Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu amefikishwa katika Mahakama ya Kisutu na kusomewa shitaka la uhaini katika moja ya kesi iliyotajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu.
“Kwa kuwa Mahakama hii ya Hakimu Mkazi wa Kisutu haina mamlaka hayo, kwa sababu kesi hiyo inatakiwa isikilizwe na Mahakama Kuu basi suala hilo limetajwa na kwa kuwa Mahakama haina mamlaka na kosa hio halina dhamana, Mwenyekiti wa CHADEMA ndugu Lissu hajapata dhamana na hakuweza kusema lolote kuhusiana na mashtaka hayo,” ameeleza Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Wakili Rugemeleza Nshala.
Hati ya mashtaka inaonesha Lissu anatuhumiwa kosa hilo kutokana na maneno aliyoyasema mnamo April 03, 2025, akiongea na watia nia wa CHADEMA juu ya kampeni ya chama hicho ya ‘bila mageuzi, hakuna uchaguzi’.
Kesi ya uhaini ni moja ya kesi yenye adhabu ya juu kabisa ambayo ni kifo, kesi ya kwanza ya uhaini ni ile ya mwaka 1969, iliyowahusisha baadhi ya wapigania uhuru akiwemo Bibi Titi Mohamed ambapo alishitakiwa pamoja na watuhumiwa wengine akiwemo mwandishi Gray Likungu Mattaka, John Dunstan Chipaka, Eliyah Lifa Chipaka, Michael Kamaliza na William Magori Chacha.
Katika kesi nyingine, Tundu Lissu pia ameshtakiwa kwa makosa ya kuchapisha taarifa za uongo.