Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe akizungumza baada ya uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 (Dira 2050) ulioongozwa na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan jijini Dododoma amesema kazi ya uundaji wa Dira iliyofanyika ni mwanzo mzuri na kinachotakiwa ni utekelezaji ili kuondoa tofauti zilizoshuhudiwa huko nyuma.
Mwanasiasa huyo mkongwe wa upinzani nchini amesisitiza kuwa salama au kesho ya iliyo bora kwa taifa la Tanzania itapatikana kwa kuweka tofauti za kiitikadi, imani, dini na kabila pembeni ili kujenga taifa moja la watu wenye mshikamano.
Tangu Januari 21, 2025 ulipomalizika Mkutano Mkuu wa CHADEMA na kushindwa kwenye uchaguzi na Mwenyekiti wa sasa wa CHADEMA Tundu Lissu, mwanasiasa huyo amekuwa akionekana na kuzungumza kwa nadra sana, jambo ambalo leo liliibua gumzo mitandaoni baada ya kuonekana katika hafla ya uzinduzi huo.
“Mimi binafsi nisingeweza kukataa kuja kwenye uzinduzi huu, kwa sababu kama tunaitaka kesho iliyo bora zaidi, lazima tufike mahali tuchore mstari tuseme kuna makosa tumeshayafanya, tunayarekebishaje tuweze kusonga mbele vema zaidi,” amesema Mbowe.
Amesema ameenda kwenye uzinduzi huo baada ya kupewa mwaliko na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo, na pia kwa kuwa alitoa maoni ya Dira wakati akiwa Mwenyekiti wa CHADEMA kama makundi mengine yalivyofikiwa kutoa maoni. Hivyo asingeweza kukataa mwaliko.
“Kwa hiyo tukaona ni haki kuangalia kama tulitoa maoni tukaangalia yale maoni yamepokelewa kwa kiwango gani,” amesema Mbowe, “ Hatujasoma kwa undani ripoti yenyewe lakini tutaifanyia kazi.”
Mbowe amesisitiza kuwa kitakachoweza kuhakikisha Dira 2050 inafanya kazi kweli ni endapo waliopo madarakani watakuwa na moyo wa kusema ukweli, moyo wa kukiri pale ambapo watakuwa wamefanya makosa ama wanafanya makosa.
Amesema hii itasaidia kuondoa tofauti na kurekebisha maeneo yote yanayopata malalamiko ya wadau mbalimbali, makundi mbalimbali ya kisiasa na yasiyo ya kisiasa.