The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Bajeti Sio Mkoba, Ni Maisha ya Kila Siku

Bajeti ya taifa ni ya kiraia, sio ya wataalamu au Wabunge pekee. Inahusu afya yetu, elimu ya watoto wetu, ajira za vijana wetu, hifadhi ya jamii, na ndoto zetu.

subscribe to our newsletter!

Wakati nikiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, pengine nilishangazwa, au kufurahishwa, na namna bajeti ya taifa ilivyowasilishwa Bungeni. Nilipenda namna Waziri wa Fedha, aliyevalia suti, akishuka kwenye ‘shangingi’ akiwa amebeba mkoba mweusi. 

Ilikuwa kama hafla fulani! Kamera zilimfuata na midahalo kwenye runinga iliendelea. Nilidhani ndio kilikuwa kiini cha bajeti ya taifa, yaani, ule mkoba na hotuba yenye takwimu iliyowasilishwa Bungeni kwa niaba ya Serikali.

Miaka kadhaa imepita, sasa nipo kwenye nafasi ya kuyatafakari haya kwa undani zaidi. Tayari nimeshafanya kazi na vyama vya wafanyakazi, taasisi za kimataifa, na mashirika mbalimbali. Leo, ninafahamu kuwa uwasilishaji wa bajeti ya taifa sio tamasha, au hafla tena. Ni tukio muhimu mithili ya msingi wa nyumba linalobainisha hatima ya taifa letu kwa mwaka wa fedha unaofuatia, hususan kwa wale wasioonekana Bungeni.

Kila mwaka, bajeti ya taifa huwasilishwa kwa lugha ya asilimia, trilioni, na miradi mikubwa. Lakini je, ni kwa kiasi gani wanajamii walio wengi huelewa bajeti hii inamaanisha nini kwao? Na je, wale wanaoiwasilisha wanadhani jamii inahitaji kuelewa? 

Huu ni mgongano wa kimtazamo. Serikali huandaa bajeti kana kwamba inaeleweka. Wananchi nao, kwa kiasi kikubwa, huikwepa kana kwamba sio ya kwao. Matokeo yake bajeti hii, ambayo ni yetu sote, hubaki kuwa ya wataalamu na wanasiasa.

SOMA ZAIDI: Bajeti ya Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar Inaakisi Umuhimu wa Sekta ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi? 

Mfano halisi ni vijana waliojiajiri katika sekta isiyo rasmi. Wengi wao hawafahamu kuwa bajeti husika huweka mikopo kwa ajili ya biashara ndogo, au kwamba kuna fungu la masuala, kama mafunzo ya stadi za kazi. Lugha ya bajeti ni ngumu, ya kiufundi, nyaraka zake ni ndefu, na mara nyingi hakuna jitihada za makusudi kuyafafanua haya yote kwa Kiswahili fasaha na rahisi ambacho Watanzania wengi wanaweza kuelewa.

Kwa mfano, hotuba ya Waziri wa Fedha mwaka 2025 ilijaa takwimu—mapato, matumizi, na miradi ya kimkakati. Ilitaja mabilioni kwa miundombinu, kilimo, na afya. Lakini kwa mama wa Nyamongo au kijana wa Liwale, hizi ni takwimu tupu na ngumu. 

Watu hawa, mara nyingi, hujiuliza maswali kama: Je, takwimu hizo zitaongeza dawa katika zahanati? Je, zitaleta stadi mpya za kazi? Je, ni kwa namna gani zitatatua changamoto za masoko kwa wakulima wadogo? Pasipo ufafanuzi sahihi na wenye muktadha, bajeti hukosa uhalisia na hata umiliki wa umma.

Uelewa wa umma

Tunaweza kujifunza kutoka mifumo ya bajeti shirikishi inayotekelezwa katika baadhi ya nchi kama vile Korea Kusini. Simaanishi tuige kila kitu ambacho jamii nyingine zinafanya, la hasha! 

Ninachomaanisha ni kuwa ni vema mchakato wa bajeti ya taifa ukawa shirikishi, yaani, ukaanza kwa kusikiliza wananchi. Sio kuwasikiliza baada maandalizi, au kuwa bajeti imeshapitishwa. Tupange kwa kushirikiana kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa.

SOMA ZAIDI: Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Yaendelea Kujidhatiti Bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali 2025/26

Kwa upande mwingine, wanahabari, wanazuoni, na asasi za kiraia wana jukumu la ziada kwenye mchakato huu. Wanapaswa kufanya ufafanuzi wa bajeti kwa kuchambua kifungu kwa kifungu na kuwaonesha wananchi bajeti inamaanisha nini kwa maisha yao. 

Taarifa haijitoshelezi pasipo muktadha. Namba na takwimu hazina maana ikiwa simulizi haimfanyi mlengwa akahisi kuguswa, au kuwa sehemu ya kinachozungumzwa.

Katika karne hii ya taarifa, uwasilishaji wa bajeti unaweza kuboreshwa kwa kutumia simulizi za kuona, sio namba pekee. Wakati Waziri anataja trilioni kadhaa kwa kilimo, au barabara, sio vibaya zikapita grafu rahisi au picha zinazoonesha matokeo yake kwa jamii yetu. 

Maboresho ya uwasilishaji wa bajeti kupitia vielelezo na picha mjongeo moja kwa moja yanaweza kumsaidia hata mama wa kijijini, au kijana wa sokoni akaelewa bajeti, ijapokuwa kidogo—sio kwa sababu ni hotuba bali kwa kuwa inaoneshwa katika maisha halisi na ya kila siku.

Mali ya Watanzania

Bajeti ya taifa ni ya kiraia, sio ya wataalamu au Wabunge pekee. Inahusu afya yetu, elimu ya watoto wetu, ajira za vijana wetu, hifadhi ya jamii, na ndoto zetu. Kuanzia mchakato wa maandalizi yake hadi pale inaposomwa Bungeni au kutangazwa kwenye vyombo vya habari, bajeti ya taifa haina budi kuandaliwa katika namna ambayo mwanajamii ataihisi kuvutiwa nayo na kuimiliki.

SOMA ZAIDI: Je, Bajeti ya Wizara ya Kilimo 2025/26 Inaakisi Matarajio ya Wakulima? 

Katika hotuba ya bajeti kwa mwaka 2025/2026, Serikali imetangaza kuwekeza zaidi ya Shilingi bilioni 1,200 kwenye kilimo, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuinua uchumi wa wananchi wengi. 

Hata hivyo, bado kuna ukosefu wa maelezo rahisi juu ya namna mkulima mdogo anaweza kunufaika. Uwasilishaji unahitaji ufafanuzi wa moja kwa moja wa namna ya kupata pembejeo kwa bei nafuu, jinsi ya kushiriki katika skimu za umwagiliaji au namna ambayo vijana wanaweza kushirikishwa kwenye ajira zinazozungumzwa. 

Bila ufafanuzi wa wazi, vifungu hivi vya bajeti hubaki kuwa namba na takwimu tu zisizo na uhalisia katika maisha ya wanajamii wa kawaida.

Ninashauri Serikali na wabunge wetu kuanza kwa kuuliza swali hili: “Bajeti hii itaeleweka kwa nani?” Kama jibu si “kila Mtanzania,” basi bado tuna kazi ya kufanya kuhakikisha tunafikia hali ambayo kila mmoja, au Watanzania wengi, watahisi kuna haja ya kufuatilia bajeti husika.  

Vilevile, Serikali ni vema ikafikiria kuwa maandalizi ya bajeti, ikiwa ni pamoja na uwasilishaji wake, walengwa wa msingi ni Watanzania na sio Shirika la Fedha Duniani, Benki ya Dunia, au wadau wa maendeleo. Tusitegemee midahalo ya siku moja au wiki kadhaa Bungeni, bali mjadala wa muda mrefu na unaoishi katika maisha halisi ya jamii yetu.

Kwa sababu bajeti ya taifa sio takwimu au namba tu bali dira na mwongozo unaobeba matarajio ya Watanzania—ikiandikwa kwa lugha ya watu, ikiwasilishwa kwa sauti ya watu, na ikatekelezwa kwa ajili ya watu, ni nguzo muhimu ya mabadiliko ya kweli. 

Tusiiache ikawa tukio na simulizi ya siku moja. Tuiweke kwenye maisha yetu ya kila siku na tuache kushangilia ule ‘mkoba’ unaobeba nyaraka za bajeti!

Venance Majula ni mtaalamu wa sera za kazi na maendeleo na mjumbe wa Bodi ya Sauti ya Vijana ya Umoja wa Ulaya Tanzania, anayejikita katika ujumuishaji wa vijana, mifumo ya maarifa, na mpito wenye haki. Unaweza kumpata kupitia majulavefama@gmail.com au X kama @venancemajula. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×