Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa amesema kuwa Maafisa Habari wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ni nguzo muhimu katika kuhakikisha Watanzania wanapata taarifa sahihi kuhusu yanayojiri katika maeneo yao.
Mchengerwa amezungumza haya wakati akifungua kikao kazi cha Maafisa Habari wa TAMISEMI kilichofanyika Mei 23, 2025 jijini Dodoma, amesema wanao mtaji wa kujua nini cha kulisha kwenye jamii.
“Kama mngeliamua jana mkasema mnataka taarifa zenu tu zitoke kwenye vyombo vya habari vyote ingewezekana,” amesema Mchengerwa. “Na pengine taarifa zenu zingeweza kutamba kwenye mitandao, vyombo mbalimbali vya habari.”
Amesema wamekuwa wakishuhudia baadhi ya vyombo vingine vya habari vikitoa taarifa zao na kusambaa kwa kasi, licha ya kutokuwa na mtaji kama ilivyo kwa maafisa habari hao ambao wanazo rasilimali za kutosha.
“Maana yake mtaji mnao kama ninyi na viongozi wanaowasimamia, wakurugenzi kwenye mamlaka ya Serikali za mitaa, wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa mkiamua pengine habari ambazo tutaziona TBC zitakuwa ni habari zenu kwenye maeneo yenu.”
Ameongeza kuwa, Maafisa Habari wamebeba dhamana ya kuhakikisha wananchi wanapata haki ya msingi ya kupata taarifa sahihi, na kurekebisha taarifa ambazo hazina ufasaha katika maeneo yao.
“Kuna wakati unasikia taarifa imetoka kwenye halamshauri fulani lakini iko kimya. Lakini hakuna kiongozi anayejitokeza kwenda kuizungumza na kwenda kuirekebisha. Nimekuwa nikiwaambia wenzangu hapa embu fuatilieni taarifa hii, waelekezeni hawa kutoka kuzungumza.”
Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo mkoani Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jaquelinevictor88@gmail.com