Katika siku ya kwanza ya mkutano mkuu maalum wa Chama cha Mapinduzi Mei 29, 2025, chama hicho kimefanya mabadiliko mengine ya Katiba yake; kwanza kuruhusu vikao vya kidigitali, pili kuongeza idadi ya wajumbe wa baraza la wadhamini kutoka nane mpaka tisa na tatu kuweka sharti la baraza la wadhamini kutoa ruhusa ya maandishi ya miradi mbalimbali ya kiuchumi ya chama hicho.
Hapa chini ni mjadala wote ulivyokua ukiongozwa na Mwenyekiti wa Chama hicho Rais Samia Suluhu Hassan:
Rais Samia: Haya waheshimiwa wajumbe sasa tunaendelea kwenye kipengelee kama inavyoonekana kwenye ratiba marekebisho madogo sana ya katiba yetu. tumeleta marekebisho madogo ya katiba yetu ya chama cha mapinduzi ya mwaka 1977 toleo la Januari mwaka huu yanayopendekezwa katika waraka huu na yamelenga mambo yafuatayo. La kwanza kama mnavyojua kwamba Chama chetu cha Mapinduzi kina kinaendelea jinsi dunia inavyoendelea. Ndani ya chama chetu cha mapinduzi sasa tunafanya kazi kidigitali pia na tumefunga mitambo ya kuweza kuwasiliana na mikoa na wilaya au mikoa kuwasiliana wilaya kuwasiliana ah ili kurahisisha utendaji wa kazi.
Kwa hiyo tumekuja na wazo la e-meetings mikutano ya kimtandao ambayo idara ya organizesheni inapendekeza vikao vifuatavyo kwa njia ya mtandao;
- Kikao cha kwanza ni sekretariati ya wilaya
- Kamati ya siasa wilaya
- Sekretarieti ya mkoa
- Kamati ya siasa mkoa
- Sekretarieti ya kamati maalum ya halmashauri kuu ya CCM taifa
- Sekretarieti ya halmashauri kuu ya CCM taifa
- Kamati maalumu ya halmashauri kuu ya CCM taifa
- Kamati kuu ya halmashauri kuu ya CCM
- Halmashauri kuu ya CCM taifa
- Mkutano mkuu wa taifa.
Sasa hivi vikao vingine tumeviweka kwa kujua kwamba jinsi tunavyoendelea huko mbele tutakuwa tunaendelea kiteknolojia na kwamba katiba yetu inatupa fursa ya kutunga kanuni za vikao hivi. Lakini kwa sasa tumeanza mikutano na kamati za siasa au halmashauri kuu za siasa za mikoa au za wilaya. Lakini mikutano ile haimo katika maelekezo ya katiba ya chama chetu.
Kwa hiyo tumeamua kuiingiza ili mikutano ile isikiuke katiba ya chama isiwe mikutano kinyume na katiba ya Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo hilo ni pendekezo la kwanza tunalokwenda kulileta kwenu. Lakini vikao husika hivi vinavyozungumzwa vitafanyika kwa njia ya mtandao endapo tu kuna ulazima au udharura. Vikao husika kwa ngazi ya wilaya na mkoa vitafanyika kwa idhini ya katibu mkuu. Watamjulisha katibu mkuu kwa nini wanafanya kikao kwa mtandao na hii ni kuepusha kutumika vibaya mitandao hii. Hilo ni swala la kwanza.
Lakini swala la pili ni swala la baraza la wadhamini. Sheria ya vyama vya siasa sura ya 258 rejeo la 2019 imetutaka idadi ya mabaraza ya wadhamini wa vyama vya siasa iwe namba isiyogawanyika kwa mbili yaani iwe 3,5, 7, 9,11, sasa baraza letu la wadhamini lina watu wanane. Kwa hiyo tunapaswa kumwongeza mtu mmoja wawe tisa na hii inakwenda kwa mujibu wa katiba yetu. Kwa hiyo tunaleta ili kuiweka kwenye katiba ili tuweze kuwa na namba kama inavyotakiwa kwenye baraza la wadhamini.
Lakini sehemu ya pili ya baraza la wadhamini katika jitihada zake za kuimarisha uchumi wa kisiasa. Tunatazamia kutumia ushauri wa kitaalamu katika shughuli zake za uwekezaji kwa lengo la kuongeza tija. Kama mnavyojua chama chetu sasa hivi tunazipa nguvu kubwa kampuni zetu za chama ili ziweze kuzalisha kwa manufaa ya chama. Tunajielekeza zaidi kwenye uwekezaji na uchumi. Kwa maana hiyo kwa mtazamo huu ni wakati muhimu wa baraza la wadhamini kuiona, kujiridhisha na kutoa maelekezo kwa miradi itakayobuniwa na ngazi za mikoa na taasisi nyingine kwa manufaa ya chama.
Katika kutekeleza jukumu hilo, baraza la wadhamini la Chama cha Mapinduzi litatoa idhini kwa maandishi. Katiba inavyosomeka sasa, Baraza la wadhamini litatoa idhini, itakasimu imeandikwa itakasimu madaraka hayo kwa kamati za siasa. Sasa ile imechukuliwa kwamba ni automatic kamati za siasa mikoa huko wakiwa na miradi wanamaliza kila kitu bila kuja kwa baraza la wadhamini. Kwa hiyo sasa tunaweka neno kwa maandishi hilo tu basi maneno mengine mantiki iko vile vile. Watakasimu kwa maandishi hii ina maana kamati za siasa sasa bidi ziombe ruhusa kwa baraza la wadhamini na wajibiwe kwa maandishi.
Kwa hiyo marekebisho matatu ni hayo. La kwanza la mikutano kidigitali, la pili namba ya baraza la wadhamini na ya tatu ni kwamba kukasimiwa yale madaraka ya miradi ni kwa maandishi waheshimiwa wajumbe wa mkutano mkuu hayo ndio marekebisho tunayoyawasilisha na kuomba ridhaa ya wajumbe wa mkutano mkuu.
Ridhaa imetolewa? [Anauliza Rais Samia]
Wajumbe: Ndiooo!
Ridhaa imetolewa? [anauliza tena]
Wajumbe: Ndiooo!
Rais Samia: Tunawashukuru sana.
Wajumbe wanapiga makofi.