The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Humphrey Polepole Ajiuzulu Ubalozi Nchini Cuba: ‘Nakosa Amani ya Moyo na Imani Katika Uongozi Niliopo Ndani Yake Sasa’

“Kwa kuwa siwezi kuendelea kuwa sehemu ya uongozi usiohamasika na utii wa misingi ya katiba ya nchi na chama, haki, maadili, utu na uwajibikaji kwa wananchi, nimeamua kwa hiari yangu kujiuzulu nafasi yangu ya uongozi na utendaji serikalini.”

subscribe to our newsletter!

Aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Hesron Polepole, amemwandikia barua Rais Samia Suluhu Hassan akimweleza kuhusu uamuzi wake wa kujiuzulu kwenye nafasi hiyo, kwa kile mwanadiplomasia huyo amekiita “kukosa amani ya moyo na imani katika uongozi” aliopo ndani yake kwa sasa.

Kwenye barua hiyo ya Julai 13, 2025, iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii, Polepole, ambaye pia alikuwa Mkuu wa Kituo cha Uwakilishi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Havana – Cuba, pamoja na uwakilishi wa eneo la Karibe, Amerika ya Kati na nchi rafiki za Colombia, Venezuela na Guyana, ameeleza yafuatayo kama sababu ya kuchukua hatua hiyo:

“Kwa muda wote wa kuhudumu ndani na nje ya nchi, nimefuatilia kwa karibu na kushuhudia kwa masikitiko makubwa mwelekeo wa uongozi usiojielekeza ipasavyo katika kusimamia Haki za watu, Amani na kuheshimu watu, kufuata kwa dhamira ya kweli na uwajibikaji wa dhati wa kushughulikia kero na changamoto zao, na kudidimia kwa maadili ya uongozi katika ngazi mbalimbali. 

“Kudhoofika kwa utekelezaji wa majukumu ya msingi ya serikali kwa ajili ya ustawi wa wananchi; mambo haya yanateteresha maslahi mapana ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Haya yote yamezidi kunifanya nikose amani ya moyo na imani katika uongozi niliopo ndani yake sasa.

“Matukio ya hivi karibuni ya wazi ya kukiuka misingi, utamaduni na desturi za Chama cha Mapinduzi (CCM) – hususan katika mchakato wa uteuzi wa wagombea ndani ya Chama ambao kwa kila awamu huwa msingi wa kukihuisha Chama na fursa ya kufanya Mageuzi ambayo kwa pamoja hukipa chama sura ng’aavu mbele ya umma kabla ya uchaguzi; desturi hii ya kufanya mageuzi ndani ya chama imekuwa nguzo muhimu ya ukubalifu na ushindi wa CCM mbele ya umma. Imekuwepo kauli maarufu ya CCM isemayo ‘Chama kwanza mtu baadaye,’ mwanzoni mwa mwaka huu, nilipoona kauli hii inafanyika vinginevyo, nimejiuliza mara kadhaa ni maslahi ya nani yanapiganwa wakati huu, mtu, kikundi au Chama Taasisi?

SOMA ZAIDI: Sasa ni Wakati wa Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania Kuwa ya Kijasiri Zaidi 

“Kwa kuwa siwezi kuendelea kuwa sehemu ya uongozi usiohamasika na utii wa misingi ya katiba ya nchi na chama, haki, maadili, utu na uwajibikaji kwa wananchi, nimeamua kwa hiari yangu kujiuzulu nafasi yangu ya uongozi na utendaji serikalini.”

Polepole, ambaye amewahi kuhudumu pia kama Mbunge wa kuteuliwa wa Bunge la Jamhuri wa Muungano, Mkuu wa Wilaya, na hata Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, aliteuliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2022 kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi kabla ya kuhamishiwa nchini Cuba hapo 2023.

Uteuzi wake mwaka 2022 ulikuja wakati Polepole, aliyepata kuhudumu kama Mjumbe wa Kamati ya Mabadiliko ya Katiba, akiwa moja kati ya watu wachache kutoka CCM waliokuwa wakiukosoa uongozi wa Rais Samia, aliyeingia madarakani Machi 19, 2021, kufuatia kifo cha mtangulizi wake, John Magufuli, hadharani.

Kupitia kipindi chake cha runinga kilichokuwa kinarushwa kwenye mtandao wa YouTube, Shule ya Uongozi, Polepole alikuwa akitoa maoni yake kuhusiana na mwelekeo wa nchi kiuongozi, akikemea rushwa na ufisadi, akitahadharisha kuhusu uwepo wa “wahuni” kwenye uongozi, kauli iliyompatia umaarufu sana mitandaoni.

Mnamo Disemba 17, 2021, hata hivyo, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilikifungia kipindi hicho kwa muda usiyojulikana kwa madai ya kuchapisha “habari za uongo,” huku Polepole mwenyewe akieelezea hatua hiyo kama moja wapo ya changamoto za “kusema ukweli.”

Kumshukuru Rais

Kwenye barua yake hiyo ya kujiuzulu ya Julai 13, ambayo nakala pia imetumwa kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Polepole amemshukuru Rais Samia kwa kumuamini kwa kumpatia wadhifa huo ambao aliupokea kwa “heshima.”

SOMA ZAIDI: Viongozi Hawa Kumi wa Tanzania Watakuhamasisha Kupenda Kusoma Vitabu

“Nilipokea kwa heshima kubwa uteuzi na dhamana uliyonipa kuwa mwakilishi wa nchi yetu katika ngazi ya kimataifa,” anaandika Polepole kwenye barua hiyo. 

“Niliamini na ninaendelea kuamini iliikuwepo kusudi na kazi muhimu ya kuyashika, kuyasimika, kuyasimamia, kuyaimarisha na kuyaendeleza maslahi mapana ya nchi yetu katika maeneo ya uwakilishi ulinipa dhamana ya kuyasimamia,” anaongeza mwanadiplomasia huyo. “Ni heshima kubwa na isiyopimika kuaminiwa kuwa Mwakilishi wako, Nchi yetu, Taifa letu, wananchi na Mamlaka ya nchi. Kwa hili, nasema asante.”

Polepole amesema ataendelea kuwa mwana CCM wa kawaida, “mzalendo na raia mwaminifu kwa Taifa na nchi yetu.”

“Ninamwamini Mungu wa Mbinguni na ninahamasika na tumaini kuu kwamba siku moja nchi yetu itaongozwa kwa misingi ya haki, maadili, usimamizi thabiti wa milko na nidhamu ya uongozi, dhamira njema, siasa safi, uongozi bora na hofu ya Mungu,” alimalizia Balozi Polepole.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×
×