Mamlaka ya Mapato Tanzania imetoa mwezi mmoja kwa wafanyabiashara wanaofanya baishara zao mitandaoni kujisajili kwa ajili ya kulipa kodi.
Haya yameelezwa leo Julai 24, 2025, katika uzinduzi wa utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano (MoU) kati ya TRA na Shirika la Kimataifa linashughulika na masuala ya Kodi (IBFD) ambao umefanyika katika Chuo cha Kodi (ITA)
Akieleza juu ya suala hilo, kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda ameeleza kuwa mamlaka hiyo imeweza kujiimarisha kiujuzi ili kwenda sambamba na mabadiliko ya uchumi wa kidigitali ambapo baadhi ya makampuni makubwa ya kidigitali hutoa huduma na kuwezesha biashara bila kuwa na makazi rasmi ndani ya nchi.
“Tumetoa mwezi mmoja kuanzia tarehe 1 Agosti mpaka tarehe 30, wale wanaofanya biashara na makampuni haya wakiwemo wenye nyumba wanazopangisha kupitia Airbnb na hawajajisajili TRA, hawachangii chochote tumewapa muda wa kuwawezesha wajisajili na wachangie kwa sababu hawajasamehewa kuchangia kulipa kodi,” alieleza Mwenda.
Mwenda amaeeleza kuwa katika mwezi mmoja huo watafanya kampeni ya kutoa elimu nchi nzima.
“Wako wanaofanya biashara za online, anauza vitu, ameweka stoo nyumbani kwake, ameacha kuwa na duka kama wenzake walivyonavyo na wao hawajasamehewa kulipa kodi.Kama kipato chao kinazidi kwa mwaka milioni nne wanapaswa na wao kulipa kodi,” alieleza zaidi Mwenda.
Kamishna Mwenda maefafanua kuwa baada ya mwezi mmoja kuisha ambao watauwa hawajajisajili watakuwa wamefanya makosa kwa mujibu wa sheria na watatozwa penati.