Mgodi wa dhahabu wa Geita (GGM) unaomilikiwa na Kampuni ya Uchimbaji Dhahabu ya Geita Gold Mining Limited, uliopo katika eneo la Geita, umekuwa moja ya migodi mikubwa na yenye faida zaidi nchini kwa muda mrefu sasa.
Tangu ulipoanza shughuli zake kama mgodi mkuu mwaka 2000, GGM umekuwa mchangiaji mkuu wa uzalishaji wa dhahabu nchini ambapo kuanzia mwaka 2020 hadi 2024, uzalishaji wa dhahabu nchini Tanzania umeongezeka kutoka tani 47 mwaka 2020 hadi tani 58.1 mwaka 2024.
Hata hivyo, licha ya umuhimu wake katika sekta ya madini, GGM imekuwa kitovu cha mjadala kuhusu mapato yanayotokana na rasilimali hii muhimu na usimamizi wake kwa manufaa ya Taifa.
Tofauti na baadhi ya kampuni nyingine za madini zinazoendesha shughuli zake nchini Tanzania, GGM haijaingia katika mfumo wa ubia na serikali ya Tanzania, ambapo kwenye mfumo huo serikali inatakiwa kumiliki hisa zisizopungua asilimia 16, kama inayoelekezwa na Sheria ya Madini ya mwaka 2010 iliyofanyiwa maboresho 2017 na kuandikiwa upya 2020 na hapo ndipo Kifungu Namba 10 cha Sheria ya hiyo, kiliporekebishwa.
Kwa mwongozo wa kifungu hicho, Serikali na mwekezaji, yaani mchimbaji mkubwa ama wa kati, wanapaswa kuingia kwenye ubia, ambapo hisa za Serikali, za bila malipo na zisizofifishwa, hazipaswi kupungua asilimia 16, zinazosalia ni za mwekezaji.
Hali hii inatofautiana na kampuni kama vile Barrick Gold, ambayo kupitia ubia wake na serikali inayoendeshwa na Twiga Minerals Corporation, imekubali mfumo huu wa umiliki.
Kupitia ushirikiano huu, serikali ya Tanzania inamiliki asilimia 16 ya hisa katika kampuni hiyo, jambo ambalo limehakikisha kuwa serikali inapokea gawio la kila mwaka kutokana na faida inayopatikana. Kwa mfano, katika mwaka wa fedha wa 2019/2020, Twiga Minerals ililipa gawio la TSh bilioni 100 kwa serikali, na katika mwaka wa 2022/2023, malipo hayo yalifikia TSh bilioni 84.
Kutokuwepo kwa ushirikiano kama huu kati ya GGM na serikali kunazua maswali mengi kuhusu mapato ambayo Tanzania inayakosa kutokana na uwekezaji wa mgodi huu mkubwa. Zaidi ya hayo, GGM inaendesha shughuli zake chini ya mkataba wa madini wa mwaka 1999, ambao una masharti tofauti na sheria za sasa za madini, hasa kuhusu masuala ya kodi na umiliki.
Akizungumza na chapisho hili Mwanasheria wa sheria za madini, Clay Mwaifani ameeleza kuwa ni vigumu sana kuingia katika mjadala wa kujua iwapo serikali inanyonywa ama la. Lakini anaeleza kuwa hii inatokana na ukosefu wa uwazi wa katika mikataba mbalimbali ya madini ambayo Tanzania imeingia ukiwamo huu wa GGM.
“Hata hivyo, wengi hatujui kwa nini Serikali na GGM hawajaingia ubia na kuunda kampuni ya pamoja ambapo Serikali itamiliki angalau asilimia 16 ya hisa na kupewa gawio la faida. Wakati Serikali inaingia kwenye ubia uliounda makampuni kama Twiga, Tembo, Nyati, Mamba na Kudu, je, haikuiona GGM? “ anahoji mtaalamu huyu wa sheria.
“Kwa kutoingia ubia na GGM, siyo tu Serikali inajikosesha fursa ya kushiriki kikamilifu kwenye sekta ya madini, bali pia inawanyima Watanzania mapato ambayo ingeyapata kama gawio la faida, mapato ambayo yangetumika kuwaletea wananchi maendeleo.”
Takwimu za mwaka 2016 zinaonesha kuwa Tanzania ni mzalishaji wa nne wa dhahabu barani Afrika, lakini sekta hiyo bado ina mchango mdogo katika pato la taifa kutokana na kiwango cha chini cha makusanyo ya mapato kutoka kwenye kampuni kubwa zinazofanya uzalishaji wa dhahabu nchini licha ya mchango wake kwenye pato la taifa kufikia asilimia 10 kwa sasa.
Ripoti zinaonyesha kuwa ukosefu wa ushiriki wa serikali katika GGM, mgodi unaochangia karibu asilimia 43 ya uzalishaji wa dhahabu nchini, ni jambo linalotia shaka, hasa ikizingatiwa faida kubwa inayopatikana.
Uzalishaji wa madini ya dhahabu Tanzania kuanzia mwaka 2021 hadi 2023.
Kwa kipindi cha miaka 23 (2000–2023), Geita Gold Mining Limited (GGM) ililipa jumla ya takriban dola za Kimarekani bilioni 2.5 kwa serikali ya Tanzania kupitia kodi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mrabaha, kodi ya mapato ya shirika, kodi ya mishahara, na tozo za leseni na bidhaa. Ripoti ya TEITI kwa mwaka wa fedha 2018/2019 inaonyesha kuwa GGM ililipa TZS bilioni 189.4 kwa serikali, ikiwa ni sehemu ya mchango wake mkubwa katika sekta ya madini nchini Tanzania.
Kwa upande mwingine, kampuni ya Twiga Minerals, ubia kati ya Barrick Gold na Serikali ya Tanzania, imekuwa mdau muhimu katika uchumi wa taifa tangu kuanzishwa mwaka 2019. Kampuni hii imetoa gawio la Shilingi bilioni 100 kwa Serikali mwaka 2019/2020 na Shilingi bilioni 84 mwaka 2022/2023. Kwa ujumla, Twiga imewekeza zaidi ya dola za Kimarekani bilioni 4.24 nchini na kufikia mwaka 2024, imelipa dola milioni 888 kwa Serikali. Kwa sasa, Twiga inachangia asilimia 51 ya mapato yote ya Serikali yanayotokana na sekta ya madini, ikidhihirisha nafasi yake ya kipekee katika kukuza uchumi wa taifa.
Hata hivyo, wadau wa sekta ya uziduaji wanaeleza kuwa kwa kuepuka mfumo wa ubia, GGM inaweza kuwa inaendelea kunufaika kwa kiwango kikubwa zaidi, huku wananchi wa Tanzania, hususan wale wanaoishi karibu na maeneo ya uchimbaji, wakikosa manufaa yanayoweza kupatikana kutokana na kutokuwepo kwa ushirikiano wa wazi na wa haki kama anavyoeleza Lucy Shao, Afisa Uchechemuzi na mawasiliano kutoka Hakirasimali.
“Ili GGM aweze kutoa hisa kwa serikali, sheria inayotakiwa kufanya kazi ni Sheria ya Mikataba ya Maliasili na Utajiri wa Taifa (Mapitio na Majadiliano Upya ya Masharti Yasiyo ya Haki) ya 2017. “ anafafanua Shao.
“Siyo tu kwamba GGM haitimizi hicho kifungu cha 10, kuna vifungu anaweza asivitimize kwa sababu mkataba wake, au makubaliano yake na serikali hayako hivyo, tukumbuke kuwa mkataba wake ulikuwa kabla ya sheria hii ya sasa.”
Shao anasisitiza kuwa GGM kuingia ubia na serikali siyo jambo la siku moja kwa sababu sheria haifanyi kazi kwa kurudi hadi pale ambapo serikali itaamua kufanya majadiliano.
Mkataba wa Madini wa GGML wa 1999
Mnamo tarehe 24 Juni 1999, Geita Gold Mining Limited (GGML) na wanahisa wake waliingia katika Mkataba wa Maendeleo ya Mgodi wa Dhahabu (Gold Mine Development Agreement – MDA) na Serikali ya Tanzania.
Wakati huo, sekta ya madini nchini Tanzania ilikuwa chini ya sheria tofauti, hasa Sheria ya Madini ya mwaka 1998, ambayo iliibadilisha Sheria ya Madini ya mwaka 1979. Sheria ya mwaka 1998 ililenga kuhamasisha uwekezaji binafsi katika sekta ya madini kwa kutoa masharti yanayovutia kwa wawekezaji, kama vile kiwango cha chini cha mrabaha wa asilimia 3 kwa madini (asilimia 5 kwa almasi) na kodi ya mapato ya asilimia 30.
Miongoni mwa vifungu muhimu katika MDA ya mwaka 1999, vililenga kuhakikisha kuwa mazingira ya kodi kwa GGML yanabaki thabiti kwa muda wote wa uhai wa mgodi. Kwa mfano, kifungu cha 4.2 cha MDA kilieleza kuwa sheria iliyokuwa inatumika kwa masuala ya kodi ya mapato ilikuwa ni Sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 1973.
Kwa upande wa umiliki, wakati mkataba wa mwaka 1999 uliposainiwa, serikali haikuwa na sharti la umiliki wa hisa katika kampuni za madini. Hali ya umiliki wa GGML imepitia mabadiliko kadhaa tangu wakati huo.
Mwaka 1999, Ashanti Goldfields Company Limited ilipata mgodi huu, na mwaka 2004, AngloGold Limited ya Afrika Kusini iliichukua Ashanti, na kuunda AngloGold Ashanti (AGA), ambayo baadaye ilisimamia GGML. Hivyo, GGML kwa sasa ni kampuni tanzu inayomilikiwa kabisa na AngloGold Ashanti Limited.
“Hili ni suala la majadiliano tu kati ya serikali na hawa wawekezaji kwenye migodi yetu”, anaeleza Silas Olang ambaye ni mshauri wa sera kanda ya afrika kutoka shirika la NRGI.
“Mifano ni mingi sana, kwa mfano Botswana, walianza kidogo hadi sasa wamefikia hadi asilimia 50% na ile kampuni. Ni jambo ambalo linalowezakana kabisa kama serikali ikiamua kulifanyia kazi,” anaongeza.
Sheria ya Madini ya mwaka 2017 ilileta mabadiliko makubwa katika usimamizi wa sekta ya madini nchini Tanzania. Aidha ilipa serikali uwezo wa kukagua na kujadiliana upya mikataba ya madini iliyopo ambayo inaweza kuonekana kuwa na masharti “yasiyofaa” au ambayo hayazingatii maslahi ya Watanzania. Masharti yasiyofaa yanajumuisha yale yanayozuia mamlaka ya serikali juu ya rasilimali zake au yanayoiweka nchi chini ya sheria za kigeni au mabaraza ya kimataifa.
Mfano mzuri wa ufanisi wa umiliki wa serikali katika sekta ya madini nchini Tanzania ni Twiga Minerals Corporation. Twiga Minerals ni ubia kati ya serikali ya Tanzania na Barrick Gold Corporation, ulioanzishwa baada ya Barrick Gold kukubali masharti mapya ya uwekezaji nchini. Serikali ya Tanzania inamiliki asilimia 16 ya hisa katika kila moja ya migodi ya dhahabu inayoendeshwa na Twiga Minerals, ambayo ni North Mara, Bulyanhulu, na Buzwagi.
Ushirikiano huu umewezesha serikali kupokea gawio kubwa. Tangu kuanzishwa kwake, Twiga Minerals imechangia zaidi ya dola bilioni 2.8 za Marekani kwa uchumi wa Tanzania kupitia kodi mbalimbali, ada, gawio, mishahara, na malipo kwa wauzaji wa ndani.
“Mbinu ni moja tu hapa, serikali imekuwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia na Afrika Kusini, na mazungumzo tu haya yanayitakiwa. Nafikiri Tanzania ianze kununua hisa kidogokidogo tu mwishoni wa siku itakuwa na ubia, ni jambo linalowezekana,” anaeleza Mwaifani akirejelea kuwa serikali kupitia Shirika la Taifa la Madini (STAMICO) inaweza kufanikisha uwekezaji.
Barack Thomas ambaye ni mtaalmu wa sheria kutoka Tanzania Trade and Investment Coalition (TATIC) anasema kwa GGML kutoingia ubia na serikali wakati kampuni nyingine zikifuata sheria hiyo ni kiashiria cha ukosefu wa usawa katika sekta hiyo, hali ambayo inaweza kulisababisha taifa kuingia kwenye migogoro ya kiuchumi na kijamii siku za usoni.
“Kuna shida hapo, kwa sababu baadaye inaweza kulifanya taifa kuingia kwenye mgogoro. Maana ni kama hakuna usawa katika uwekezaji. Haiwezekani muwe wawekezaji kwenye taifa moja na sekta moja, lakini bado mmoja ananufaika zaidi kwa hiki, na mwingine kwa kile – hiyo siyo sawa kabisa,” alisema Thomas.
Akiangazia suala la mapato na maslahi kwa serikali, Thomas alieleza kuwa haiwezi kusemwa moja kwa moja kama taifa linapoteza au la, kwani hali hiyo inahitaji uchambuzi wa kulinganisha mikataba na matokeo yake kwa taifa.
“Siwezi kusema moja kwa moja kuwa serikali inapoteza au haipotezi, kwa sababu hapo lazima ufanyike uchambuzi wa kulinganisha,” aliongeza.
Katika hoja nyingine, Thomas alihoji kimya kinachoizunguka kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), akifananisha na hatua kali zilizochukuliwa dhidi ya Acacia Mining hadi kuundwa kwa ubia wa Twiga Minerals.
“Kuna maswali yanayotafakarisha. Kama ilitungwa sheria ya kuanzisha majadiliano mapya ya mikataba, na serikali ileile ikawa na ujasiri wa kuigusa Acacia hadi kuundwa kwa Twiga, kwa nini haikugusa GGML? Kwa nini hakuna taarifa yoyote inayoeleza kuhusu GGML?” alihoji kwa msisitizo.
Kwa upande wake, CAG mstaafu, Mkurugenzi Mtendaji wa Wajibu Institute na Mwenyekiti wa Bodi ya Tanzania Extractive Industries Transparency Initiative (TEITI) Ludovick Utoh anasisitiza kuwa serikali kutoingia ubia na GGML kuna uwezekano mkubwa wa kupoteza mapato muhimu ambayo ingeyapata endapo ingekuwa na ubia.
“Uhalisia ni kwamba serikali inapoteza mapato, hilo halina ubishi,” anasema. “Iwapo serikali ingekuwa mshirika wa moja kwa moja katika umiliki, maana yake ni kwamba baada ya kodi, kile kinachobaki kingegawanywa kati ya wamiliki ambapo serikali nayo ingepata sehemu yake kama mshirika.”
“Kwa sasa kinachobaki baada ya kodi ni faida kwa wawekezaji binafsi pekee, na si faida ya moja kwa moja kwa serikali kama mmiliki mwenza” anaongeza.
Mapato ya dhahabu nchini Tanzania kwa mwaka 2021 hadi 2024.
Utoh anatahadharisha kuwa hali hii inaweza kusababisha mvutano katika siku za usoni, hasa ikizingatiwa kuwa sheria za kimataifa zinataka kuwe na usawa wa kisheria kwa kila mwekezaji, jambo linaloweza kuwa changamoto endapo ushiriki wa serikali hautawekwa bayana na kwa uwazi.
“Kikawaida, kila mwekezaji anatakiwa apewe huduma au mazingira ya uwekezaji yanayolingana. Sasa pale ambapo mwekezaji mmoja anapendelewa kwa namna fulani, lazima jambo hilo lizue maswali. Wakiamua kuliibua, linaweza kusababisha mvurugano usiokuwa wa lazima.”
Mkataba wa Madini wa GGML wa mwaka 1999 una uwezekano mkubwa wa kujumuisha vifungu vya uthabiti wa sheria (stabilization clauses), ambavyo vinalenga kulinda wawekezaji dhidi ya mabadiliko yasiyotarajiwa katika sheria au kanuni baada ya mkataba kusainiwa. Vifungu hivi vinahakikisha kuwa masharti ya mkataba yanabaki sawa kwa muda wote wa uhai wa mradi, bila kujali mabadiliko yoyote ya sheria yanayoweza kupitishwa na serikali.
Mazungumzo Kati ya Serikali na GGML Kuhusu Umiliki
Licha ya sheria ya mwaka 2017 kuweka sharti la umiliki wa asilimia 16, utekelezaji wake kwa GGML haujaanza kutokana na mazungumzo yanayotajwa kuendelea kuhusu uwezekano wa kujumuisha umiliki wa serikali au kurekebisha mkataba uliopo.
Hata hivyo, akizungumza na mwandishi wa makala hii, mkuu wa kitengo cha mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina Bw. Sabato Kosuri ameeleza kuwa juhudi za kufanya majadiliano na GGML zinaendelea.
“Serikali inaendelea na majadiliano kwa mujibu wa sheria ya madini na kanuni zake. Majadiliao haya yapo kwenye hatua za mwisho za ukamilishaji” anaeleza Kosuri.
Juhudi za kupata maoni kutoka kwa GGML hazikufanikiwa baada ya Afisa Mahusiano wa kampuni hiyo, Rhoda Lugaziya, kueleza kwa kifupi kuwa hayuko tayari kuzungumza kuhusu jambo hilo na wala hakuna haja ya kufanya hivyo.
Matonyinga Makaro ni mwandishi wa kujitegemea kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anaweza kupatikana kupitia matonyingamakaro@gmail.com.
*Makala hii imeandaliwa kufuatia programu ya mafunzo ya uandishi wa habari ambayo Makaro alishiriki. Mradi huu ulipata msaada kutoka Thomson Reuters Foundation kupitia Media Foundation for West Africa, kama sehemu ya juhudi zake za kimataifa za kuimarisha jamii huru na zenye haki ya kupata taarifa sahihi. Msaada wowote wa kifedha au wa aina yoyote uliotolewa kwa mwandishi haukuwa na ushawishi wowote wa kiuhariri. Maudhui ya makala hii ni mali ya mwandishi pekee na hayahusiani wala kuidhinishwa na Thomson Reuters Foundation, Thomson Reuters, Reuters, wala mashirika mengine yoyote yanayohusiana nayo.