Dodoma. Wakati jamii, wadau na serikali ikiendelea kutekeleza afua mbalimbali za hedhi salama hapa nchini, baadhi ya wasichana wanaoishi eneo la Ng’hong’hona wamekuwa wakitumia vipande vya magodoro kujisitiri wakati wa hedhi, huku sababu tamaduni na mazoea ya jamii husika yakitajwa zaidi.
Utaratibu huu wa kutumia magodoro umekuwa kama sehemu ya utamaduni uliorithishwa kutoka kizazi hadi kizazi, hata hivyo kufuatia kupata elimu, mabinti wengi katika eneo hilo wanatamani kuona hali hii ikibadilika katika jamii.
Mwaka 2022, Martha 17, mwanafunzi wa kidato cha nne alipovunja ungo alimfuata mama yake na kumueleza hali halisi. Baada ya kumueleza alielekezwa na mama yake namna ya kutumia magodoro kujisitiri.
“Akaniambia nachana kipande cha godoro kinakuwa chembamba. Na akanielekeza namna ya kuweka kwenye nguo ya ndani. Niliendelea kutumia hadi sasa hivi. Nikisha tumia nafua na kuanika bafuni kuna kamba nimeweka,” anaeleza Martha wakati akiongea na The Chanzo Mei 17, 2025.
Martha ni miongoni mwa wasichana ambao hawakuwahi kutumia pedi tangu kuzaliwa kwao. Vipande vya magodoro wakati wa hedhi, imekuwa ni sehemu ya maisha yake.
“Godoro unapotumia husababisha damu kuvuja,” anasema Martha akionesha hali ya kuona aibu. “Najisikia vibaya, wakati mwingine damu zinapita hadi kwenye nguo niliyovaa wanafunzi wakikuona wanakuwa wanakucheka.”
Taarifa ya Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu [NIMR 2021] ilibainisha kuwa asilimia 17 ya wasichana Tanzania walishindwa kuhudhuria masomo yao pindi wakiwa katika hedhi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo maumivu ya tumbo, kuogopa fedheha endapo wangechafuka na kukosa vifaa salama vya hedhi asilimia 42.
Kupoteza Kujiamini
Kukosa vifaa salama vya hedhi ni moja ya sababu kubwa inayofanya wasichana wengi kupoteza kujiamini, na hata kuwaathiri katika masomo yao. Elizabeth ,17, ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule moja ya Sekondari Dodoma na mtoto wa pili kuzaliwa kati ya watoto watatu katika familia yao, anakumbuka vizuri siku aliyovunja ungo.
Alianza kusikia dalili tofauti mwilini mwake, ikiwemo kuumwa tumbo. Ghafla alijihisi kulowa kwenye nguo yake ya ndani. Hali hiyo ilimfanya aende msalani kuangalia nini kimetokea. Alijikuta amechafua nguo zake za ndani, hivyo kuamua kumfuata dada yake na kumueleza kilichotokea.
“Nikamfuata dada yangu nikamuambia, nakumbuka alikuwa na pedi moja akanipatia. Baada ya kunipatia akanielekeza namna ya kuitumia.”
Tangu alipotumia pedi hiyo moja aliyompatia dada yake, hakuwahi kutumia tena zaidi ya vipande vya magodoro hadi sasa. Anasema, mara nyingi anapotumia magodoro anapoteza uwezo wa kujiamini anapokuwa katika mazingira ya shule,
“Mwalimu anapokuwa darasani anafundisha, na upo kwenye hedhi na unatumia godoro unaogopa kunyoosha mkono na unagopa kunyanyuka,” anasema. Pia unapotumia godoro huwa lina harufu mbaya halafu pia linachubua.”
Kwa kawaida, Elizabeth hukata vipande vitatu hadi vitano vya godoro ili kujisitiri. “Kwa siku huwa natumia vapande viwili hadi vitatu. Kwa hiyo nikishatumia vile viwili navifua na navitumia vile vingine vilivyobaki. Ninapovifua huwa naanika juani,” anafafanua Elizabeth.
Hali iliyomkuta Elizabeth, ni hali alyokutana nayo Avelina pia, ambapo anakumbuka hali ya sintofahamu iliyomkuta mwaka 2022 alivyovunja ungo akiwa darasani. Aveline anayesoma kidato cha nne katika anaeleza kuwa akiwa darasani alihisi kubanwa na haja ndogo. Na alipokwenda msalani alijikuta amechafua nguo yake.
“Nikarudi darasani nikawa sijisikii vizuri nikaogopa kuwaambia marafiki zangu nikasema watanicheka,” anasema. “Nikatoka nje nilivyorudi nyumbani nikawa ninaogopa sikumuambia mama. Ile nguo ya ndani niliyoichafua nikaifua mama hakujua,”
Aveline, mtoto wa sita kuzaliwa kati ya watoto sita katika familia yao, anasema mwezi uliofuata alijikuta akipata hedhi tena. Hali hiyo, ilimfanya amueleze mama yake.
“Mama akanikatia kigodoro akaniambia nivae niende shule. Nikirudi nitakuta amenikatia vingine tena,” anasema. “Nilishinda na kipande cha godoro siku nzima, nilikuwa nikijisikia nikitoa harufu, na sikuwa na amani darasani.”
“Hata wanafunzi wenzangu walikuwa wakicheka nilikuwa nikihisi wakinicheka mimi,” anasema. “Mwalimu anapokuwa darasani ni ngumu kumsikiliza, najihisi kama nimejichafua . Ninachotamani mtoe elimu kwa wazazi ili wajue matumizi ya pedi kwa sababu hawaelewi wanasema tukitumia pedi tutapata madhara kwenye kizazi.”
Utamaduni
Wenyeji wa jamii ya hapa Ng’hong’hona ni wagogo kwa asilimia kubwa na kumekua na imani kwamba watoto wao wakitumia pedi watakuwa wahuni. Kutokana na imani hii, suala la kutumia magodoro limekuwa jambo la kawaida, huku matumizi ya pedi yakipigwa kisogo. Hata hivyo, suala hili limekua likiwaathiri mabinti kisaikologia n ahata kiafya.
Joyce 15, ni mwanafunzi wa kidato cha pili, anaeleza baadhi ya changamoto alizokutana nazo baada ya kuvunja ungo akiwa shambani kwenye mavuno.
“Nilipomuambia mama asubuhi yake akaniambia nitakuchania vipande vya godoro kwa ajili ya kujisitiri. Akanichania ilikuwa vipande vitano vya godoro. Nilitumia asubuhi kimoja na jioni kimoja. Damu zilikuwa zinapitiliza wakati mwigine, nilikuwa nikiwashwa,” anasema Joyce.
“Wazazi wapewe elimu kuhusu matumizi ya pedi maana kuna wazazi wengine hawaamini kuhusu matumizi ya pedi . Wanahisi kwamba pedi zinasababisha uhuni, na zinamfanya mtoto wa kike anakuwa na hisia kali.”
Anna Charles Makamu Mkuu wa shule ya sekondari Ng’hong’hona na mlezi wa watoto wanaoishi katika mazingira magumu anasema, kuhusu kutumia magodoro kujisitiri anaeleza kuwa wameendelea kujitahidi kutoa elimu kwa wanafunzi na pia kujiaandaa tahadhari zinaotokea.
“Ila kuna elimu ambayo tunawapatia wanafunzi wetu wanapokuwa katika siku zao,” anaeleza Anna Makamu. “ Elimu hii huwa tunaitoa tunapokuwa na vikao vyetu walimu wa kike pamoja na wanafunzi wa kike. Tunaelimisha namna gani wanatakiwa kujisitiri wanapokuwa katika siku hizo.”
Afisa Miradi wa Shirika la The Living Smile International linalofanya kazi katika mtaa wa Ng’hong’hona Venance Kibengwe, anasema jamii ya Ng’hong’hona haina uelewa kuhusu matumizi ya pedi. Badala yake watoto wamekuwa wakielekezwa na wazazi au walezi kutumia magodoro jambo ambalo limekuwa likiwaondolea hali ya kujiamini.
“Kwa sababu kwenye jamii yetu hasa ya Ng’hong’hona wazazi wanaamini matumizi ya pedi ni hatari, jambo ambalo halina uthibitisho wowote wa kiafya. Kwa sababu wengine wamekuwa wakihusisha matumizi ya pedi kusababisha ugumba jambo ambalo si la kweli.”
Naye, Monica Patrick ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika Lisilo la Kiserikali linalojikita kuwawezesha wasichana na wanawake kutimiza malengo yao anasema, wasichana wengi wamekuwa wakitumia vitu mbadala kujisitiri wakati wa hedhi ikiwemo majani, kinyesi cha ng’ombe, mabunzi ya mahindi na wanaotumia magodoro wakiamini kwamba itawasiadia kufyonza damu wanapokuwa katika hedhi.
Anasema, hiyo husababisha hatari kwa afya za watoto wa kike. “Inaleta hisia za kuchukia hedhi , inafikia hatua anajiuliza kwa nini mimi nilizaliwa msichana. Na kwa nini kila mwezi naingia katika hedhi,” Monica anaiambia The Chanzo. Monica anapendekeza Serikali kuondoa kodi kwenye pedi, ili kurahisisha upatikanaji wa pedi kwa bei rahisi, na ikibidi kuondolewa kwa bei ili ziweze kupatikana kwa urahisi ama bure.
Mwongozo wa hedhi salama
Katika kukabiliana na baaadhi ya changamoto zinazowakabili watoto wa kike hasa mashuleni, serikali imeandaa mwogozo wa hedhi salama.Afisa Afya na Mratibu Ngazi ya Taifa wa Hedhi Salama kutoka Wizara ya Afya, Mariam Mashimba anasema, kwa kiasi kikubwa Serikali imekuwa ikishirikiana na wadau kuhakikisha inatatua changamoto za hedhi hususan katika shule.
“Katika mwongozo wetu tumeweka bayana kabisa kwamba wasichana na wanawake watumie bidhaa ambazo zimethibitishwa na mamlaka zetu,” anasema Mariam wakati akiongea na The Chanzo. “Tumesema hivyo, kwa sababu kuna jamii nyingi inachukulia kawaida, wengine wanaona kwa nini nisinunue hata kitenge kipya. Mbali na kusema kwamba wanatumia magodoro kuna wengine sasa wanasema basi kwa nini nisitumie khanga.”
“Kumbuka ile khanga na vitenge unaona kitenge kinaondoa ile rangi, lazima tujiulize rangi inaenda wapi. Hasa unaweza ukafirikia kwamba unapotumia vitambaa ambavyo vinachuja rangi, ambavyo havijathibitishwa wakati mwingine magodoro yanayotumika yanaweza yakaharibu via vya uzazi.”
Mwongozo huo umeweka bayana dhana ya ufundishaji walimu watakao kuwa wakifundisha wasichana shuleni, kwamba ni mambo gani ya kuelimisha ili jamii iepuke kutumia bidhaa ambazo zinahatarisha afya zao wakati wa hedhi.
“Mbali na via vya uzazi wengi wao wamekuwa wakipata maambukizi kupitia njia ya mkojo UTI. Unakuta mtu anavaa pedi muda mrefu, kwenye mwongozo tumebainisha angalau masaa sita yasizidi masaa nane. Unakuta mtu ameshinda nayo toka asubuhi mpaka saa 12 jioni. Na hiyo ni kutokana na kwamba asipate gharama atumie mbili kwa siku.”
Kabla ya mwongozo huo, anasema Serikali ilikuwa tayari imeweka utaratibu kwamba kupitia fedha zinazotolewa za mgao kwenye shule za asilimia 10 za fedha za uongozi yaani ‘administration’ zitumike kwa ajili ya kununua pedi za dharura.
“Mwanafunzi yoyote anapokuwa shuleni anapopata hiyo changamoto anapewa pedi. Lakini hiyo, haitoshi bado wadau kwa kiasi kikubwa walitusaidia kukusanya hizo taulo za kike.”
Hata hivyo, anasema familia zinapaswa kuwa na bajeti ya kununua pedi. “Kwa sababu tunaweka bajeti za vyakula, tunasahau kwamba tuna mabinti wa kike tuna wanawake katika familia zetu.”
Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana mkoani Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jaquelinevictor88@gmail.com