Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimefanya mabadiliko madogo ya Katiba yake ya mwaka 1977 (toleo la Mei 2025) kupitia mkutano mkuu maalum wa Taifa uliofanyika kwa njia ya mtandao, Julai 26, 2025, ambapo sasa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa inaweza kupeleka majina zaidi ya matatu ya watia nia wa chama hiko ngazi ya Ubunge na Uwakilishi Zanzibar kwa ajili ya kupigiwa kura za maoni.
Kifungu cha Katiba ya CCM kilichofanyiwa marekebisho ni Ibara 105(7) F inayohusu majukumu ya Kamati Kuu katika mchakato wa uteuzi wa wagombea wa CCM ngazi ya Ubunge na Ujumbe Baraza la Wawakilishi. Kifungu hiko kimeongezewa maneno “isipokuwa kama Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa itaamua vinginevyo.”
Ibara hiyo hivi sasa inasomeka kama, “Kufikiria na kuteua majina ya wana CCM wasiozidi watatu kwa kila jimbo la uchaguzi, walioomba nafasi ya Ubunge na Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi ili wakapigiwe kura za maoni, isipokuwa kama Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itaamua vinginevyo.
Mabadiliko haya yanakuwa nyongeza ya mabadiliko ya mfumo wa uteuzi wagombea wa CCM wa nafasi za dola yaliyofanywa katika mkutano mkuu wa mwezi Mei, 2025 uliofanyika jijini Dodoma.
Akizungumzia mapendekezo hayo madogo ya uchaguzi kabla ya wajumbe kupiga kura, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Samia Suluhu Hassan amesema kuwa wamelazimika kurudi kwenye mkutano mkuu kufanya mabadiliko hayo kutokana na mwitikio mkubwa wa wanachama waliojitokeza kuomba ridhaa ya kuwa wagombea wa CCM, hivyo isingekuwa sawa kurudisha majina matatu kwa wajumbe kama Katiba inavyosema.
“Tulitanua demokrasia kwa kutaka wajumbe wa kuchagua wawe wengi zaidi, jambo lile limevutia wana CCM wengi kuomba kugombea,” amesema Mwenyekiti wa CCM Samia, “Kwa maana hiyo kuna maeneo yana wagombea wengi hadi 39, hadi 40. Kwa hiyo tumeona kwenda na watatu kati ya watu wengi hao si jambo la busara.”
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na CCM, katika nafasi za ubunge wa majimbo 272 ya uchaguzi nchini, watia nia 3,585 wameomba ridhaa ndani ya chama ambapo kwa upande wa Tanzania Bara na 524 upande wa Zanzibar. Kati ya watia nia hao ambao jumla yao ni 4,109, walioenda majimboni wanawake ni 263.
Kwa upande wa Uwakilishishi kwenye Baraza la Wawakilishi Zanzibar waliochukua fomu ni 503.
SOMA ZAIDI: CCM Yaeleza Sababu ya Kufanya Mkutano Mkuu wa Ghafla Kwa Njia ya Mtandao: ‘Marekebisho Madogo ya Katiba’
Kwa mujibu wa ratiba ya CCM vikao vya mchujo vitaendelea Julai 27, 2025, ambapo Kamati ya Usalama na Maadili ya CCM Taifa itakaa kupitia majina ya watia nia wote wa Ubunge na Uwakilishi Zanzibar, kisha Kamati Kuu itafanya mchujo Julai 28, 2025 kupatikana kwa majina yatakayopelekwa kupigiwa kura za maoni na wajumbe Agosti 4, 2025.
Mabadiliko haya ya Katiba ya CCM yamehusu pia uteuzi wa wagombea kwa ngazi ya udiwani ambapo Ibara ya 91(6)C imefanyiwa marekebisho na kuwezesha majina ya uteuzi kuweza kupelekwa zaidi ya matatu kwa wajumbe kwa ajili ya kupigiwa kura za maoni. Lakini kutokana na mchakato wa uteuzi wa majina matatu kwa ngazi ya udiwani ulishafanyika, Mwenyekiti wa CCM ameeleza kuwa hakuta kuwa na mabadiliko ya awali.