Dodoma. Tatizo la ndoa za utotoni linaendelea kuiumiza kichwa Serikali pamoja na wadau mbalimbali, hasa wakifikiria ni kwa namna gani watalitatua katika wakati huu ambao inaelezwa kuwa jamii imekuwa ikighushi vyeti vya ndoa ili kufanikisha adhma ya kuwaozesha watoto wenye umri chini ya miaka 18.
Kitendo cha vyeti vya ndoa kughushiwa kimekuwa kikizifanya mamlaka na wadau kukwama kutekeleza jukumu la kuzuia na kuchukua hatua dhidi ya vitendo hivyo, baada ya kuthibitishiwa kupitia cheti kuwa aliyeozeshwa amefikia umri sahihi wa kuolewa.
Moja kati ya eneo ambalo tatizo hili limeonekana hapa nchini ni huko katika wilaya Kondoa iliyopo mkoani Dodoma, ambapo Afisa Ustawi wa halmashauri ya Kondoa Mji, Khadija Abdallah, Machi 6, 2025, alikiri kuwa jamii kwenye halmashauri hiyo imekuwa ikifanya vitendo hivyo, japo kuwa siyo kwa kiasi kikubwa sana.
“Unakuta unaambiwa mtoto ni mdogo anayeoolewa, ukienda [kusitisha unakuta] wameshaghushi cheti cha ndoa anaonekana ni mkubwa na wameandika miaka 18,” Khadija anasema.
Afisa huyo anaeleza kumekuwa hakuna ushirikiano baina ya jamii na mamlaka katika kupambana na udanganyifu kwenye vyeti vya ndoa, hali ambayo imekuwa ikirudisha nyuma jitihada za kulimaliza tatizo hilo.
“Unakuta cheti cha ndoa kimeandikwa miaka mikubwa, ukija kuona hata sura ya hiyo miaka hana, au unaomba taarifa za shule unapata taarifa ya miaka kuwa midogo. Au unaomba kadi au cheti cha kuzaliwa unakuta miaka midogo.”
Kutokana na uwepo wa hali hiyo Khadija amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanaendelea kutoa elimu kwa jamii ili iachane na vitendo hivyo kwani havina afya kwa ustawi wa watoto wa kike.
SOMA ZAIDI: Sensa 2022: Ndoa Zimeongezeka Kidunchu, Talaka, Kutengana Juu
“Mara nyingi tunakuja kukuta mtoto amejifungua akiwa na miaka 16, 17, ukimuuliza anasema ameoolewa. Elimu imeendelea kutolewa ili jamii iachane na vitendo hivyo, na sisi tukiambiwa kwamba kuna harusi kama hiyo tunawahi kabla haijafungwa, tunaizuia.”
Machi 2025 The Chanzo ilifunga safari hadi kata ya Thawi iliyopo Kondoa vijijini. Lengo la safari hiyo ilikuwa ni kwenda kuzungumza na jamii lakini pia kuona hali halisi ya jinsi ndoa za utotoni na vitendo vya kughushi vyeti vya ndoa vinavyofanyika.
Safari ya kufika huko hakikuwa nyepesi, nikiongozana na mwenyeji wangu kwa kutumia usafiri wa bodaboda mara baada ya kufika Kondoa mjini tulianza kuzipunguza kilomita tukielekea kwenye kata hiyo.
Hali ya barabara haikuwa nzuri, ilikuwa imejaa mashimo na mawe lakini pia tulipanda milima ya kutosha na kupita katika mabonde mengi. Kuna wakati nilitamani kuairisha safari hiyo kutokana na ugumu wake, mwisho nikajipa moyo mpaka tukafanikiwa kufika tulipotaka.
Nikiwa kwenye kata hiyo nilikutana na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Tanzania (KKKT), Usharika wa Kondoa Mji na Mkuu wa Jimbo la Kondoa, Eliezer Mbwambo, ambapo kanisa lake ni moja ya sehemu ambayo watu wamekuwa wakifunga ndoa.
Mchungaji Mbwambo alinieleza kuwa ameshawahi kukutana na tukio la watu kutaka kufunga ndoa, sasa ulipofika wakati wa kuchukua taarifa zao ili kuweza kukamilisha suala hilo alibaini binti ana umri chini miaka 18.
“Mwaka juzi wako vijana waliifika ofisini kwangu wanataka kuandikisha ndoa. Nilipouliza umri kama msajili wa ndoa nikakuta kijana anayetaka kuoa ana miaka 19, na msichana anayetaka kuoelewa ana miaka 17.”
Mbwambo anaendelea kusema, “kwa kweli nilikataaa kuandikisha ile ndoa na niliwarudisha. Na niliwaita wazazi wao nikazungumza nao, kwamba hawa bado ni watoto wasubiri ule umri unaotakiwa kisheria.”
Mbwambo ameeleza kuwa kanisa litaendelea kutoa mafundisho ili watu wazingatie umri sahihi wa watu kuoa na kuolewa.
“Wazazi wasiozeshe watoto kwa tamaa za mahari au mali. Waozeshe watoto kwa umri unaotakiwa, ili wasije wakawaletea shida. Kwa sababu tunafahamu kuwa mtoto wa kike anapoolewa chini ya umri kuna matatizo kiafya, kwa sababu bado anakuwa hajakomaa.”
SOMA ZAIDI: Ndoa za Utotoni Zinavyowanyima Fursa Mabinti Kutimiza Ndoto Zao
Sehemu nyingine ambayo ndoa zinafungishwa ni kwenye misikiti, ambapo
Ayubu Salim, Imamu wa Msikiti wa Thawi yeye aliiambia The Chanzo kuwa amekuwa akiwaelimisha waumini wake wasiwe wanaozesha watoto katika umri mdogo, kulingana na madhara ambayo yatawakumba.
Tunashindwa kuwasaidia
Mratibu wa Mtandao wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni Tanzania (TECMN), Lilian Kimati, ameiambia The Chanzo kuwa katika shughuli zao za kupambana na ndoa za utotoni kipindi cha nyuma wamewahi kukutana na changamoto ya watu kugushi vyeti vya ndoa katika mkoa wa Dodoma.
“Tuliungana na wadau na viongozi wengine wa Serikali, pamoja na wasichana kwa ajili ya kuendelea kupinga vita dhidi ya ndoa za utotoni hususan kwenye kughushi vyeti vya ndoa kidogo hali ikatulia,” anasimulia Lilian. “Sasa naona imerudi tena kwa mujibu wa taarifa unazoniambia.”
Lilian akaeleza kuwa vitendo vya kughushi vyeti vya ndoa vinakwamisha jitihada za mapambano dhidi ya suala hilo licha ya elimu kubwa ambayo wamekuwa wakiitoa kwa jamii juu ya athari za ndoa za utotoni.
“Cheti cha Serikali ni nyaraka ya Serikali kwa mujibu wa Serikali,” Lilian anasema. “Kama kuna cheti cha Serikali kimesainiwa, kwa hiyo huyu mtoto wa kike unakuta tunashindwa kumsaidia kwa sababu cheti cha Serikali kinaidhinisha huyu kwamba ameolewa kihalali. Na si mwanafunzi, yupo juu ya umri wa miaka 18.”
“Hapo labda mtoto mwenyewe atupe ushahidi kwamba hivi vitu vimeghushiwa pamoja na ushirikiano mzuri na wazazi. Lakini pale mtoto wa kike anapokaa kimya, mwisho wa siku tunashindwa kumsaidia huyu mtoto kisheria labda tufanye uchunguzi wa ndani zaidi.”
Nikiwa katika kata ya Thawi nilikutana na Saumu Heri, ambaye alinieleza kuwa aliolewa mwaka 2008, wakati huo akiwa na miaka 17.
Kitendo cha Saumu, 34, kuolewa katika umri mdogo kimemuachia kumbukumbu ambazo hawezi kuzisahau. Moja ya kumbukumbu hizo ni kitendo cha mtoto wake wa kwanza kupoteza maisha baada ya kushindwa kujifungua kwa njia ya kawaida kutokana kupata ujauzito akiwa na umri mdogo, ambapo nyonga zake zilikuwa bado hazijatanuka.
Baada ya kufanikiwa kupata watoto wawili, hali ya ndoa yake ilibadilika baada ya mume wake kuacha kutimiza majukumu yake hali iliyopelekea ndoa yao kuvunjika.
“Mume akawa hahudumii familia kama inavyotakiwa,” anasema Saumu. “Nililazimika kukata mkaa ili nitunze watoto licha ya kuwa nina mume. Niliendelea na maisha yale, nikaona kwamba ninaumia peke yangu ni bora niishi peke yangu, nikaomba talaka.”
SOMA ZAIDI: Tunawezaje Kujenga Jamii Yenye Mtazamo Chanya Kwa Wanawake wa Makundi Maalumu?
“Maisha ya ndoa katika umri mdogo sikuweza kuyamudu,” Saumu anaendelea kusimulia. “Napenda kuwaambia wanangu, wasije wakapita maisha ambayo nimepita mimi. Wakazane kusoma ili wajikomboe, siwezi nikakubali mimi sijasoma wanangu wasisome. Nitapambana kwa hali ya yoyote maana elimu ndiyo ufunguo wa maisha.”
Tatizo linapungua
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), tatizo la ndoa za utotoni hapa nchini limekuwa likipingua katika miaka ya hivi karibuni.
Shirika hilo linaeleza kuwa takribani asilimia tano ya wanawake wenye umri wa miaka 20 hadi 24 hapa nchini waliolewa kabla ya kufikisha miaka 15, ambapo idadi yao ni takribani wanawake milioni 1.4.
UNICEF inaendelea kubainisha kuwa takribani asilimia 29 ya wanawake wenye umri wa miaka 20 hadi 24 waliolewa kabla ya kufikisha miaka 18, ambapo idadi yao ni takribani wanawake milioni 6.4.
Hata hivyo, UNICEF inabainisha kuwa tatizo wanawake kuolewa wakiwa chini ya umri wa miaka 18 hapa nchini limekuwa likipungua tangu mwaka 2007. Kwa mwaka huo asilimia za tatizo hilo ilikuwa ni 37.0, mwaka 2012 ilikuwa ni asilimia 31.2, mwaka 2017 ilikuwa ni asilimia 29.8 na mwaka 2022 ilikuwa ni asilimia 29.1.
UNICEF inaitaja mikoa ya mikoa ya Shinyanga, Tabora na Dodoma kuwa ndiyo vinara kwa kuwaozesha watoto kabla hawajafikisha miaka 18.
Hatuna taarifa
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Mtoto kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mathias Haule, ameiambia The Chanzo kuwa wizara hiyo haina taarifa za watu kughushi vyeti vya ndoa ili waweze kuozesha watoto wenye umri chini ya miaka 18.
“Suala la kufoji vyeti vya ndoa halina uhusiano wa moja kwa moja na ndoa za utotoni, kwa sababu wanaofanya hivyo watakuwa wanataka kupata nafuu fulani katika kujipatia kipato kwa udanganyifu,” aanasema Haule.
“Hivyo, suala hilo ni jinai na inatakiwa kudhibitiwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), ambao ndiyo wenye dhamana ya kufuatilia uhalali wa vyeti hivyo, ingawaje hata kufuatilia ni ngumu kwa sababu watoaji wa vyeti via ndoa ni wengi.”
Haule ameeleza kwamba ili kukabiliana na tatizo hilo ni vyema mifumo ya utoaji wa vyeti vya ndoa ikahuishwa na wadau wakubwa ambao ni Serikali kupitia ofisi za wakuu wa wilaya.
Mkurugenzi wa Utetezi wa Taasisi isiyokuwa kiserikali ya TWAWEZA Afrika Mashariki, Annastazia Rugaba, ameiambia The Chanzo katika shughuli zao wamewahi kukutana na tatizo la kughushi umri wa cheti cha ndoa huko maeneo ya Tabora.
Annastazia ameeleza kuwa jamii inafanikisha kughushi vyeti vya ndoa kwa sababu watu wengi hawana vyeti vya kuzaliwa. Katika hali hiyo inaweka ugumu wa kuthibitisha kuwa anayeolewa ana umri chini ya miaka 18.
SOMA ZAIDI: Utajuaje Kama Mwanao Anafanyiwa Ukatili wa Kingono?
“Yaani unakuta mtoto hana cheti cha kuzaliwa, wakiandika miaka 18 hata mkitilia mashaka mkashitaki mkasema huyu mtoto hana miaka 18 inakuwa ngumu kuingilia kati. Ukikosa cheti cha kuzaliwa ni rahisi sana kwa jamii kughushi umri wa watoto na kupelekea ndoa za utotoni,” anasema Annastazia.
Madai ya Annastazia yanaweza kuthibitishwa na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2023/2024 inaonyesha kuwa ni Watanzania watatu kati ya 10 pekee ndiyo wamesajiliwa na kupewa vyeti vya kuzaliwa, huku saba wakiwa hawana taarifa za kuzaliwa zao.
“Hata kama mtu akichana cheti chake cha kuzaliwa, au akikichoma ili kusudi aweze kughushi kwenye cheti cha ndoa, basi tuwe tuna uhakika wa kuchungulia kwenye mifumo ya RITA.”
“Na tukiweza kuangalia kwenye mifumo ya RITA, tutamkuta huyu mtu mbona ameandika cheti cha ndoa ana miaka 18, lakini kwenye cheti chake cha kuzaliwa kwa mujibu wa takwimu za RITA anaonekana ana miaka 15. Tukiweza kutatua hili tatizo la kuwapa watoto vyeti itapunguza hiyo shida ya ndoa za utotoni,” Annastazia anamalizia kusema.
Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana mkoani Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jaquelinevictor88@gmail.com