Hivi karibuni nimebahatika kusoma kitabu kiitwacho Manufacturing Consent: The Political Economy of Mass Media kilichoandikwa na Edward S. Herman and Noam Chomsky. Licha ya ukweli kuwa kitabu hiki kimeandikwa muda mrefu, mwaka 1988, tena kwa kutumia rejea na mifano ya muundo wa vyombo vya habari na siasa za Marekani, nchi inayotumia sana propaganda, lakini ujumbe wake ni mahususi, maridhawa na mbashara katika muktadha wetu hapa Tanzania.
Tena, nadiriki kusema kwamba labda, ni muhimu kushikishana maudhui na dhumuni la kitabu hiki sasa kuliko miaka thelathini na zaidi iliyopita. Si vibaya kusema, waandishi kwa kiasi fulani walikuwa manabii wa nyakati kwa ufanisi katika kazi zao.
Kwa kifupi, kitabu hiki kinaeleza kwa undani sera na muundo wa vyombo vya habari na jinsi vilivyo tegemezi na visivyo huru katika kufanya kazi zake. Kwa nje na harakaharaka, wengi tunafikiria kuwa vyombo vya habari ni huru na vinajitegemea bila kuingiliwa katika kutimiza wajibu wao. Kumbe, wakati mwingi, vyombo vya habari vinatumika na wakati mwingine kudhibitiwa kwa faida ya kampuni za biashara na wamiliki wa vyombo hivyo.
Noam na Edward pia wanaeleza kinagaubaga, tena kwa mifano, jinsi propaganda mbalimbali, hasa za kiserikali za kipopulisti zinavyotumika na kuendeshwa katika kuandaa, kuchakata, kuchuja, kuchagua, kudhibiti habari kabla ya kuwafikia walaji, wasikilizaji, wasomaji, na watazamaji. Kwa ujumla, kitabu hiki kinasaidia sana kutafakari upya yale ambayo tumelazimishwa kuyakawaidisha katika sekta nzima ya habari.
Tafsiri yake ni kwamba nyuma ya pazia la vyombo vya habari kuna vita vya ruzuku na kimaslahi, itikadi za kisiasa na chochoro za kimadaraka. Ni ukweli kuwa siasa na sera za vyombo vya habari na mitandao ya kijamii zina ushawishi na nguvu kubwa, ni kama mhimili mwingine wa dola usioonekana kwa macho.
‘Manufacturing consent’
Waandishi wa kitabu hiki wanatumia maneno ya kimombo, manufacturing consent, kuelezea kazi ya vyombo vya habari vya umma. Lakini ni nini maana ya maneno haya haswa? Kwa kifupi, na kwa tafsiri isiyo rasmi, tunaweza kusema manufactured consent ni mbinu inayotumika katika medani za siasa ili kuuteka umma, kuutoa na kudhoofisha nguvu na mamlaka yake ya kikatiba kama ndiyo wananchi; wenye nchi.
Waandishi wa hiki kitabu wanasema kuwa mbinu hii hujionesha pale ambapo umma hutolewa, au hupotezewa kujadili mambo yao ya maana na kupelekwa kwenye mijadala isiyo na msingi.
SOMA ZAIDI: Mchumi Jeffrey Sachs Anavyouchambua Umasikini Kwenye ‘The End of Poverty’
Nikitolea mifano ya hapa Tanzania, iliyo karibu nasi, tunaweza kuliona hili kwenye namna vyombo vya habari vyetu, kwa makusudi au kulazimishwa, vinaacha kujadili uhitaji wa katiba mpya, sheria huru na haki za uchaguzi, ukosefu wa ajira, rushwa na utekaji, badala yake vinajikita na habari zinazohusu michezo, ndoa ya msanii fulani au kujadili ubuyu, kulishwa porojo na udaku kama wasemavyo Wabongo. Na hizo habari za udaku ndizo zitasomeka kama ndizo breaking news. Ni siasa za viinimacho zinachezwa, yaani, kucheza karata ya mtawala kuupuza na kuupumbaza umma.
Kwa hiyo, hiyo ni mbinu ya kughilibu na kupotosha umma kwa kutumia vyombo vya habari, watu mashuhuri, na michezo ambayo ina mashabiki wengi. Kwa sababu, katika nyakati hizi za attention economy ile kupata attention na uungwaji mkono na umma ndiyo rasilimali yenye thamani kubwa. Vivyo hivyo, hii mbinu inajionesha pale ambapo mtawala anatengeneza tatizo halafu ghafla bin vuu anatumia tatizo hilohilo kama chombo cha kisaikolojia kulaghai na kuhadaa wananchi kwa kuleta suluhisho.
‘Propaganda model’
Kwenye kitabu hiki, propaganda model ndiyo muhtasari, yaani ndio kiini na injini ya ufanyaji kazi na ufanisi wa hii dhana nzima ya manufacturing consent. Propaganda ni aina ya mawasiliano, habari au matangazo yaliyotiwa chumvi sana yenye madhumuni ya kushawishi watu ili wabadili mawazo yao. Ili hilo lengo litimie, lazima kutengeneza mazingira ya uungwaji mkono na wananchi kwa wingi, ikiwezekana hata ‘kuwanunua.’
Kimkakati, hiyo ajenda hutengenezwa na kusukwa kwa kuvuta watu zaidi kihisia, ili ionekane ni ya maana na ni ya “kweli na ya kizalendo” hata kama kwa makusudi ni habari ya kupotosha na inaeleza upande mmoja tu wa shilingi. Propaganda ni mbinu za dola kudhoofisha harakati na ukombozi kamili wa wote. Tukirejelea mifano ya hapa kwetu, moja ya propaganda ambayo umma ulihadaliwa kwa nguvu ni kwamba ‘Wamasai’ wanahamishwa Ngorongoro ili kulinda hizo hifadhi!
Propaganda nyingi ambazo waandishi hawa wanazieleza ni zile zenye ajenda ovu na chuki, bila uwazi na ukweli wote, inayotengeneza mvutano au hata chuki kati yetu na wao. Kwa mfano, katika mazingira yetu, propaganda nyingi hasi na kuchafuana zitakuja wakati wa vuguvugu la uchaguzi. Hali kadhalika, kuna propaganda ambazo zinaweza kutumika kama mbinu za kivita. Kwa sasa tunazishuhudia nyingi zikienezwa na kupandikizwa kwenye vita kati ya nchi za Israel and Iran.
Kwa utafiti na uzoefu wa hawa waandishi, wanataja baadhi ya mazingira na vitu ambavyo vinastawisha na kuendeleza au kukawadaisha hii propaganda model, ikiwemo hali halisi ya umiliki wa vyombo vya habari. Wamiliki wa vyombo vya habari wengi ni wafanyabiashara na wanasiasa, hivyo wamewekeza huko ili kulinda maslahi na majina yao kwa gharama yoyote ile. Hivyo, waandishi mara nyingi wanaegemea na kutegemea upande wa hayo makundi yenye nguvu na ushawishi.
SOMA ZAIDI: ‘Animal Farm’ ya George Orwell Inavyotusaidia Kuelewa Dhana ya Uongozi wa Umma na Uwajibikaji
Vyombo vingi vya habari vinategemea sana matangazo ya kisiasa na biashara ili kuishi. Hivyo, habari zao lazima zipendelee wadhamini wa hayo matangazo. Zile habari zinazokosoa waziwazi hao wadhamini na biashara zao, basi hizo habari zinadhibitiwa.
Waandishi wa kujitegemea, taasisi au vyombo huru vinavyokosoa rushwa, utekaji na kutetea maslahi ya umma, kwa mfano, hupata mashambulizi ya kila namna, kuanzia kufunguliwa mashitaka, kupotezwa wao na kalamu zao, au hata kuhongwa ili tu vifunge midomo.
Katika mazingira kama yetu ambapo Serikali inajiingiza na kuweka mikono yake kila pahala, basi vyombo vingi vya habari vimefungwa mikono na vingine hadi kuuza uhuru wao, hivyo kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi, utaalamu na uhuru katika kuhabarisha, kuelimisha, kutafiti na kuchambua habari.
Kwenye hii propaganda utaambiwa, kwa mfano, kuwa wingi wa magazeti na vyombo vya habari mithili ya utitiri ni ishara ya ongezeko la uhuru wa habari. Hii siyo kweli hata kidogo. Ndio maana wananchi wanachukizwa na kukerwa na udhibiti wa kupitiliza wa vyombo vya habari na mitandao ya kijamii; wananchi wanaelewa lugha na mbinu za kipropaganda. Hivyo, wana uwezo wa kudadisi na kutafuta habari za uhakika na kweli ili kukwepa kulishwa ‘matango pori.’
Ujumbe wa kitabu leo
Kitabu hiki kina umuhimu sana leo, wakati huu, hasa hii dhana nzima ya propaganda na namna inavyofanya kazi, ukiitazama kiundani na upana inafikirisha zaidi. Hata leo, vyombo vingi vya habari vinafanya kazi kwa ridhaa na manufaa ya mashirika ya biashara na kuridhisha makuwadi wa soko huria.
Mitandao ya kijamii kama Facebook na TikTok inachuja habari na inachukua taarifa za watu hata bila ridhaa yao kwa maslahi ya kibiashara. Pia, leo kuna udhibiti na uchakataji wa taarifa kupitia algoriti, au algorithms, ambazo huwanyima watu fursa ya kufikiria nje ya chujio na mfumo uliowekwa.
SOMA ZAIDI: ‘Elimu Isipomkomboa Maskini, Basi Ndoto Yake ni Kuwa Mnyonyaji’
Kitabu kinakemea hatari ya habari nusu-nusu za kupikwa, bandia, za kueneza hofu kama ya ugaidi, udini, uchina. Kitabu kinaweka bayana na kuonya kuhusu udanganyifu unaoweza kufanywa kupitia vyombo vya habari hata katika nchi zinazojinasibu na kujinadi kuwa ni visiwa vya amani na demokrasia.
Waandishi wanatia hamasa na kutufungua macho wasomaji kuendelea na utamaduni wa kutafuta taarifa kwa kina, kupitia vyombo tofauti na mbadala, na kuendeleza tafakuri huru hata kama haziwaridhishi watawala.
Katika nchi nyingi za Afrika, uhuru wa vyombo vya habari bado ni mdogo sana, kuna changamoto zaidi. Hivyo, vyombo kila kukicha vinatengenezewa sheria za kubanwa na kutawaliwa na makucha ya Serikali. Serikali zinakuja na sheria kali ili kubana uhuru wa vyombo vya habari. Si ajabu kusikia kuwa habari za uchaguzi mwaka huu zinatangazwa na waandishi waliosajiliwa na Serikali tu, wakati waandishi wana sheria na maadili yao na taasisi zao. Ni kama Serikali inajipatia haki turufu katika kila jambo la umma.
Katika mfumo huu wa propaganda, kuna habari hazitangazwi, nyingine zinatangazwa nusunusu tu bila utafiti wala kina, na vyombo vingine vya habari vinafungiwa. Yote hayo ni kupunguza na kubana uhuru wa vyombo vya habari na kulinda maslahi ya watawala na wamiliki wa vyombo hivyo.
Jitihada za wananchi
Pamoja na juhudi za kudhibiti, kufungia na kuchuja habari, wananchi wanajitafutia njia mbadala ya kujihabarisha. Hii ni muhimu sana. Wananchi siyo wajinga kuwa wao ni wasindikizaji wa maendeleo na walaji tu wa habari, pia wao ni waandishi na washirika wa kujihabarisha na kujielimisha.
Sio wajibu wa umma kumfurahisha mtawala, hasa yule ambaye anahalalisha utapeli wa kisiasa. Umma unatakiwa kudahili na kusajili wanasiasa na kuwa macho, au vigilant, na jinsi hawa watumishi wanapokengeuka na kubadili sheria ili ziwape kinga na pale wanapokataa mabadiliko yenye manufaa kwa umma.
Na mwisho, waandishi wanaoonesha umuhimu wa kuendeleza utamaduni wa kudadisi, uhuru tunduizi uendelee. Ni hulka na silaha muhimu sana ili kutambua hizi mbinu za kifashisti za kuteka umma kwa hizo propaganda rafu na za bei chee!
Umma unatakiwa kujua na kukumbuka mtaji wa nguvu, hasa nguvu ya kura yake. Walishatusanua, magwiji wa falsafa ya siasa kama David Humes na wapigania haki za kiraia kama Frantz Fanon, Steve Biko, na wengine, kuwa watawala hawana nguvu yoyote ya kuushinikiza umma kufanya, au kutofanya, jambo fulani, mpaka umma ukubali wenyewe.
Watawala hawana madaraka kama wanavyotuaminisha na kututunisha. Wanachofanya ni mwendelezo wa kughilibu na kuitumia hiyo kama chombo cha kudhibiti umma.
Isaac Mdindile ni mwanaharakati wa haki za binadamu na mazingira. Kwa mrejesho anapatikana kupitia ezyone.one@gmail.com au X kama @IsaacGaitanJr. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.