Mamlaka ya Mapato Tanzania imetangaza msamaha wa adhabu kwa magari yanayotumiwa na yaliyopo nchini lakini yanachangamoto mablimbali za kikodi, msamaha huu ulioanza Agosti 01 na kumalizika Disemba 31, 2025, utahusu magari yale yaliyo kwenye makundi haya:
(i) Magari yaliyoingizwa nchini kwa muda (temporary importation) na yameendelea kukaa nchini
(ii) Magari yaliyoingia Tanzania Bara kutokea Zanzibar bila kufuata taratibu za kiforodha
(iii) Magari yaliyoingizwa nchini kwenda nchi nyingine (transit) na yakabakizwa nchini
(iv) Magari yaliyosamehewa kodi lakini umiliki wake umehamishwa kwa watu wasiostahili kupewa msamaha
(v) Magari yaliyoingizwa nchini kwenda nchi nyingine ambayo muda wake umeisha na hayakupata kibali cha nyongeza kukaa nchini
Katika taarifa iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, Mamlaka hiyo imeeleza kuwa imekuwa ikipata changamoto za usimamizi wa magari hayo ambayo hayakulipiwa ushuru na kodi wakati wa kuingizwa nchini. Hivyo TRA imetangaza rasmi kipindi cha msamaha kuanzia Agosti 01, 2025 mpaka Disemba 31, 2025, ambapo wamiliki wa magari husika watatakiwa kujitokeza kulipa ushuru na kodi huku riba na adhabu vyote vikisamehewa.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 70(1) cha Sheria ya Utawala wa Kodi Sura 438 na Kifungu cha 249 cha Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mshariki ya mwaka 2004, Kamishna Mkuu wa Mamlaka anatoa Msamaha wa kodi kwa wamiliki wa magari ya aina iliyotajwa…ambayo yaliingizwa nchini kwa kujua au kutokujuwa kwamba hayakulipiwa ushuru na kodi husika,” imeleza taarifa hiyo kutoka TRA.
“Katika kipindi cha msamaha, wamiliki wa magari husika watawajibika kulipa kiasi cha ushuru na kodi husika, kiasi cha riba na adhabu vyote vitasamehewa,” taarifa hiyo imeendelea kufafanua.
TRA imeeleza kuwa magari yaliyo kwenye makundi tajwa yatakayokamatwa baada ya tarehe 31 Disemba 2025, ambayo ushuru na kodi zake hazikulipiwa kikamilifu yatashughulikiwa kwa mujibu wa sheria ikiwemo mashtaka ya jinai huku wahusika wakitakiwa kulipa ushuru na kodi, ikiwa ni pamoja na adhabu na riba.