Katika taarifa ya hali ya ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi iliyowasilishwa katika taarifa ya bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ya mwaka 2025/26 leo Mei 20, 2025, Tanzania imeeleza kuwa kumekuwepo na tishio la kiusalama katika mpaka wa Tanzania na Uganda kutokana na mgogoro wa kimpaka.
“Hali ya usalama katika mpaka huu wenye urefu wa kilomita 397.8 ni shwari. Hakuna tukio la kuhatarisha usalama wa nchi yetu,” ilieleza ripoti hiyo ya Wizara.
“Pamoja na hali hii, kumekuwepo na tishio la kiusalama linalotokana na Mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Uganda. Pamoja na jitihada za kumaliza mgogoro huu, bado serikali ya Uganda inaendelea kudai kuwa mpaka wake na Tanzania katika eneo la Kagera unapita katika 01° kusini mwa ikweta badala ya marundo ya mawe yaliyopo,” taarifa hiyo inaeleza.
Wizara ilieleza zaidi kuwa mazungumzo yanaendelea chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi