Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza kufanya Mkutano Mkuu Maalum hapo Julai 26, 2025, utakaofanyika kwa njia ya mtandao, huku agenda kuu ikielezwa kuwa ni kufanya marekebisho madogo ya Katiba ya chama hicho tawala nchini Tanzania.
Mkutano huu unaweka rekodi katika historia ya chama hicho, ikiwa ni mara ya kwanza kwa chama hicho kilichotawala nchini kwa takriban miongo sita kufanya Mkutano Mkuu mara tatu katika mwaka wa uchaguzi. Pia, hii inakuwa mara ya kwanza kwa CCM kufanya Mkutano Mkuu kwa njia ya mtandao.
Hata hivyo, akiongea na waandishi wa habari leo Julai 25, 2025, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla, ameeleza kuwa mkutano huo unafanyika kimtandao kwa mujibu wa Katiba.
“Kwenye Katiba yetu, sisi tunaruhusiwa kwa vikao hivyo kufanya mkutano kwa njia ya mtandao,” Makalla alieleza kwenye mkutano wake na wanahabari uliofanyika Dodoma. “Na ajenda kubwa ya Mkutano Mkuu huu maalum ni marekebisho madogo ya Katiba. Kwa hiyo, agenda ya Mkutano Mkuu huu maalum ni moja tu: marekebisho madogo ya Katiba.”
Mkutano huu maalum unafanyika kwa njia ya mtandao kufuatia marekebisho ya Kikatiba yaliyofanyika mnamo Mei 29, 2025. Hata hivyo, wakati wa kufanya marekebisho hayo Mwenyekiti wa CCM, Samia Suluhu Hassan, alieleza kuwa vikao ambavyo vitaanza kutumia njia hiyo ni mikutano na kamati za siasa, au halmashauri kuu za siasa za mikoa au za wilaya.
“Kwa hiyo, tumekuja na wazo la e-meetings, mikutano ya kimtandao, ambayo idara ya oganizesheni inapendekeza vikao vifuatavyo kwa njia ya mtandao,” Rais Samia alieleza.
“Kikao cha kwanza ni sekretariati ya wilaya; Kamati ya siasa wilaya; Sekretarieti ya mkoa; Kamati ya siasa mkoa; Sekretarieti ya kamati maalum ya halmashauri kuu ya CCM taifa; Sekretarieti ya halmashauri kuu ya CCM taifa; Kamati maalumu ya halmashauri kuu ya CCM taifa; Kamati kuu ya halmashauri kuu ya CCM; Halmashauri kuu ya CCM taifa; Mkutano mkuu wa taifa,” aliongeza Samia, ambaye pia ni Rais wa Tanzania.
“Hivi vikao vingine tumeviweka kwa kujua kwamba jinsi tunavyoendelea huko mbele tutakuwa tunaendelea kiteknolojia na kwamba Katiba yetu inatupa fursa ya kutunga kanuni za vikao hivi,” alifafanua Rais Samia. “Lakini kwa sasa tumeanza mikutano na kamati za siasa au halmashauri kuu za siasa za mikoa au za wilaya. Lakini mikutano ile haimo katika maelekezo ya katiba ya chama chetu.”
Mkutano huu Mkuu Maalum uliotangazwa rasmi leo, haukuwa kwenye ratiba rasmi iliyotangazwa na chama hicho mnamo Julai 23, 2025, na hata ratiba kabla ya hapo baada ya mkutano uliopita. Hata hivyo, ratiba ya chama hicho kuelekea uchaguzi ilibadilika baada ya kikao cha Kamati Kuu cha uteuzi wa watia nia kilichopangwa Julai 19, 2025, kuahirishwa kutokana na sababu za kiufundi.
Alipoulizwa kuhusu marekebisho yanayotegemewa kufanyika kwenye Katiba, Makalla alieleza kuwa jambo hilo litajulikana kesho.
“Naomba niwathibitishie maandalizi ya mkutano huu yamekamilika,” alifafanua Makalla. “Katika wilaya zetu, katika mikoa yote na kesho tutakuwa na mkutano huo na kazi yetu kama sekretarieti ni kufanya maandalizi ya kufanyika kwa mkutano huu.”
“Niwathibitishie kwamba maandalizi yamekwenda vizuri na kesho mtashuhudia Chama cha Mapinduzi kikifanya Mkutano Mkuu wa Taifa Maalumu wa chama kwa njia ya mtandao,” Makalla alisisitiza zaidi. “Dunia inabadilika na chama hiki kinathibitisha ukongwe wake, uimara wake na kwenda na wakati.”