The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Sakata la Simba, Yanga na TFF: Ni Muhimu Serikali Ilinde Mashabiki Kisheria

Ni lazima itafutwe njia ya kudhibiti ufanyaji wa maamuzi yenye athari kwa mashabiki na hilo liwe kisherie ili viongozi wa michezo waache kutumia busara na hekima badala ya sheria na kanuni walizohjiwekea wenyewe.

subscribe to our newsletter!

Mgogoro unaoendelea kati ya klabu ya Yanga SC na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambalo linaimiliki Bodi ya Ligi (TPLB), hautakiwi uishe kimyakimya, bali na fundisho ambalo litachonga njia nzuri zaidi ya uendeshaji mpira wa miguu, usimamizi, uwazi, na uwajibikaji.

Tayari Serikali imeingilia kati sakata hilo lililoanza baada ya mechi baina ya Yanga na Simba kuahirishwa bila ya kuheshimu kanuni kwa hoja kwamba kulikuwa na viashiria vya kuvunjika kwa amani na rushwa. 

Hiyo ni baada ya Simba kudai kuwa haingepeleka timu uwanjani Machi 8, 2025, kutokana na kuzuiwa kufanya mazoezi mepesi siku moja kabla kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Kikanuni, Simba ilikuwa na haki ya kutumia uwanja huo kwa mazoezi mepesi siku moja kabla, lakini haikutoa taarifa kwa wahusika, ambao ni meneja wa uwanja na kamishna wa mechi kama mwongozo wa kanuni unavyotaka.

Kitendo cha kuahirisha mechi saa mbili kabla ya muda wa kuanza mchezo huo kwa kutumia kisingizio cha usalama na rushwa kilipingwa vikali na Yanga, ambayo ilipeleka timu uwanjani licha ya taarifa hiyo ya kuahirisha mechi.

READ MORE: Waliovurunda ‘Dabi ya Kariakoo’ Walazimishwe Kuomba Radhi Hadharani

Na kuonyesha kuwa haikuridhishwa na kitendo hicho, Yanga ilikata rufaa Mahakama ya Kimataifa ya Michezo (CAS), licha ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabuni, kuziita pande zote za kuzungumza nazo kwa nyakati tofauti.

Kuna mapungufu mengi yamejitokeza, yakiwemo kutokuwepo kwa vyombo vya usuluhishi na uamuzi wa migogoro vinavyokubalika, kutoheshimu kanuni, kufanya maamuzi kwa mazoea, kutokuwepo na vyombo tofauti vinavyosimamiana kwa ajili ya utawala bora na kutojali wadau wa michezo na hasa mashabiki.

Nafasi ya mashabiki

Langu nalichukua la mwisho ingawaje yote ni muhimu.

Wakati klabu kubwa za barani Ulaya zilipokubaliana kuanzisha Super League, mashabiki waliongoza kwa kupinga mashindano hayo ambayo yasingetumia sifa ya matokeo ya ndani ya nchi kufuzu mwishoni mwa msimu.

Mashabiki walipinga vikali mashindano hayo na walifanikiwa kuzuia mechi moja ya Ligi Kuu ya England. Mashabiki wa Manchester United waliandaa maandamano nje ya uwanja wa Old Traford na hoteli ya Lowry kabla ya timu hiyo kucheza na Liverpool na kulazimisha mechi hiyo kutochezwa.

SOMA ZAIDI: Kwa Kuifokea Yanga, Karia Ameonesha Upande Kwenye Sakata Kati ya Klabu Hiyo na Simba

Mashabiki hao walifufua vita yao dhidi ya familia ya Glazer inayomiliki hisa zote za Manchester United, baada ya kutangaza kuwa itajiunga na Super League ya Ulaya. 

Hoja yao ilibadilika kuwa hakuwa anajali maslahi ya mashabiki katika kufikia uamuzi wa kujiunga na mashindano hayo ambayo yangekuwa na donge nono kwa timu shiriki, lakini yakishirikisha klabu zenye chapa maarufu kuliko kiwango cha timu kwenye nchi husika.

Hilo liliigusa Serikali ya Uingereza ambayo sasa imewasilisha bungeni muswada ambao utaanzisha ofisi ya mratibu wa mpira wa miguu, ambayo itadhibiti klabu kujiunga na mashindano mapya yasiyoruhusu ushindani ili kuingia, kulinda mashabiki na kudhibiti wamiliki wa klabu kujifanyia maamuzi hovyo, kudhibiti klabu kutobadilisha mambo ya kimsingi nay a kihistoria kama rangi za jezi za nyumbani na mengine mengi.

Hii ni kwa sababu mpira wa miguu nchini Uingeresza ni biashara kubwa inayoajiri watu wengi na kuingizia nchi kipato. Na wanaokuza biashara hiyo ni mashabiki ambao unazi wao kwenye mpira wa miguu haumithiliki.

Uahirishaji hovyo wa mechi

Hakuna shaka kwamba uamuzi wa kuahirisha hovyo mechi ya Simba na Yanga haukuzingatia watu hawa muhimu, na inaonekana wazi tabia hiyo ilishaanza kujijenga kwa wasimamizi wa mpira wa miguu na kuwa utamaduni.

SOMA ZAIDI: Ni Kupoteza Muda Kujadili Kanuni Sakata la Simba, Yanga

Ni mwaka mmoja uliopita TPLB iliahirisha mechi baina ya Simba na Kagera iliyokuwa ichezwe Uwanja wa Kaitaba, ikiwa ni saa mbili kabla ya muda wa kuanza mchezo. Kagera ilifika uwanjani, lakini Simba na waamuzi hawakufika. Simba iliomba iahirishiwe mechi hiyo kwa sababu ilidai ina wachezaji wenye mafua.

Miaka miwili iliyopita, TPLB ilibadili muda wa mchezo baina ya Simba na Yanga bila ya sababu za msingi. Mchezo ulikuwa uchezwe saa 11:00 jioni lakini TPLB ikabadili muda hadi saa 1:00 jioni huku mashabiki wakiwa wameshanza kuingia uwanjani kuanzia asubuhi.

Wiki hii, TPLB imesogeza mbele kwa siku moja, mchezo baina ya Yanga na Tabora United uliokuwa uchezwe Aprili mosi. Hapo ni kwa mechi zinazozihusu Simba na Yanga kwa kuwa ndio zinaangaliwa kwa macho yote, lakini huko kwingine uahirishaji ni jambo la kawaida.

Kurudisha kiingilio, au kutumia tiketi za mchezo ulioahirishwa kuingilia uwanjani siku mechi hiyo inapopangwa upya, si kuwajali mashabiki bali ni kuwadharau. Ni kuona kuwa walichopoteza ni kiingilio tu na si vitu vingine vyenye thamani kubwa zaidi.

Shabiki aliyepanga kutoka Januari kuwa Machi 8 atasafiri kutoka Mwanza kuja Dar es Salaam kuishuhudia mechi hiyo, kwake kiingilio si kitu cha thamani kubwa. Safari ya Mwanza hadi Dar es Salaam ina thamani kubwa zaidi ya hicho kiingilio, achilia mbali malazi na vitu vingine muhimu akiwa safarini na ugenini.

SOMA ZAIDI: CCM Imeongeza Wapigakura Kuzuia Rushwa, Kwa Nini TFF Imewapunguza?

Huyu ni mtu ambaye kama ni muajiriwa, alifanya kazi kubwa kupata  ruhusa ya siku hizo nne, na kama ni mfanyabiashara aliacha shughuli zake chini ya usimamizi wa mtu mwingine. Na mwingine anaweza kufunga biashara kwa siku hizo tatu au nne aione mechi hiyo.

Hasira ya mtu huyo inakuwa kubwa kiasi gani anaposikia eti mechi imeahirishwa. Akiwa pale uwanjani atachukua hatua gani. Huyu anaweza kupiga, au kuchomoa kitu chochote kilicho mbele yake, na kwa kawaida kinachokuwa mbele yake huwa ni viti. Hasira za mashabiki huishia katika kung’oa viti na kuvirusha.

Hawa hawana mtetezi. Hunyanyuka vitini na kuanza kutoka uwanjani wakilalamika, hawajui wapeleke wapi malalamiko ya hasara waliyoingia.

Kama Waziri Kabudi ameona haja ya kuingilia kati suala hilo, basi moja ya vipaumbele vyake iwe ni hawa mashabiki kusumbuliwa na kupoteza mali zao ambazo wangezitumia kuboresha maisha yao lakini wakaamua kupeleka kwenye burudani ambayo haikuwepo.

Sheria maalumu

Serikali haina budi kuliangalia hili kwa umakini na kutengeneza sheria itakayolinda hawa mashabiki na kuweka uwajibikaji kwa waendeshaji wa michezo, ambao sasa wamejawa na kiburi kwa kudhani hawawezi kuingiliwa na yeyote.

SOMA ZAIDI: Kufuta Kadi Nyekundu Haitoshi, Tuanzie Uchunguzi kwa Refa Japhert Smarti

Ni lazima itafutwe njia ya kudhibiti ufanyaji wa maamuzi yenye athari kwa mashabiki na hilo liwe kisheria ili viongozi wa michezo waache kutumia busara na hekima badala ya sheria na kanuni walizohjiwekea wenyewe.

Busara na hekima huwekwa kwenye kanuni ili kuzuia ubinafsi na maslahi binafsi katika maamuzi. Unaposikia kulitumika busara kuokoa mpira wa Tanzania, ujue kuna upande ulinyimwa haki yake ya msingi.

Kwa hiyo, pamoja na Profesa Kabudi kutafuta suluhisho la sakata hilo kabla ya msimu huu kumalizika, suala la kutafuta suluhisho la kudumu liwe kipaumbele na utendaji na ufanyaji maamuzi udhibitiwe kisheria.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×