Tumetoka kusherekea Siku ya Baba Duniani, na bado mioyo yetu imejaa shukrani. Tunawawaza akina baba wanaotuzunguka, waliotulea, na sisi wenyewe ambao tunaendelea kujifunza kuwa baba bora, si kwa ukamilifu, bali kwa upendo na jitihada za kila siku.
Kwa muda mrefu, baba bora alionekana kama yule anayehudumia familia kifedha: analeta chakula, analipa ada, anajenga nyumba. Lakini leo tunaelewa kuwa watoto wetu wanahitaji zaidi. Wanahitaji uwepo wetu wa kweli, moyo wetu, na usikivu wetu. Waweze kutuona, kutusikia, na kuhisi ukaribu wetu.
Wengi wetu tulikulia katika familia ambazo baba alikuwa mbali kihisia, mkali kupita kiasi, au hakuwa mtu wa mazungumzo. Lakini leo, tunachagua njia tofauti. Tunajifunza kusema, “nakupenda,” “nipo kwa ajili yako,” na “niambie kinachokusumbua.” Tunachagua kutengeneza mazingira ya nyumbani yanayoruhusu watoto wetu kujieleza bila woga, na kukua wakiamini kuwa wao ni wa thamani.
Uwepo wetu, hata kwa njia ndogo kama kuwasikiliza au kucheza nao, una maana mkubwa kuliko tunavyodhani. Tunajenga kumbukumbu, tunajenga maelewano, na tunajenga kizazi kinachoamini katika upendo wa kweli.
Ndiyo maana, tunachukua nafasi hii kuwapongeza baba wote wanaojitahidi kujenga namna mpya ya kuwa baba, wale wanaochagua upendo badala ya ukali, ushirikiano badala ya mamlaka, na uwepo wa kihisia badala ya kuwa tu kivuli kinachoonekana kimwili.
SOMA ZAIDI: Je, Tumefikiria Kulea Watoto Wanaojali Mazingira?
Wakati wa kuandika makala hii binti mmoja alisimulia jambo ambalo limebaki vichwani vyetu hadi leo:
“Nikiwa darasa la saba nilikuwa na hedhi na niliumwa sana. Mama hakuwa nyumbani. Baba ndiye aliyenisaidia. Alinichukulia pedi, alinioshea jeans zangu ambazo zilikuwa zimechafuka, akanisindikiza hospitali. Sitosahau upendo wake, hakuona aibu wala kuniona kama mzigo aliona mtoto wake anahitaji msaada.”
Shuhuda kama hizi hutufundisha kuwa baba anaweza kuwa mlezi kamili bila kujali ni mtoto wa kiume au wa kike. Tunapojitoa kusaidia watoto wetu kwa hali zote, tunawaonesha kwamba tunawathamini na kuwapenda, hata katika hali ngumu au zinazodhaniwa kuwa ni “za kina mama tu.”
Tunajua hatuwezi kuwa wakamilifu, lakini siku hizi tunajitahidi. Tunauliza maswali. Tunaangalia maudhui ya malezi bora. Tunaingia kwenye vikundi vya wazazi mtandaoni. Tunajua kuwa kujifunza si dalili ya udhaifu ni uthibitisho wa kujali maslahi ya watoto wetu. Tunajifunza kuwasikiliza watoto wetu. Tunajifunza kusema “samahani.” Tunajifunza kukiri tunapokosea. Kwa kufanya hivyo, tunawafundisha watoto wetu kuwa binadamu ni kujifunza kila siku na kwamba upendo hauhitaji ukamilifu, bali ni nia tu.
Sisi ni kizazi kipya cha wababa, tuendelee kutafakari safari zetu za malezi ili tuendelee kuwa baba wa tofauti, baba wa karibu, baba shupavu kweli kweli. Na watoto wetu, familia zetu, na jamii yetu zitanufaika kwa hilo kwa miaka mingi ijayo.
Kwa baba yeyote anayejitahidi — tunakupongeza.
Kwa baba anayejifunza — tunakushukuru.
Kwa baba anayechagua kupenda watoto wake kwa dhati— tunasimama pamoja nawe.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.