The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

‘G – 55’ Ndani ya CHAUMMA Mpya: Nani Yuko Kwenye Usukani?

Wakati CHAUMMA mpya ikionekana imepata rasilimali mpya za kuwawezesha kufanya kazi hapa na pale, mijadala ya wananchi inaonesha chama hicho kina mlima mrefu wa kupanda kuwaaminisha Watanzania kuwa kina imani ya dhati katika siasa. 

subscribe to our newsletter!

Gumzo linaendelea kwenye vijiwe vya siasa juu ya muujiza ulioonekana kutokea katika chama cha siasa cha CHAUMMA; kutoka kwenye kushindwa kuendesha mkutano wa ndani kwa kukosa fedha mpaka kuweza kukodisha kumbi katika hoteli kubwa na kusafirisha mamia ya watu kutoka mikoani.

Muujiza huu umetokea baada ya waliowahi kuwa viongozi wa CHADEMA na wale wa kundi la  ‘G – 55’ kupokelewa rasmi CHAUMMA wakati wa kikao cha halmashauri kuu ya chama hiko kilichofanyika Mei 19, 2025, katika ukumbi wa hoteli ya Golden Tulip jijini Dar es Salaam.

Katika kikao hiko cha halmashauri kuu ya CHAUMMA waandishi waliopiga kambi ukumbini hapo siku hiyo baada ya mwaliko ikiwemo wa The Chanzo, walishuhudia kuwa licha mkutano huo kuwa ni wa CHAUMMA ila waliohusika kufanya shughuli za uratibu walikuwa ni kundi la viongozi waliokuwa wanahamia siku hiyo.

Katika jambo ambalo liliibua minong’ono ni pamoja na kushuhudiwa kwa watu wa karibu wa Mwenyekiti wa zamani wa CHADEMA Freeman Mbowe akiwemo mlinzi wake mkuu Khalfan Bwire wakionekana kuwa mstari wa mbele katika uratibu wa tukio la siku hiyo lililoshuhudia CHAUMMA kupokea kundi la wanasiasa wapya. 

Licha ya watu wa karibu wa Mbowe kuonekana siku hiyo, kilichoshangaza zaidi ni pale ambapo hata kadi za uanachama za wanachama waliojiunga na CHAUMMA pamoja na fulana za CHAUMA kuonekana kuletwa na mmoja wa wageni hao kutoka CHADEMA ambaye aliwasili mapema kabla ya kikao cha halmashauri kuu ya CHAUMMA hakijaanza. 

Katika kikao hicho baadhi ya viongozi wa CHAUMMA walitangaza kujiuzulu na kisha baadae wanachama wapya waliweza baada ya kukabidhiwa kadi walipatiwa nyadhifa mbalimbali. Ambapo Katibu Mkuu wa CHAUMMA, Mohamed Masoud, alijiuzulu na nafasi yake ikachukuliwa na Salumu Mwalimu, Masoud akabaki kuwa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar. 

Naibu Katibu Mkuu Bara, Rahman Rungwe, alijiuzulu na nafasi yake ikachukuliwa na Benson Kigaila, na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Kayumbo Mohamed, pia alijiuzulu na nafasi yake ikachukuliwa na Devotha Minja.

Nani yuko kwenye usukani?

Funga mechi kuhusu CHAUMMA ilikua ni mkutano walioufanya mnamo Mei 21, 2025 katika ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam, ukumbi unaochukua watu takribani 1,000,. Chama hicho kiliweza kuwaleta watu waliowatambulisha kama wanachama wapya kutoka mikoa mbalimbali, kikiwalipia usafiri na malazi. 

Mkutano huo umeibua maswali mengi, hasa juu ya gharama za kuuandaa, watu wakihoji vyanzo vyake. CHAUMMA yenyewe imesisitiza kwamba hizo ni fedha kutoka kwa “wadau” wake. Lakini pia Katibu Mkuu mpya wa chama hicho, Salumu Mwalimu, alitangaza chama hicho kitazunguka mikoa 16 kwa helikopta kujinadi kwa wananchi, hoja iliyowaacha wengi katika butwaa juu ya muujiza uliotokea.

“Naomba niwatangazie rasmi ya kwamba kuanzia tarehe 30 mwezi wa tano, siku ya Jumamosi, tutazindua operesheni kubwa inayoitwa C4C Tusonge Mbele,” alieleza Salum Mwalimu. “Tutakwenda mikoa yote ndani ya siku 16, mikoa yote ndani ya siku 16, maana yake ni chopa juu.”

CHAUMMA iliyokua na makao yake katika ofisi binafsi za Mwenyekiti wake, Hashim Rungwe, Kijitonyama, Dar es Salaam, tayari inategemewa kuhamia katika eneo lingine. Mabadiliko haya ya haraka haraka na ya gharama kubwa yanaendelea kuzua maswali, hasa kwa kuwa chama hicho kinafahamika kuwa hakina wanachama wengi.

“CHAUMMA, chini ya Mwenyekiti Hashimu Rungwe Sipunda, wamepata wapi fedha ya kupiga kampeni, au kujinadi, kutangaza chama chao siku 16 kuanzia tarehe 30 mwezi wa tano wakitumia chopa?” anauliza Abel Majiko mfanyabiashara katika Soko Kuu Dodoma alipohojiwa na The Chanzo kuhusu namna wananchi wanavyolichukulia suala la wanasiasa kuhama hama vyama.

“Nyuma yao mimi nina imani yupo mkubwa wao, na nadhani ndiye atakayegombea Urais kwa CHAUMMA, siwezi kumtaja ni nani, lakini nyuma yao kuna mkubwa wao,” aliongeza zaidi Majiko.

Sehemu kubwa za pilika pilika za G-55 zinazofanyika zimekuwa zikihusishwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa zamani wa CHADEMA, Freeman Mbowe. Hii ni baada ya watu wake wa karibu, ikiwemo wasaidizi wake wa moja kwa moja, kuwa vinara katika maandalizi na shughuli za CHAUMMA. 

Baadhi ya watu waliosafirishwa kutoka mikoa mbalimbali kuhudhuria mkutano wa CHAUMMA Dar es Salaam wameripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari kudai kuambiwa kuwa walikuwa wanakwenda kwenye kikao kilichoitishwa na mwenyekiti huyo wa zamani wa CHADEMA. Hadi sasa Mbowe mwenyewe hajakanusha wala kuthibitisha madai haya hadharani.

Kutokuaminika na wananchi

Wakati CHAUMMA mpya ikionekana imepata rasilimali mpya za kuwawezesha kufanya kazi hapa na pale, sehemu kubwa ya mijadala ya wananchi inaonesha chama hicho kina mlima mrefu wa kupanda kuwaaminisha Watanzania kuwa kina imani ya dhati katika siasa. 

“Ukiwa kiongozi, umeshakuwa kiongozi, uwe na msimamo ili watu wengine wale unaowaongoza wakufuate,” alieleza Mariam Mrema mfanyabiashara mdogo wa Dodoma. “Lakini ukiwa kiongozi, halafu huna msimamo, atakufuata nani? Umeenda ugenini ndio unafika tu unashika ufagio unafagia, haiwezekani lazima watu wakujadili.” 

Katika kuuaminisha umma juu ya dhamira yao kwa wananchi, Naibu Katibu Mkuu wa CHAUMMA, Mohamed Masoud, alijaribu kufafanua na  kukitenga chama hicho na hoja ya kuwa “vibaraka,” hasa katika kukiwezesha chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM), kutimiza na kuendeleza malengo yake ya kisiasa.

“Mimi nasema mgomvi wetu ni yule anayeshika dola,” alieleza Mohamed Masoud, wakati wa mkutano wa kuwapokea wanachama wapya katika ukumbi wa Ubungo Plaza mnamo Mei 21, 2025. “Mtakapokwenda katika maeneo yenu, mtapata kejeli sijui kibaraka, nawaomba mtakapoondoka hao watu wapuuzeni.”

“Huwezi kushindana na mbuyu, utie sumu kidogo kidogo chini,” aliongeza Masoud. “Nendeni mkapeleke sera za chama cha ubwabwa, na hoja zilizokuwa bora za kujenga amani, utulivu katika nchi yetu. Sasa wenzetu ukitamka hivyo, wanahisi wewe ni kibaraka, ubwabwa utalikaje bila ya amani?” 

Pamoja na maelezo ya Masoud na viongozi wengine wa chama hicho, bado baadhi ya wananchi wanakiona chama hicho kwa taswira ya kuwa ni mpango wa chama tawala, hasa katika kutafuta uhalali wa kisiasa kwenye uchaguzi  wa mwaka 2025, uchaguzi ambao chama kikuu cha upinzani, CHADEMA, kimeeleza kuwa hakitashiriki kama hakutakuwa na mabadiliko muhimu.

“Mimi nina shaka kidogo na juu ya uhamiaji wao CHAUMMA,” Majiko alidokeza kwenye mahojiano na The Chanzo. “Kwa sababu hawa watu wangechaguliwa CHADEMA sidhani kama wangeondoka.”

“Walikuwa wamezoea kula na mirija, kunyonya; sasa walivyoona bwana Tundu Atiphas Lissu kaingia na [John] Heche wana mfumo na muelekeo tofauti, watu wanasema duka lao limefungwa ndipo wakaamua kukata shauri,” aliongeza mwananchi huyo.

SOMA PIA: ‘CHADEMA G55’: Makovu ya Uchaguzi, Ushawishi Hafifu na Ndoto za Kujiletea Mabadiliko Binafsi Nyuma ya Kivuli cha Mbowe

Baadhi ya wananchi pia wanaonekana kuwahusisha G-55 na CHAUMMA mpya na matakwa ya kujineemesha kupitia mkwamo wa kisiasa unaoonekana nchini.

“Wao walituaminisha, tena kwa maneno makubwa sana, wakasema hawa mafisadi hawa, sijui wako hivi, na wakakusanya watu wengi kwenye mikutano mbalimbali,” anahoji Paschali Mariki, mfanyabiashara mdogo kutoka mkoani Dodoma. 

“Wakawaingiza vijana wengi kwenye mazingira hayo, sasa hatimaye wameondoka, niambie wale vijana, au wadau, waliowafuata na kuumia kwa ajili ya kuona kwamba wana sehemu ya utendaji wa haki, wataawaambiaje?” 

“Kitendo cha kuondoka kwa muda mfupi baada ya kukosa nafasi za uongozi, hiyo sisi kwetu tunaona wametufanyia kitu sio sahihi kabisa kama Watanzania,” anaendelea kutoa hoja Mariki. “Kwa sababu madhumuni ya wao kuwa chama cha upinzani ni kwa ajili ya maendeleo, sasa anavyoondoka hivi maana yake tunaona dhahiri kwamba wanaenda kufuata  masuala ya uongozi sio masuala kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.”

Katibu Mkuu mpya wa CHAUMMA, Mwalimu, ameeleza kuwa chama hicho cha upinzani kina surprise waliyoiandaa kwenye mikutano yao, huku wengi, hasa katika mitandao ya kijamii, wakiamini ni ushiriki wa kiongozi wa zamani wa CHADEMA katika mikutano hiyo inayokuja, ikiwemo ule ambao chama hicho kinatarajiwa kufanya hapo Jumamosi, Mei 24, 2025, jijini Dar es Salaam.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×
×