Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere na aliyekuwa msaidizi wa Rais wa kwanza wa Tanzania, Joseph Butiku, ametoa maoni yake juu ya mjadala ulioibuka kuhusu mchakato wa uteuzi wa mgombea wa Urais ndani ya CCM.
Butiku ameeleza kuwa ingawa kulikua na makosa katika taratibu, amesema makosa hayo yamefanyika nia ikiwa njema, na kusisitiza maamuzi yaliyofanyika ni halali kwa kuwa Mkutano Mkuu ulikua ni chombo kilichoweza kufanya maamuzi.
Butiku ameongea haya, katika kipindi cha Dakika 45 cha kituo cha ITV. Ambapo Butiku alitupa lawama kwa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete kwa yale aliyoyasema kuwa ushauri wake ulisababisha makosa hayo ya kiutaratibu.
“Safari hii kulikuwa na kasoro kidogo ambazo zimetokea wanasema taratibu hazikufuatwa. Niwe mkweli kwa kiwango fulani ni kweli, isingekuwa kweli usingesikia matatizo ambayo hayajawahi kutokea. Huu sio uchaguzi wa kwanza tumeanza uchaguzi 1965, miaka mingi tumepita katika chaguzi na CCM imekuwa wote tunakwenda vizuri,” ameeleza Butiku katika mahojiano hayo.
Akieleza juu ya utaratibu Butiku, anafafanua kuwa utaratibu wa kupata mgombea kwanza huanza kwenye Kamati Kuu, Halmashauri Kuu baadae Mkutano Mkuu. Anafafanua zaidi kuwa hata hivyo kwa wakati huu wajumbe waliitwa katika mkutano mkuu wa Januari 2025, kwa malengo tofauti na uteuzi wa mgombea. Hata hivyo hoja ya uteuzi iliweza kuibuka hapo baadae katika mkutano huo ambao nay eye alikua mshiriki.
“Sasa pale [Katika Mkutano Mkuu] safari hii ikatokea kidogo ni kama utaratibu wa Bunge wa hoja binafsi, mjumbe mmoja akasimama akapendekeza kwamba tuyamalize hapa hapa, sisi si ndio wakubwa, sisi si ndiyo wenyewe, tuyamalize hapa hapa wakamuunga mkono,” anaeleza Butiku.
Hata hivyo Butiku alitupa lawama kwa ushauri uliotolewa na Mzee Jakaya Kikwete, baada ya hoja hiyo ya kufanya uteuzi wa mgombea wa Urais kutolewa.
“Kama uliona, nimtetee mwenyekiti, kama ulion, mwenyekiti wetu mama Samia kidogo alijua utaratibu kidogo akasema mmh [akasita] akatokea mzee mmoja akasema ngoja nikusaidie Mwenyekiti akamruhusu, Mzee Kikwete akaeleza, akasema sisi si ndio sisi, ndio wakasema sisi ndio sisi. Wakafanya ule uamuzi [kwa] nia njema.”
“[Hata hivyo] utaratibu huu wa hoja binafsi ya mjumbe katika mkutano mkuu hatuna katika chama, haipo, mwenyekiti wetu alisita sita kidogo lakini alishauriwa akakubali na mimi simlaumu hata kidogo,” aliendelea kufafanua Butiku.
“Wako wakongwe wa chama waliokuwa wamekaa pale. Wakaja baadae na utaratibu wa pale pale kuhalalisha kile kilichotokea, wameanzia juu kwenye Mkutano Mkuu baadae sasa kwa agizo la Mkutano Mkuu wamekwenda chini kufuata utaratibu, hilo ndio tatizo,” aliongeza.
Butiku anaongeza ingawa kulikua na makosa ya kiutaratibu, hasa kwenye kutoa hoja binafsi, maamuzi yaliyofanywa na Mkutano Mkuu ni halali. Akieleza kuwa hakuna aliyepinga maamuzi yaliyofanyika katika mkutano ule. Butiku aliendelea kusisitiza makosa hayo ya kiutaratibu ni madogo, yachukuliwe kwa kuangalia ukuaji wa kidemokrasia.
“Na mimi nadhani ni tatizo dogo katika nchi zetu ndogo hizi vyama vyetu vichanga hivi katika utaratibu tulioanza nao, tunajifunza katika kuishi katika mazingira ya vyama vingi na mazingira ya chama chenye kanuni. Ni dogo lazima tuwape benefit of doubt ya makosa madogo madogo, wote tunakosea hata katika familia zetu,” aliongeza.
“Tusilaumiane, tukubali kwamba tunakua na haya yaliyotokea na yale yaliyotokea na pengine yale yatayotokea yatusaidie kujifunza maana halisi ya demokrasia,” alisisitiza zaidi.