabu Hiyo na Simba

Lakini Yanga, ambayo huweka kambi yake Avic Town iliyo umbali kama kilomita 40 kutoka feri ya Kigamboni, ikasema itapeleka timu uwanjani kwa kuwa uahirishaji huo wa mechi haukuzingatia kanuni. 

Kwa kuzingatia muda wa kuahirisha mechi na muda ambao timu hutakiwa ziwe zimeshawasili uwanjani, ni lazima timu ya Yanga ilikuwa ndio kwanza inavuka daraja la Kigamboni kuelekea Uwanja wa Benjamin Mkapa, kama kilomita nyingine 20.

Bila shaka, na kama ilivyo kawaida, kikao cha waziri na viongozi wa pande hizo kitakuwa ni cha kutafuta muafaka wa tarehe mpya ya mechi na kama kutakuwa na mtu atakayebainika kuwa alikosea, washiriki wataombana radhi humohumo au kuambiwa ukweli.

Ukweli na uwazi

Lakini katika dunia ya sasa, ukweli na uwazi ndio unaoleta uwajibikaji. Ni lazima jambo hilo lizungumzwe kwa ukweli na uwazi kujua walioahirisha mechi katika hali ya utata ni nani na walifanya hivyo kwa lengo gani. 

Hawa ni lazima wajulikane kwa jamii kuwa ndio waliosababisha taharuki kubwa kwa mashabiki na Watanzania kwa ujumla pamoja na fedheha kwa mpira wa miguu.

SOMA ZAIDI: Ni Kupoteza Muda Kujadili Kanuni Sakata la Simba, Yanga

Ni jambo lililo wazi kuwa mechi za mpira wa miguu haziwezi kusimamishwa, au kuahirishwa, kwa mambo ya ukiukwaji wa kanuni ambao umeshawekea adhabu zake na utaratibu wa kushughulikiwa.

Ni majanga makubwa tu kama mabadiliko ya ghafla ya hali ya hewa, tetemeko, mafuriko, magonjwa ya mlipuko na mambo mengine ndiyo yanayoweza kuwa nje ya uwezo wa wasimamizi na waendeshaji wa ligi.

Haiwezekani watu waliokutana kwenye kikao cha Kamati ya Usimamizi wakawa hawajui ukweli huu. Ni lazima walifanya hivyo kwa makusudi, hasa baada ya kugundua kuwa msimamo wa Simba ulikuwa thabiti kuwa wasingepeleka timu uwanjani na walijua madhara ya msimamo huo.

Kwa maana hiyo, watu waliovunja kanuni kwa makusudi hawawezi wakaachiwa kirahisi tu kwamba wameomba radhi kikaoni halafu mambo yaendelee kama kawaida.

Kuomba radhi

Ili kuonyesha kuheshimu mashabiki, ambao kwa mara ya pili mfululizo wanasumbuliwa kiuchumi na kijamii kutokana na vitendo vyao vya kuahirisha mechi kiholela, ni lazima kikao cha muafaka kiwalazimishe watu hao wajitokeze hadharani na kuomba radhi ili wawajibike kwa jamii na wanamichezo wote kwa ujumla.

SOMA ZAIDI: CCM Imeongeza Wapigakura Kuzuia Rushwa, Kwa Nini TFF Imewapunguza?

Wenzetu wanatunga sheria zaidi ili kulinda mashabiki ambao ndio nguzo kubwa ya michezo duniani, lakini huku watu wanatoa taarifa ya kuahirisha mechi kiholela bila ya kuonyesha kujali athari ambazo mashabiki wamezipata, hasa kwa mechi kubwa kama hizo ambazo watu husafiri kutoka kona mbalimbali za nchi na nje, na huanza kuingia uwanjani mapema.

Kitu cha kufikiria ni kwamba kama tangazo hilo la kuahirisha mechi lingewaudhi mashabiki hao na kuanza vurugu za kung’oa viti na pengine kushambuliana au kushambulia wahusika, hali ingekuwaje? Ingekuwa rahisi kudhibiti watu labda 20,000 ambao walikuwa wamshaingia uwanjani wakati huo?

Vipi kuhusu kampuni ambazo zilijihusisha na mechi hiyo kama Azam Media, NBC, SportsPesa, M-Bet, GSM, Mohamed Enteprises na nyingine nyingi, ni kwa jinsi gani ziliathiriwa na uamuzi huo wa kuahirisha mechi?

Kuwajibika

Hawa wote na wengine wengi ni lazima waone waliokosea wanawajibika na kuwajibika si kujiuzulu pekee, hata kutoa tamko la kuomba radhi wote walioathirika ni kuwajibika pia kwa kuwa kunajenga kumbukumbu kuwa likitokea tatizo jingine, waathirika waterejea tamko la kuomba radhi.

Kikao hicho pia kitoke na ahadi ya mamlaka kuangalia upya mfumo wa usimamizi kwa kuwa hauweki uwajibikaji kwa wanaohusika kusimamia ligi. 

SOMA ZAIDI: Kufuta Kadi Nyekundu Haitoshi, Tuanzie Uchunguzi kwa Refa Japhert Smarti

Kama mwenyekiti wa TPLB ndiye mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi na huyohuyo ndiye mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Bodi ya Ligi. Huyu ndiye amefanya uamuzi wa kuahirisha mechi na bado anaenda kuongoza kikao cha Kamati ya Uongozi, atawajibishwa na nani?

Kwa hiyo, mbali na makosa ya kimazoea ambayo yalifanywa na wenye mazoea kuamua jambo lenye taharuki kubwa, kutakiwa kulazimishwa kuomba radhi hadharani, muundo wa bodi na usimamisi wa shughuli za bodi ni lazima ubadilishwe ili uweke uwajibiakaji.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×