Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewasili mjini St George, katika visiwa vya Grenada jana Julai 27, 2025, ambapo anategemewa kushiriki katika Jukwaa la nne la Kibiashara na Uwekezaji kati ya Afrika na Karibiani litakalofanyika kuanzia Julai 28 na kumalizika Julai 30.
Hii inamaanisha Majaliwa atakosa kushiriki kikao cha uteuzi cha watia nia wa nafasi za Ubunge CCM, ambapo, yeye ni mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho.
Majaliwa pia hakuonekana kuungana na viongozi wenzake waandamizi katika Mkutano Mkuu uliofanyika Julai 26, 2025, kwa njia ya mtandao ambapo viongozi waandamizi wa CCM walikutana katika ukumbi wa mkutano wa NEC (White House) Makao Makuu ya CCM, Jijini Dodoma.
Katika Mkutano Mkuu wa mwezi Mei 2025, taarifa ya utekelezaji wa ilani 2020-2025, iliwasilishwa na Naibu Waziri Mkuu Doto Mashaka Biteko, kwani Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alikuwa kwenye ziara ya kikazi nchini Japan.
Majaliwa alitangaza kubadili mawazo ya kugombea katika jimbo la Ruangwa katika siku ya mwisho ya uchukuaji fomu za uteuzi mnamo Julai 02, 2025, ambapo alieleza kuwa mabadiliko ni jambo la kawaida.