Ujauzito ni safari ya kipekee inayobadilisha siyo tu umbo la mwili wa mwanamke bali ubongo wake pia. Tafiti za kisayansi zimebaini kuwa ujauzito husababisha mabadiliko makubwa katika ubongo wa mwanamke, ikiwa ni pamoja na kupungua kwa ukubwa wa sehemu fulani za ubongo.
Ingawa mabadiliko haya yanaweza kuonekana kama jambo la kutia wasiwasi, tafiti zinaonesha kuwa ni sehemu ya mwitikio wa asili wa mwili ili kumuandaa mama kwa ajili ya kumlea mtoto wake.
Utafiti uliochapishwa katika Nature Neuroscience umethibitisha kuwa ujauzito husababisha kupungua kwa sehemu ya kijivu, au gray matter, katika maeneo mahususi ya ubongo. Sehemu ya kijivu kwenye ubongo huhusika na kazi ya kuchakata taarifa, kudhibiti hisia, ujifunzaji na kumbukumbu, pamoja na utambuzi wa kijamii au kuhusiana kijamii.
Kwa kutumia vipimo vya teknolojia ya MRI, yaani miyonzi, watafiti waligundua mabadiliko katika ubongo wa wanawake kabla na baada ya ujauzito, wakibaini kuwa upungufu wa sehemu ya kijivu ulitokea hasa katika maeneo yanayohusiana na utambuzi wa kijamii, udhibiti wa hisia, na uundaji wa ukaribu, kwa maana ukaribu na mtoto au mtu wa karibu.
Watafiti wamebaini kuwa mabadiliko haya yanaweza kudumu kwa angalau miaka miwili baada ya kujifungua. Hata hivyo, jambo la kuvutia ni kwamba, ingawa baadhi ya sehemu za ubongo hupungua kwa ukubwa, ufanisi wake huongezeka.
SOMA ZAIDI: Leo Tujadili Namna Tunavyoweza Kukuza Watoto Wetu Kuwa Wasomaji Wazuri
Hii ina maana kuwa badala ya kuwa kikwazo, mabadiliko haya yanamuwezesha mama kuwa makini zaidi katika kugundua mahitaji ya mtoto wake na kumhudumia kwa upendo na uangalifu mkubwa.
Baadhi ya wanawake wajawazito wanaripoti kuwa na changamoto za kumbukumbu, yaani kuwa msahaulifu, hali inayojulikana kitaalamu kama baby brain au momnesia. Hii inaweza kujitokeza kama kusahau vitu vidogo kama mahali ulipoweka funguo au kushindwa kukumbuka majina kwa haraka.
Watafiti wanaamini kuwa hii inatokana na ubongo kuelekeza nguvu zake zaidi katika mahitaji ya msingi ya mtoto, kama vile kuimarisha uhusiano wa kihisia na kumlinda dhidi ya hatari.
Baada ya kujifungua, ubongo wa mama huanza kurejea katika hali yake ya kawaida. Tafiti pia zinaonesha kuwa ndani ya miezi sita hadi mwaka mmoja, ubongo huanza kurejea katika ukubwa wake wa awali, huku ukibaki na uwezo wake mpya wa kuelewa mahitaji ya mtoto kwa haraka zaidi.
Mabadiliko haya ya ubongo yana faida kubwa kwa mama na mtoto. Kupungua kwa baadhi ya sehemu za ubongo husaidia kuimarisha hisia za upendo na ukaribu kati ya mama na mtoto wake. Hali hii humuwezesha mama kumtambua mtoto wake kwa haraka, kujibu mahitaji yake kwa wepesi, na kumlinda dhidi ya mazingira hatarishi.
SOMA ZAIDI: Tunawezaje Kuwasaidia Watoto Kujisomea, Kujitayarisha na Mitihani?
Aidha, tafiti zinaonesha kuwa wanawake wanaopitia mabadiliko haya kwa kiwango kikubwa huwa na uwezekano mdogo wa kupata msongo wa mawazo baada ya kujifungua, yaani postpartum depression. Hii ni kwa sababu mabadiliko haya yanasaidia katika utulivu wa kihisia na kuimarisha hisia chanya kwa mama baada ya kujifungua.
Ingawa inaonekana kama jambo la kushangaza, kupungua kwa baadhi ya sehemu za ubongo wakati wa ujauzito ni hatua ya kiasili inayomwezesha mama kuwa mlezi bora kwa mtoto wake. Ni uthibitisho wa jinsi mwili wa mwanamke unavyobadilika kwa njia za ajabu ili kuhakikisha kuwa mtoto anapata uangalizi bora zaidi.
Hivyo basi, badala ya kuhofia mabadiliko haya, wanawake wajawazito wanapaswa kuelewa kuwa ni sehemu ya safari ya kuwa mama, safari inayoleta uhai, upendo, na uhusiano wa kipekee kati ya mama na mtoto wake.
Pia, tunatoa wito kwa jamii na familia kutoa ushirikiano kwa mama mjamzito na yule aliyejifungua ili kumpa muda wa kutulia na kurudisha ubongo wake katika ukubwa wa kawaida, wengi wa wanawake wamekuwa wakibezwa kwa kuwa wasahaulifu bila kujua sababu hasa ya mabadiliko haya katika takriban wanawake wote wanaopitia mcahakato huu.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.