Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa inatarajia kukutana siku ya Jumamosi, Julai 19, 2025 kwa ajili ya kikao cha kawaida kitakachofanyika jijini Dodoma kuanzia saa nne asubuhi.
Kikao hiko ambacho kitaongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan kitatanguliwa na kikao cha sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM inayoendelea kuketi jijini Dodoma kuendelea na mchakato wa mchuo wa watia nia ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya ajenda za kikao cha Kamati Kuu.
Mchakato huu wa uteuzi unaoendelea kwa sasa ngazi ya taifa unahusu uteuzi wa wagombea kuwania nafasi ya Ubunge wa Jimbo, Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi, Ubunge wa Viti Maalum na Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Viti Maalum.
Taarifa ya CCM kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Jumatatu, Julai 14, 2025, ilieleza kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi aliongoza kikao cha kawaida cha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ambayo inatajwa kufanya kazi ya kupokea na kuchambua majina ya watia nia wa nafasi hizo.
Kikao cha Kamati Kuu kinachotarajia kufanyika kitakuwa ndio kikao cha juu cha mchujo wa watia nia kwa ajili ya uteuzi wa wagombea wa CCM, ambapo majina machache yatarudishwa kwa wajumbe wa majimboni na jumuiya za chama hiko kwa ajili ya kura za maoni.