Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Amani Golugwa ametoa tathimini ya michango wanayoendelea kuipokea kutoka kwa Watanzania kupitia njia mbalimbali ambapo katika kipindi cha mwezi uliopita wamekusanya Milioni 105. za michango.
Golugwa ameeleza haya akiongea waandishi wa habari leo Aprili 11, 2025, katika ofisi za chama hicho Mikocheni jijini Dar es Salaam. Michango hiyo imekusanywa kupitia benki ya NMB, kiasi cha Sh. 19,717,971; M-PESA (0744 446 969) kiasi cha Sh. 71,487,831; MPESA Digital kiasi cha Sh. 11,300,000; Airtel Sh. 1,633,343 na CRDB Sh. 928,490.
“Tunajisikia Fahari, tunajisikia heshima, tunajisikia kuwajibika kwa watu ambao wanakiongoza chama chao,” ameeleza Amani Golugwa.
Golugwa amefafanua zaidi kuwa michango hiyo imetumika kuendesha mikutano waliyoipanga katika kanda ya Nyasa na Kusini. Chama hicho kimeeleza pia kimepokea michango ya mali ikiwemo mafuta, chakula na malazi kila walipopita.
Golugwa amegusia pia kuhusu kampeni ya, ‘hakuna mageuzi, hakuna uchaguzi’ kuwa sio uasi.
‘Tunahitaji kuyatatua matatizo na dosari za uchaguzi ambazo wote tunaamini kuna mahali patafikia kikomo, wananchi hawataweza kuvumilia tena, hata wanasiasa hawataweza kuvumilia tena.”
One Response
Wanasema siyo UHAINI. Hawajakataa kuhusu uasi, ambayo ina maana tofauti.