The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Watoto Wetu Wanatazama na Kusikiliza Nini Wakati Huu wa Likizo?

Kadri watoto wanavyoendelea kurudia kuona au kusikiliza maudhui yasiyofaa, kama vurugu na lugha chafu ndivyo wanavyoanza kuyaona haya kama sehemu ya maisha ya kawaida.

subscribe to our newsletter!

Kipindi cha mapumziko ya kati ya mwaka kwa watoto wa shule kinaendelea. Watoto wengi wako nyumbani wakipumzika baada ya mihula mirefu ya masomo, lakini katika familia nyingi, hawako chini ya uangalizi wa karibu. Wazazi wapo kazini, wengine wamesafiri, na kwa wengi, simu, runinga au intaneti ndizo zimeteuliwa kuwa “walezi wa muda.”

Katika mazingira haya, mtoto anaweza kutumia masaa mengi kwa siku akitazama vipindi, filamu au video zinazopatikana mitandaoni, au kusikiliza muziki kwenye redio , YouTube, spotify n.k., bila muongozo wa mtu mzima. 

Hali hii inaweza kuonekana kama ya kawaida na ambayo haina madhara, lakini kwa kweli, ina athari kubwa kwa ukuaji wa kihisia na kijamii wa mtoto. Kadri watoto wanavyoendelea kurudia kuona au kusikiliza maudhui yasiyofaa,  kama vurugu, lugha chafu, dharau kwa wanawake, au ulevi ndivyo wanavyoanza kuyaona haya kama sehemu ya maisha ya kawaida.

Tafiti zinaonesha kuwa watoto wanaotumia muda mwingi kutazama filamu na muziki bila usimamizi huanza kuonesha mabadiliko ya tabia: hukasirika kwa haraka, huiga lugha zisizofaa, au hukosa huruma kwa wengine. Wengine hufikiri kwamba ili uwe “mwanaume kamili” au “binti wa mjini” ni lazima uongee au uvae kama walivyowaona kwenye video, au kusikia kwenye nyimbo. Hii ndiyo hali halisi tunayoshuhudia kwenye jamii zetu kila siku.

Kwa mantiki hiyo, ni wazi kwamba muziki na filamu vina ushawishi mkubwa kwa watoto.  Lakini ni muhimu tukumbuke: muziki na filamu si jambo baya. Vikiwa katika muktadha sahihi, vinaweza kuwa na mchango mkubwa kwa maendeleo ya mtoto. Filamu zenye mafunzo huweza kusaidia watoto kuelewa tofauti ya mema na mabaya, na hata kuwahamasisha kutimiza ndoto zao. Vivyo hivyo, nyimbo zenye ujumbe mzuri huweza kujenga maadili, kuimarisha lugha, na hata kusaidia watoto kueleza hisia zao.

SOMA ZAIDI: Pongezi kwa Akina Baba Wote Wanaojenga Taswira Mpya ya Kuwa Baba

Burudani inaweza pia kuwa daraja la mazungumzo kati ya mzazi na mtoto. Wimbo mmoja unaweza kufungua mazungumzo kuhusu mahusiano yenye heshima, au filamu moja ya familia inaweza kuchochea mjadala kuhusu haki, marafiki, au utatuzi wa migogoro. Ndiyo maana hatutaki kuzuia burudani; tunataka watoto wetu waweze kutambua maudhui yapi yanafaa na yapi hayafai.

Kama wazazi au walezi, hatuhitaji kutumia ukali au kuwakataza watoto kutokusikiliza mziki au kutazama filamu, bali tunaweza kuchagua njia ambazo tunaweza kushirikiana na kuwaelekeza watoto ka ukaribu.  

Tunapokaa na watoto wetu kutazama vipindi au kusikiliza nyimbo, hata ikiwa ni kwa muda mfupi, tuwape nafasi ya kujifunza kuchambua wanachokiona au kusikia. Tunaweza kuwauliza maswali kama, “Unadhani huyu mhusika alifanya jambo sahihi?” au “Ujumbe wa huu wimbo unakufundisha nini?” Kwa kufanya hivyo, tunawasaidia watoto wetu kujenga uwezo wa kuchagua kwa uelewa maudhui wanayotazama.

Tunaweza pia kuweka ratiba ya burudani na muda wa kutazama vipindi kwenye runinga, muda wa kucheza, muda wa kusoma, nk. Hii huwasaidia watoto kuwa na mpangilio wa siku na pia kupunguza utegemezi wa simu au runinga kama vyanzo pekee vya furaha na burudani. Hata kama hatupo nyumbani, bado tunaweza kutumia teknolojia kuweka mipaka. Simu na runinga nyingi zina vichujio vya wazazi, au parental controls, ambavyo vinaweza kusaidia kudhibiti maudhui wanayopata watoto.

Lakini zaidi ya teknolojia, ni mawasiliano kati yetu na watoto wetu yanayoweka msingi wa uaminifu. Watoto wanaohisi kuwa wanaweza kuzungumza nasi bila hofu, huwa tayari pia kusikiliza tunapowaongoza. Badala ya kusema tu, “Acha kusikiliza huu wimbo,” tunaweza kusema, “Mdundo wake ni mzuri, lakini ujumbe wake haujengi tutafute wimbo mwingine wa kusikiliza. ‘’ 

SOMA ZAIDI: Je, Tumefikiria Kulea Watoto Wanaojali Mazingira?

Kuna mama mmoja alisimulia jinsi mwanae wa kiume mwenye miaka 10 alivyopata tabia ya kutumia lugha chafu nyumbani. Alipokaa na kuzungumza naye, waligundua kuwa alikuwa anaiga kutoka kwenye kipindi alichokuwa anakitazama kila mchana akiwa peke yake nyumbani. 

Mama huyo alisema, “Nilijisikia vibaya, lakini nikajua si kosa lake, ni kosa langu mimi kutokufuatilia anachotazama. Tangu siku hiyo nimekua makini, tunaweka ratiba, na nilimweleza kwa nini maneno hayo si sahihi.” Mfano huu unaonesha wazi kuwa watoto huiga wanachokiona, na kwamba mzazi anayejali anaweza kubadilisha mwelekeo wa mtoto kwa njia ya mazungumzo na uwepo wa karibu.

Watoto wanatuangalia sisi. Wanajifunza zaidi kutokana na kile tunachofanya kuliko tunachosema. Kama sisi wazazi tunatetea filamu za vurugu, au tunashabikia nyimbo za kudhalilisha wanawake, basi tunapeleka ujumbe wa kuruhusu sumu hiyo ndani ya familia zetu. 

Lakini kama wazazi wa kweli, tuna fursa ya kipekee ya kukuza na kuimarisha mawasiliano na mahusiano yetu na watoto, pamoja na kujenga tabia njema kupitia burudani zenye mwelekeo. Tusiachie redio, mitandao au televisheni/runinga zilee watoto wetu. Tuwepo. Tuwaongoze. Tuwaulize. Tuwasikilize.

Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×
×