The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Gharama za Huduma za Afya Chanzo Kikuu cha Umasikini Afrika. Uhandisi Jeni kwa Afya Unaweza Kupunguza Tatizo Hili

Elimu kuhusu manufaa ya matumizi ya GMO katika sekta ya afya itasaidia sana katika kupunguza ukinzani kutoka kwa jamii, na kuongeza kukubalika kwa teknolojia hii.

subscribe to our newsletter!

Afrika inashuhudia ongezeko kubwa la gharama za huduma za kiafya, ongezeko la uhitaji wa madawa ya binadamu unaosababiswa na ongezeko la watu, kukua kwa miji, na ongezeko la magojwa yasiyo ya kuambukizwa, hali ambayo imepelekea ugumu kwa watu wengi kumudu gharama za huduma za afya bora. 

Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2024 inaonesha kwamba “gharama kubwa za huduma za afya barani Afrika zinaendelea kuwasukuma zaidi ya watu milioni 150 katika janga la umasikini,” huku Serikali za nchi za Afrika zikiendelea kupambana kwa hali na mali kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma bora za afya. 

Hata hivyo, wadau wanakubaliana kwamba licha ya juhudi hizi, ikiwemo kujenga mifumo endelevu ya ugharamiaji wa huduma za afya, bado kuna haja ya kufanya zaidi ili kuhakikisha kwamba watu kote barani Afrika wanapata huduma bora za afya wanazohitaji.

Tafiti pia zinaonesha kwamba, changamoto zinazopelekea kuongeza gharama za huduma za kiafya barani Afrika ni pamoja na uhaba wa viwanda vya kuzalisha madawa kwa ajili ya matumizi ya binadamu, uhaba wa malighafi za kuzalisha madawa, na uwekezaji mdogo kwenye sekta ya kuzalisha madawa ya bidanadamu.

Uhandisi Jeni

Moja kati ya teknolojia ambazo zinaweza kuongeza uzalishaji wa malighafi kwa ajili ya uzalishaji wa dawa za binadamu na kupelekea kupunguza utegemezi wa mataifa yaliyoko nje ya bara la Afrika kwa ajili ya madawa ya binadamu ni teknolojia ya uhandisi jeni. 

SOMA ZAIDI: Chakula cha Msaada Kutoka Marekani na Mijadala ya Usalama Wake

Pamoja na kuwa teknolojia ya Uhandisi Jeni hupata ukinzani kwenye matumizi yake, hususani katika kilimo, kunakotokana na uelewa mdogo wa watu juu ya teknolojia hiyo, ukweli ni kwamba upo ushahidi wa kutosha wa kisayansi unaodhihirisha pasi na shaka yoyote teknolojia kuleta mapinduzi makubwa kwenye sekta ya afya.

Teknolojia hii ambayo mwanzo ilikuwa ikitumika hasa katika kutatua changamoto zinazopelekea uzalishaji mdogo wa mazao ya kilimo, ikiwemo kuzalisha mbegu zinazokinzana na magonjwa, wadudu na mabadiliko ya tabia nchi, ikiwemo kuhimili ukame, imepata mapokezi mazuri kwenye sekta ya afya duniani, hasa kwenye matumizi yake kwenye kutengeneza dawa za binadamu, kama vile chanjo, utengenizaji wa protini ya matibabu ya saratani, na kadhalika.

Mbinu inayotumika inajulikana kama “kilimo-dawa,” au pharming kwa kimombo, ambapo dawa za binadamu huzalishwa kwa kutumia mazao ya kilimo, hasa mimea iliyobadilishwa vinasaba.  

Wanasayansi wanatueleza kwamba teknolojia hii imekuwa na mchango mkubwa sana duniani, hasa kwa kupunguza gharama za uzalishaji wa madawa kama vile uzalishaji wa dawa zakibiolojia, au biopharmaceuticals kwa kimombo, kama insulini au kongosho ambayo inasaidia matibabu ya ugonjwa wa kisukari na kingamwili za monoklonoli, au monoclonal antibodies kwa kimombo, ambazo zinasaidia kupambana na magojwa ya saratani.

Matumizi ya viumbe vilivyobadilishwa vinasaba katika uzalishaji wa madawa umeongeza ufanisi wa matibabu, ikiwemo kuchagiza uwezo wa kuzalisha protini za binadamu kwenye amira, au yeast, au mifumo ya bakteria imepunguza utegemezi wa vyanzo vya zamani, jambo ambalo limepunguza gharama za uzalishaji na kurahisisha upatikanaji wa madawa haya kwa watumiaji.

SOMA ZAIDI: GMO: Suluhisho la Usalama wa Chakula Afrika?

Matumizi ya mazao na viumbe vilivyobadilishwa vinasaba yanategemewa kuongezeka kutokana na ufanisi na ubora wa teknolojia mpya zinazotumika kubadili vinasaba kwa gharama ndogo, ufanisi mkubwa na muda mfupi wa katika uzalishaji.

Lakini swali la msingi bado linabaki, ukizingatia ukinzani ambao teknolojia unakutana nayo, kama tulivyogusia hapo juu: Je, uzani wa faida na hasara za kukubali au kutokukubali kutumia teknolojia hii umelalia wapi?

Tafiti zinaonesha kuwa mchango wa mazao yaliyobadilishwa vinasaba katika uzalishaji wa madawa ya binadamu hauwezi kupuuzwa ukizingatia ongezeko la magojwa, kuongezeka kwa gharama za huduma za afya barani Afrika, changamoto za mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la watu duniani, na ukuaji wa kasi wa sayansi, teknolojia na ubunifu.

Tafiti zaidi

Kwa hiyo, upo umuhimu mkubwa wa Serikali za mataifa ya Afrika, wadau na mashirika binafsi kuwekeza katika tafiti zitakazowezesha kuthibisha ubora wa teknolojia hii na kupelekea kurekebisha sera na kuwezesha matumizi ya teknolojia hii barani Afrika. 

Mataifa ya Afrika kama Misri na Afrika Kusini ni mfano mzuri, wameanza matumizi ya GMO katika uzalishaji wa madawa. Bara la Afrika linahitaji kuwekeza zaidi katika utengenezaji wa maabara za kisasa kwa ajili ya kuimarisha tafiti za kibioteknolojia ili kuzalisha madawa mengi kuendana na mahitaji yanayozidi kuongezeka.

Elimu kuhusu manufaa ya matumizi ya GMO katika sekta ya afya itasaidia sana katika kupunguza ukinzani kutoka kwa jamii, na kuongeza kukubalika kwa teknolojia hii. Madhara kama vile usugu wa vimelea na athari za aleji yanaweza kuzuiliwa kwa kuweka taratibu madhubuti za majaribio ya kliniki, ufuatiliaji wa baada ya matumizi, na taarifa kwa watumiaji.

Martinus Sospeter, ni mwasilishaji wa sayansi kutoka Katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo. Kwa mrejesho anapatikana kupitia martinuss530@gmail.com. Rebeca Kachembeho ni mtafiti wa bioteknolojia ya kisasa katika chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, na Jackline Martine, ni mwandishi chipukizi wa sayansi. Haya ni maoni binafsi ya waandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×