Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) siku ya Jumamosi, Julai 12, 2025 kilitoa taarifa ya viongozi wake wawili ambao ni wajumbe wa sekretarieti ya chama hiko taifa kuwa wamekamatwa nchini na Jeshi la Polisi katika maeneo tofauti walipokuwa kwa ajili ya safari ya nje ya nchi.
Viongozi hao ni Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA, Bi Brenda Rupia ambaye kwa mujibu wa taarifa ya chama hiko alikamatwa mpakani Namanga alipokuwa akielekea nchini Kenya.
Mwingine ni Mtaalamu wa Rasilimali Watu, Miradi na Uwekezaji wa CHADEMA Leonard Joseph Magere aliyekamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere alipokuwa akielekea nchini Uingereza.
Jeshi la Polisi kwa nyakati tofauti limethibitisha kuwakamata maafisa hao wawili wa CHADEMA kwa kueleza kuwa wanakabiliwa na tuhuma. Wameeleza kuwa wamemkamata Bi. Brenda kwa mahojiano kutokana na tuhuma za kutoa taarifa za uongo na uchozezi, huku Magere akiwa na tuhuma za makosa ya jinai.
CHADEMA wameeleza kuwa viongozi hao wawili walikuwa kwenye safari za kuhudhuria vikao pamoja na mafunzo nje ya nchi baada ya chama hiko kupewa mwaliko.
Ikumbukwe pia mwezi Mei Naibu Katibu Mkuu Bara wa CHADEMA, Amani Golugwa naye alikamatwa Uwanja wa Julius Nyerere alipokuwa safarini kwenda Ubelgiji kwa madai ya tuhuma zilizokuwa zinamkabili.
Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche Kupitia ukurasa wa mtandao wa X amehoji namna Jeshi la Polisi kuwakamata viongozi hao wakiwa safarini, ilihali ni watu wanaofahamika kwa anuani zao, hivyo wangeweza kuitwa muda wowote.
“Kwamba viongozi wenye anuani, wapo kila siku. Wana tuhuma za jinai, hamjawahi kuwakamata au kuwaita kujieleza, mpaka siku wanaposafiri Uwanja wa Ndege ndio mnakumbuka makosa yao kupitia uhamiaji,” amehoji Heche.