Mara nyingi tunasema kwamba watoto ni waigizaji wazuri lakini je, tumewahi kufikiria wanachoiga ni nini? Kutoka namna tunavyoongea na kuongelea wengine, jinsi tunavyokabiliana na changamoto, hadi maamuzi tunayofanya kila siku, yote yanaunda maisha yao ya baadaye.
Tafiti zinaonesha kwamba watoto hujifunza zaidi kutokana na kile tunachofanya/kutenda kuliko kile tunachosema. Nadharia ya Social Learning ya Albert Bandura inathibitisha hili: watoto huangalia, huiga, na baadaye hutumia tabia walizoona nyumbani kama mwongozo wa maisha yao.
Hebu tuangalie tabia 10 za maisha ambazo watoto wetu hujifunza kutoka kwetu na nini tunaweza kufanya kuonesha mfano bora.
Uongeaji, kukabiliana na migogoro
Watoto wanajifunza namna ya kuwasiliana na kuyakabili mambo kwa kutuona sisi. Tukipiga kelele au kufunga milango kwa hasira, nao hujifunza kufanya hivyo. Tukiepuka kuzungumza kuhusu hisia, nao huona kama si kawaida kuzungumzia matatizo.
Tufanyeje?
Tukisikilize kwa makini bila kuwakatisha wanapoongea. Tuepuke kutumia matusi au sauti za juu (kufoka), hasira na maneno ya kejeli na fedheha tunapokbili changamoto mbele yao.
Badala yake, tuseme “Najisikia vibaya au sijafurahishwa kwa sababu…” ili waone na kuiga njia ya heshima ya kutatua na kukabiliana na changamoto na kujenga mahusiano bora na watu wanaowazunguka.
SOMA ZAIDI: Je, Tunawafundisha Watoto Wetu Kuchagua Chakula Bora?
Tuwafundishe huruma kwa kuuliza, “Unafikiri mwenzio anajisikiaje?” pale wanapohitilafiana na kutumia namna isiyo na utu kutatua changamoto.
Kazi, uwajibikaji
Watoto wanaangalia namna tunavyoshughulikia majukumu yetu, kuanzia kazi zetu hadi kazi ndogo za nyumbani. Tukikwepa majukumu, nao watayakimbia. Tukijitahidi, nao watajifunza kufanya bidii.
Tufanyeje?
Tuwape kazi rahisi kama kufagia, kumwagilia bustani, au kutoa vyombo mezani baada ya kula. Tusipongeze matokeo pekee, bali jitihada pia. Tuseme, “Hongera kwa kujaribu kwa bidii.”
Watuone tukitimiza ahadi na kumaliza kazi tulizoanza. Pia tuhakikishe wanaona upambanaji wetu na kujali muda katika kutekeleza majukumu yetu katika mazingira ya nje na nyumbani.
Tabia za kula
Tunapochagua vyakula, tunawafundisha watoto. Wakitukuta tunakula vyakula ambavyo sio vizuri kwa afya zetu kila siku, wataona hivyo ndivyo kawaida. Lishe njema hujengwa nyumbani.
Tufanyeje?
SOMA ZAIDI: Tudhibiti Hasira Zetu Tunapokerwa na Watoto. Mwongozo Huu Utatusaidia Kufanikisha Hilo
Tule chakula cha familia pamoja mara kwa mara. Tuwahusishe watoto kupanga mlo au kununua mboga sokoni. Tuwaeleze kwa lugha rahisi kwa nini matunda na mboga ni bora kuliko vyakula vyenye mafuta na vya sukari.
Kutumia Pesa
Tafiti zinaonesha kwamba tabia za kifedha huanza kabla ya miaka saba. Tukitumia fedha zetu bila mpangilio, nao watakua bila nidhamu ya kifedha.
Tufanyeje?
Tuwape poket money na tuwafundishe kuipangilia, kwa mfano, sehemu ya kutumia, sehemu ya kuweka akiba. Tuwahusishe kwenye mipango midogo midogo ya kifedha nyumbani, kama kuweka akiba kwa ajili ya zawadi ya kifamilia.
Tuwe wawazi kuhusu sababu ya kuweka akiba au kipaumbele kwa mahitaji muhimu.
Kujitunza
Kama hatujipi muda wa kupumzika au kujali afya zetu kwa kula vizuri na kufanya mazoezi, watoto hujifunza kuwa kujitunza si muhimu. Afya ya mwili na akili inahitaji mfano mzuri.
Tufanyeje?
SOMA ZAIDI: Watoto Wetu Wanatazama na Kusikiliza Nini Wakati Huu wa Likizo?
Tulale kwa wakati, tufanye mazoezi, na kula chakula bora. Tuseme tunapochoka: “Nahitaji kupumzika kidogo ili nipate nguvu tena.” Tushirikiane nao katika shughuli zinazojenga afya, kama matembezi ya jioni au michezo ya nje.
Wema na huruma
Watoto hufuata mfano wetu. Tukiwadharau watu na kuwazungumzia vibaya wengine, huku tukiwahimiza watoto kuwa wawe watu wema, hawataamini maneno yetu.
Tufanyeje?
Tuwatendee wema na kuwaonesha heshima watu wote haswa wale wanaotoa huduma kama wahudumu wa nyumbani, duka, walinzi au dereva wa nyumbani na hata wa daladala, na kadhalika.
Tusiseme maneno mabaya kuhusu watu au kuwadharau na kuwafokea mbele ya watoto. Tufanye matendo mazuri pamoja na watoto kama kusaidia wenye uhitaji, kusaidia jirani, au kumwandikia mtu barua ya shukrani, kuwazungumzia watu vizuri na kushukuru mtu anapotuhudumia.
Kushughulikia ‘stress’
Tukiwafokea watu tunapokasirika au kubaki kimya huku tukiumia, watoto huiga tabia hizo. Hawataweza kutafuta njia za afya za kukabiliana na changamoto watakazozipitia.
SOMA ZAIDI: Pongezi kwa Akina Baba Wote Wanaojenga Taswira Mpya ya Kuwa Baba
Tufanyeje?
Tukipata msongo wa mawazo, tuchukue hatua za kujituliza, kama kupumua kwa kina au kutembea na tuwaelezee tunachofanya, ili waelewe. Tuwafundishe kutafuta suluhu badala ya kukata tamaa. Tuwaoneshe kuwa kuomba msaada si udhaifu bali ni nguvu.
Kujifunza
Kama sisi wenyewe hatupendi kujifunza na tunachukulia elimu kama adhabu, nao wataiona hivyo. Lakini tukionesha hamasa ya kujifunza zaidi, nao watapenda kujifunza.
Tufanyeje?
Tuwe na muda wa kusoma pamoja kila siku, hata dakika 15. Tusikilize maswali yao na tushirikiane kutafuta majibu. Tujifunze kitu kipya kama familia: kupika mapishi mapya, kujifunza maneno ya Kiswahili sanifu, au hata lugha nyingine.
Usafi
Nyumba yenye fujo na ambayo haina tamaduni ya usafi huwafanya watoto kuona hali hiyo ni kawaida. Mazingira yenye mpangilio hujenga nidhamu na utulivu.
SOMA ZAIDI: Je, Tumefikiria Kulea Watoto Wanaojali Mazingira?
Tufanyeje?
Tupange mifumo rahisi: nguo chafu zinenda kwenye vikapu vya nguo, ratiba ya kusafisha chumba chao, kupanga nguo zao ndogondogo wenyewe. Tufanye usafi kuwa jambo la kufurahisha tuwawekee muziki na tuwapongeze wanaposhiriki.
Mtazamo kuhusu maisha
Tukilalamika kila wakati, watoto watakua na mtazamo hasi kuhusu maisha yao. Watoto wenye mtazamo chanya hujenga uimara na kufanikisha mambo yao kwa ufanisi zaidi, kulingana na utafiti wa chuo kikuu cha Harvard.
Tufanyeje?
Tuwe tunafanya ibada ya shukrani: kila mmoja aseme kitu kimoja kizuri kilichotokea siku hiyo. Tusiwe walalamishi, haswa mbele ya watoto badala yake, tuwaoneshe kuwa changamoto za maisha ni kitu cha kawaida na zinaweza kutatuliwa na tuwafundishe kuwa na tumaini hata katika matatizo.
Jukumu la malezi ni kuchukua hatua ndogo ndogo kila siku. Watoto wetu hawahitaji wazazi wakamilifu, wanahitaji wazazi wanaojitahidi. Tabia ndogo ndogo tunazoonesha leo zitakuwa urithi wa maisha yao kesho.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.