Akizungumza leo katika uzinduzi wa sera mpya ya mambo ya nje toleo la 2024, Rais Samia Suluhu ameonya juu ya wanaharakati kutoka nje wanaoingilia mambo ya Tanzania.
“Tumeanza kuona mtiririko au mwenendo wa wanaharakati ndani ya region yetu hii kuanza kuvamia na kuingilia mambo yetu huku, sasa kama kwao wameshadhibitiwa wasije kutuharibia huku. Tusitoe nafasi, walishaharibu kwao, walishavuruga kwao; nchi iliyobaki haijaharibika watu wako na usalama na amani na utulivu ni hapa kwetu,” alieleza Rais Samia.
“Kuna majaribio kadhaa, niwaombe sana vyombo vya ulinzi na usalama na nyinyi wasimamizi wa sera zetu nje. Kutokutoa nafasi, kwa watovu wa adabu wa nchi nyingine kuja kutovuka hapa kwetu. Nimeona clip kadhaa za kunisema niko bias na nini; ninalofanya ni kulinda nchi yangu na ndio wajibu niliopewa. Kwa hiyo hatutatoa nafasi kwa kiumbe yeyote kuja kutuvurigia hapa; awe yupo ndani au anatoka nje hatutatoa hiyo nafasi,” aliongeza zaidi.
Rais Samia ameyaongea haya leo ikiwa kuna wanaharakati kadhaa waliozuiliwa kuingia Tanzania, sehemu kubwa walikua wakija kuhudhuria kesi ya uhaini inayomkabili kiongozi wa CHADEMA, Tundu Lissu. Baadhi ya wanaharakati hao ni pamoja na Jaji Mkuu wa zamani wa Kenya Willy Mutunga,Kiongozi wa chama cha Kenya’s People’s Liberation Party (PLP), Martha Karua pamoja na mwanasheria Gloria Kimani na Lynn Ngugi.
Wanaharakati Boniface Mwangi kutoka Kenya na mwanasheria Agather Atuhaire kutoka Uganda wamekamatwa na polisi.