The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Haya Hapa Mambo Kumi Yakuyafahamu Kuhusu Papa Francis

Ni pamoja na kunusurika kuuawa mara mbili, pamoja na kufanya kazi za usafi akiwa masomoni kusaidia shughuli za kanisa.

subscribe to our newsletter!

Dunia inaomboleza kifo cha Pope Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, aliyefariki akiwa na umri wa miaka 88, kikitokea Jumatatu ya Pasaka, masaa machache baada ya kiongozi huyo kukutana na kufanya mazungumzo ya faragha na Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance.

Jina lake rasmi likiwa ni Jorge Mario Bergoglio, Papa Francis alichaguliwa kutumikia nafasi hiyo hapo Machi 13, 2013, katika hatua inayotajwa kuwashangaza wafuatiliaji wengi wa Kanisa Katoliki waliokuwa wakimuona kiongozi huyo wa kidini mwenye asili ya Argetina, aliyeguswa sana na watu masikini, kama mtu wa nje.

Kufuatia taarifa za kufariki kwake, The Chanzo inakuwekea hapa mambo kumi, iliyoyapata kutokana na utafiti wa kimtandao, kuhusu Papa Francis ambayo pengine ulikuwa huyajui kuhusu kiongozi huyo mashuhuri wa Kanisa Katoliki duniani.

Mosi, Jorge Bergoglio alikuwa mtaalamu wa kemikali kabla ya kuwa Kasisi. Kabla ya kuingia seminari, Bergoglio alisoma kemia na kufanya kazi kama mtaalamu wa kemikali katika maabara ya sayansi ya chakula huko Buenos Aires, Argentina. Alijishughulisha zaidi na kuchunguza bidhaa za maziwa na viuatilifu—tofauti kabisa na theolojia!

Pili, alikaribia kuuawa mara mbili. Mara ya kwanza ilikuwa ni pale alipokuwa Mkuu wa Jeshi la Wajesuiti. Wakati wa “Vita Chafu” ya Argentina (1976–1983), Bergoglio aliwaficha wanasiasa waliopinga utawala wa kijeshi.Ushujaa wake ulimfanya awe kwenye orodha ya watu wa kuuawa, na alinusurika kwa chupu chupu kutekwa na kuuawa.

Mara ya pili, Bergoglio alikoswa koswa kuuawa na kikundi cha kimafia huko Italia. Ilikuwa mwaka 2015 ambapo vikosi vya ujasusi vya Italia vilimtahadharisha Pope Francis kwamba ‘Ndrangheta, kikundi cha mafia kutoka Calabria, kilikuwa kimezungumza juu ya kumuua kwa sababu ya mageuzi yake ya kupambana na ufisadi katika mifumo ya fedha ya Vatikani.

Jambo la tatu ni kwamba Bergoglio alifanya kazi ya usafi kwa siri alipokuwa akiishi Ujerumani. Inadaiwa kwamba wakati wa kusoma Ujerumani miaka ya 1980, Bergoglio—ambaye tayari alikuwa kasisi—alichukua kazi ya usafi usiku ili kutuma pesa kwa parokia maskini huko Argentina. Aliweka siri hii kwa miongo kadhaa.

Nne, Francis alikuwa Papa wa kwanza kuosha miguu ya wanawake, na Waislamu, wakati wa ibada ya Alhamisi Kuu, akivunja mila ya zamani; kumteua mwanamke kuwa Naibu Katibu wa Jimbo Kuu, Raffaella Petrini, mwaka 2021; na kukubali kubariki watu kwenye ndoa za jinsia moja.

Tano, akiwa na umri wa miaka 21, Bergoglio alipoteza sehemu kubwa ya mapafu yake ya kulia kutokana na maambukizi makali. Madaktari walimtahadharisha kuwa huenda asingekuwa na muda mrefu wa maisha—lakini baadaye akawa Papa akiwa na miaka 76 na akaendelea kufanya kazi licha ya kusumbuliwa na shida ya kupumua za hapa na pale.

Sita, mnamo mwaka 1976, Serikali ya kijeshi ya Argentina iliwataka Wajesuiti wawili kwa nia ya kuwaua. Badala ya kuwafukuza, Bergoglio aliwasaidia kwa siri kukimbilia Brazil, kisha akawadanganya maafisa wa Serikali kwa kusema kwamba watu hao “walitoweka tu.”

Saba, Pope Francis anasifika kwa kuwa mtu asiyependa makuu. Kwa mfano, alikataa kuishi kwenye ghorofa rasmi ya Papa, na badala yake akaishi kwenye nyumba ya wageni ya Vatikani.  

Aliendelea kutumia viatu vyake vyeusi vya Argentina kwa miaka mingi badala ya viatu vyekundu vya kitamaduni vya Papa.  Pia, Papa Francis alimwita mtoto jukwaani wakati wa hotuba, na kumruhusu kuketi kwenye kiti chake, huku yeye akihubiri kutoka sakafuni.  

Nane, sinema ambayo Papa Francis aliipenda zaidi ni Babette’s Feast, sinema inayozungumzia neema na kujitolea, ameielezea kama mfano wa kazi ya Kanisa. Pia, alipenda dansi ya tango, na alipenda pia mashairi ya mshairi wa Kiagertina, Jorge Luis Borges.

Tisa ni kwamba Papa Francis amekuwa akitembea na “Kumbukumbu ya Kifo” mfukoni mwake. Amewahi kuweka wazi kwenye mahojiano yake na vyombo vya habari kwamba yeye hutembea na kipande cha karatasi chenye maneno, “Nitakufa, lakini dhambi zangu zitasalia.” Papa Francis amekuwa akiitafsiri hatua hii kama kichocheo cha toba na unyenyekevu.

Kumi ni kwamba kuna imani kwamba Francis atakuwa ni Papa wa mwisho wa kimila wa Kanisa Katoliki kutokana na mageuzi kadhaa aliyoyatekeleza wakati akihudumu kama kiongozi wa taasisi hiyo yenye nguvu na ushawishi mkubwa duniani.

Mageuzi haya ni pamoja na kupunguza mamlaka ya Vatikani, kukuza uongozi wa waamini wa kawaida, na ukuzaji wa harakati za utunzaji wa mazingira. 

Hatua hizi zimewafanya baadhi ya wanahistoria kubashiri kwamba Francis amebadilisha uongozi wa Papa kutoka kuwa wa “kifalme” na kuwa “shirikishi” zaidi, na kuiweka ofisi ya Upapa kwenye mwelekeo mpya kabisa.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×