Dodoma. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema kinaendelea na mchakato wa kuwapata wagombea katika ngazi mbalimbali ambao watakagombea katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka 2025.
Akiongea na waandishi wa habari katika ofisi za makao makuu ya chama hicho Katibu wa NEC Itikadi Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa Amos Makalla amesema, wakati mchakato huo unaendelea ni muhimu wanachama na watia nia katika ngazi mbalimbali wakawa watulivu mpaka kamati kuu itakapo toa uamuzi wa mwisho.
“ Kwa utaratibu wetu na mchakato ndani ya Chama cha Mapinduzi mpaka sasa hakuna mtu aliyeenguliwa au kukatwa kama ambavyo inaripotiwa katika vyombo vya habari,” amesema Makalla.
Makalla amesema zaidi ya wanachama wa CCM 30,000 walijitokeza kugombea katika nafasi mbalimbali za uongozi ambazo zinajumuisha nafasi ya Ubunge, Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na Udiwani.
Kwa mujibu wa utaratibu mpya wa CCM majina ya watia nia watatu kwa ngazi za Ubunge wa majimbo na udiwani yatarudishwa kwa wajumbe kwa ajili ya kupigiwa kura ya maoni ili chama hiko kiweze kupata mpeperusha bendera.