Wabunge wa Viti Maalum 13 kutoka ‘Kundi la Wabunge 19’ waliofukuzwa CHADEMA mwaka 2020 ambao walitangaza kujitosa CCM na kuomba nafasi za kuteuliwa ubunge na ubunge wa viti maalum katika uchaguzi mkuu 2025 wamepitishwa kwenye mchujo uliofanywa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM Taifa, hivyo wanaenda kwenye hatua inayofuata ya kura za maoni.
Akitangaza majina ya wanachama wa CCM waliopita katika chujio la Kamati Kuu leo Julai 29, 2025, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla amewataja wananchama wa CCM 11 waliotoka kundi la wabunge 19 waliopita kwenye mchujo wa ubunge wa majimbo na wawili wamepita kwenye mchujo wa ubunge wa viti maalum ngazi ya mkoa.
Waliopita katika mchujo wa ubunge ni pamoja na Esther Matiko jimbo la Tarime Mjini, Esther Bulaya jimbo la Bunda Mjini, Nusrati Hanje jimbo la Ikungi Mashariki, Jesca Kishoa jimbo la Iramba Mashariki, Hawa Mwaifunga jimbo la Tabora Mjini na Cecilia Paresso jimbo la Karatu.
Wengine ni Kunti Majala jimbo la Chemba, Grace Tendega jimbo la Kalenga, Felister Njau jimbo la Moshi Vijijini, Sophia Mwakagenda jimbo la Rungwe na Stella Fiyao jimbo la Ileje. Kwa upande wa viti maalum ni Salome Makamba anayegombea viti maalum mkoa wa Shinyanga na Tunza Malapo anayegombea viti maalum mkoa wa Mtwara.
Watia nia hawa watakwenda kupambana na wenzao waliotangazwa kwenye kura za maoni zinazotarajia kupigwa na wajumbe wa CCM hapo Agosti 4, 2025.