Kesi ya kiongozi wa chama cha upinzani CHADEMA, Tundu Lissu, imeendelea leo Mei 06, 2025, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga, ambapo Hakimu huyo ametoa wito kwa Jamhuri kuharakisha upelelezi wa kesi hiyo. Kesi hiyo ya kosa la uhaini iliyosajiliwa kwa shauri la jinai namba 8607 la mwaka 2025, ilianza kwa upande wa Jamhuri kuuliza kama Tundu Lissu amejumuika kwa njia ya mtandao.
“Ahirisho la mwisho ilibainishwa kwamba shauri hili litasikilizwa kwa njia ya mtandao hatujajua status ya mtuhumiwa sasa kama yupo naye amejumuika kwa njia hii au la,” alihoji Wakili wa Jamhuri Thawabu Yahya Issa.
Kamishna Msaidizi wa Magereza na Mkuu wa Gereza la Ukonga Juma Mwaibako akaieleza Mahakama kuwa Tundu Lissu amesema hawezi kupanda Mahakamani kwa njia ya mtandao. Kufuatia majibu hayo, Mawakili wa Jamhuri wakatoa wito kwa Mahakama kuangalia namna ya kutoa amri mshtakiwa kufika Mahakamani.
“Kwa majibu ya Afisa wa Magereza inaonesha amekiuka amri ya Mahakama ya kuhudhuria Mahakama kwa njia ya mtandao, Mahakama sasa inayo wajibu wa kuamua namna gani ya kumuamuru mshtakiwa aweze kufika Mahakamani,” alieleza Wakili Thawabu Yahya.
Na kuongeza: “Lakini kwa leo shauri lilikuwa kwa ajili ya kutajwa upelelezi wa shauri hili bado Mheshimiwa tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.”
Mawakili wa Lissu wakiongozwa na Wakili Mpale Mpoki wakahoji sababu ya upelelezi kuendelea kuchukua muda.
“Nikisoma Charge sheet za particular za offense sioni ni kitu gani kingine mnaendelea kupeleleza, hamuhitaji kwenda forensic, hamuhitaji kwenda kwa ballistic expert, kila kitu kipo. Kitu gani kinachofanya upelelezi uwe kamili, tuambiwe, ili hata sisi, tukienda kwa mteja wetu tumuambie kitu gani kimekwamisha kuendelea kwa upelelezi wa kesi yake,” alisema Wakili Mpoki.
Akijibu hoja hiyo wakili wa Jamhuri alieleza kuwa wanaandaa nyaraka, na watazipandisha mtandaoni muda wowote kuanzia wakati huo, huku akisisitiza ni mambo mengi ya kipelelezi.
“Sentensi ya jumla ni kwamba upelelezi bado na sheria inaturuhusu. Hakuna ambapo tumekiuka kanuni yeyote ya sheria. Upelelezi wa shauri hili bado, utakapokamilika tutapandisha nyaraka kwa mujibu wa taratibu na tutawapatia upande wa pili,” alifafanua tena Wakili wa Jamhuri.
Kesi hiyo ipo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa usikilizwaji wa awali, ambapo baada ya kukumalilika itahamia kwenye Mahakama Kuu ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Katika usikilizaji huo leo Wakili wa jamhuri alipoulizwa tena kueleza ni lini upelelezi utakamilika, alieleza kuwa hakuna sheria inayowalazimisha kueleza wanachokifanya, ambapo Wakili wa Tundu Lissu alioneshwa kutokuridhishwa.
“Kosa hili adhabu yake ni kunyongwa,mteja wetu hana dhamana, yupo ndani. Tukianza kutoa blanket statement [kauli za ujumla] namna hii za kusema kwamba silazimishwi kusema nimefikia upelelezi kiasi gani, inakuwa hatumtendei haki mteja,” alieleza Wakili Mpoki.
“Tuna-deal na maisha ya mtu hapa, serikali ikija na maneno kwamba hakuna sheria inayosema, inakuwa hatuko serious na hii kesi. We are dealing with serious issues, pamoja na hiyo tunazungumzia demokrasia ya nchi, kwa hiyo hatutaki blanket statement kwamba upelelezi ukiwa tayari tutapandisha, lini? hilo ndilo swali,” aliongeza Mpoki.
Wakili Jeremiah Mtobesya akaongezea zaidi juu ya hoja za Wakili Mpoki, kwa kuhoji juu ya ombi la Jamhuri kutaka kesi ihairishwe huku akisisitiza sheria inataka kuwe na sababu rasmi.
“Wanasema ali-intimidate [alitishia] kwa maneno, maneno wameyaweka kwenye charge sheet, mshtakiwa wanaye, sasa unapeleleza nini?” alihoji Mtobesya.
Wakili wa serikali alirudia kusisitiza kuwa hawapo tayari kuweka taratibu za kipelelezi, huku akieleza kuwa sheria inaruhusu Jamhuri kufanya hivyo.
“Wao hakuna walichoomba wanalalamika tu lakini hakuna wanachosema Mahakama ifanye nini sasa, isiahirishe shauri? Sisi tumeomba iwe tarehe nyingine wao wanochoomba nini,” alisema Wakili wa Jamhuri, Thawabu Yahya Issa.
Hoja ya Wakili wa Serikali ikafanya mabishano kupata joto kidogo ambapo Wakili Mpoki alijibu: “Tumesema committal proceeding zifungwe twende High Court tukasikilize, kama hawana karatasi za kutengeneza vitabu vya commital watuambie.”
Committal proceeding hizi ni hatua za awali za usikilizaji wa kesi, kabla haijaenda katika Mahakama Kuu ambapo shauri hilo linakuwa linaenda kusikilizwa rasmi.
Kufuatia hoja ya Wakili Mpoki, Wakili wa Jamhuri akaiomba Mahakama kumtaka Wakili Mpoki kutumia lugha nzuri.
“Mheshimiwa tunaomba Wakili Mpoki atumie lugha nzuri, anaposema kwamba kama hatuna karatasi, sidhani kama ni lugha nzuri kusema. Kwa hiyo tukiomba kwamba atuletee karatasi atatuletea karatasi au atafanyaje? Inakuwa kama tunageuza Mahakama kama mechi ya mpira analeta ushabiki.”
Hakimu Kiswaga akaongea na pande zote mbili na kusisitiza kutumia lugha za kimahakama hasa kwa kuwa shauri linarushwa live, ‘dunia inafuatilia’.Hakimu Kiswaga akatoa wito rasmi wa Jamhuri kueleza upelelezi umefikia wapi.
“Natoa wito kuhakikisha kwamba mnafanya upelelezi wa haraka, tarehe ijayo tupate status mmefikia wapi. Hatuwezi tukawa tu tunaahirisha shauri, tunatoa muda mpaka lini. Tarehe ijayo mtupe status shauri limefikia wapi kwenye upelelezi”
Baada ya hapo Mahakama ikaahirisha shauri hilo mpaka Mei 19, 2025.