Tangia CCM kupuliza rasmi kipenga cha mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuwania uteuzi hapo Jumamosi, Juni 28, 2025, majina mbalimbali ya wanachama wa CCM wamejitokeza kuchukua fomu kutafuta ridhaa ya chama chao ili waweze kupeperusha bendera katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba.
Zoezi hili la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuwania uteuzi linahusu nafasi Ubunge wa Jimbo, Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi, Ubunge wa Viti Maalum, Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Viti Maalum, Udiwani wa Kata au Wadi na Udiwani wa Viti Maalum.
Mjadala mkubwa umeibuka katika nafasi za Ubunge wa Jimbo kutokana na sababu mbalimbali. Lakini mojawapo ni kuwepo kwa majina ya vijana waliojitokeza kwenda kugombea katika majimbo ambayo wabunge wake wanaomaliza muda ni Mawaziri au Manaibu Waziri katika Serikali.
Baadhi ya vijana hao waliojitokeza ni pamoja na mwanasheria Davis Betram Komba ambaye amejitosa jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma ambalo mbunge anayemaliza muda wake ni mwanasiasa mkongwe nchini na Waziri wa Afya, Jenista Mhagama ambaye amekuwa mbunge wa Peramiho kwa miaka 20.
Komba baada ya kuchukua fomu siku ya Jumamosi Juni 28, 2025 alisema kuwa anaamini uongozi ni kupokezana kijiti, hivyo yeye kama kijana ameona wakati ni sasa kwa kuwa Bunge lijalo litakuwa Bunge ambalo litaanza sambamba na utekelezaji wa Dira Mpya ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
“Kila kizazi kina jukumu la kusaidia kutimiza ndoto ya pamoja ya maendeleo ya jamii,” amesema Komba.
Katika jimbo la Ubungo mkoani Dar es Salaam ambalo mbunge anayemaliza muda wake ni Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, kijana wa CCM Hamis Abeid Baruani ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM wilaya ya Ubungo tayari amechukua fomu Jumapili, Juni 29, 2025.
Hii ni mara ya pili kwa Baruani kujitosa kwenye kinyang’anyiro hiko ndani ya CCM ambapo mwaka 2020 hakufua dafu mbele ya Prof. Mkumbo ambaye alishinda katika kura za maoni na chama chake kumpitisha kuwa mpeperusha bendera ya ubunge jimbo la Ubungo.
Katika jimbo la Siha mkoani Kilimanjaro ambalo hivi sasa mbunge wake ni Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel kijana wa CCM, Kennedy Mmari amejitokeza kuchukua fomu siku ya Jumamosi, Juni 28, 2025, siku ambayo aliitaja kuwa mwanzo wa safari ya kusikiliza, kujifunza, na kutumikia kwa moyo wote.
“Nimelelewa Siha. Nimepitia changamoto zake, nimeiona thamani yake, na naamini sasa ni wakati wa kizazi kipya kutoa mchango wake.” amesema Mmari.
Ukiacha kwa baadhi ya mawaziri hawa, wapo vijana wa CCM waliojitosa katika majimbo ambayo wabunge wa sasa ni wanasiasa wakongwe, ikiwemo jimbo la Urambo ambalo mbunge anayemaliza muda wake ni Margaret Simwanza Sitta.
Katika jimbo hilo la Urambo kijana wa CCM Daud Ngassa ambaye ni mtaalamu wa wa Sayansi ya Vinasaba (DNA) kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali alichukua fomu ya ubunge Jumapili, Juni 29, 2025.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na makao makuu ya CCM, zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuwania kuteuliwa katika nafasi mbalimbali litahitimishwa siku ya Julai 2, 2025. Ambapo zoezi hilo litafuatia na vikao mbalimbali vya uteuzi vya ngazi husika ili kupatikana majina yasiyozidi matatu kwa kila nafasi ambayo yatapigiwa kura ya maoni na wajumbe wa ngazi husika.
SOMA ZAIDI: CCM na Ilani ya Uchaguzi ya 2025-2030: Ushindi Si Swali la ‘Je, Itashinda?’ Bali ‘Itashinda kwa Kiasi Gani?’
Katika hatua nyingine zoezi la uchukuaji fomu ya ubunge limezua gumzo baada ya majina ya vigogo mbalimbali kujitosa kwenye kinyang’anyiro, ikiwemo aliyekuwa Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, Dk Charles Mahera ambaye alikuja kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) naye amechukua fomu kusaka nafasi ya uteuzi ndani ya CCM jimbo la Butiama.
Wengine ni mwanasiplomasia Balozi Liberata Mulamula ambaye amechukua fomu Ubunge wa viti Maalum CCM vyuo vikuu, aliyekuwa mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania, Masanja Kadogosa kachukua Bariadi Vijijini, aliyekuwa Katibu Binafsi wa Rais John Magufuli, Ngussa Samike amechukua Sengerema na mtoto wa Hayati Magufuli Jesca Magufuli amechukua ubunge wa viti maalum CCM mkoa wa Geita.