Urafiki kwa mtoto si jambo dogo. Ni moja kati ya mambo ya kwanza yanayojenga uelewa wake wa dunia, namna ya kujiamini, kuwasiliana na wengine, na kuelewa thamani yake binafsi. Watoto hujifunza mengi kupitia marafiki zao, lakini pia wanaweza kuumia sana kupitia urafiki ambao sio mzuri. Kama wazazi au walezi, tuna jukumu la kuwasaidia kuelewa tofauti kati ya urafiki wa kweli na ule ambao sio wa kweli.
Tunapowafundisha watoto wetu kuchagua marafiki kwa busara, tunawasaidia siyo tu kuwa salama, bali pia kuwajengea misingi ya heshima binafsi, huruma kwa wengine, na ujasiri wa kusema “hapana” pale inapohitajika.
Katika makala hii, tutapitia kwa kina jinsi tunavyoweza kuwasaidia watoto wetu kutambua urafiki mzuri ni upi, kuwatambua marafiki wenye tabia ambazo hazijengi, na namna ya kuwa marafiki wema bila kupoteza sauti yao wenyewe.
Kwa nini urafiki ni msingi wa maisha kwa mtoto?
Tafiti mbalimbali, zikiwemo za jarida la Child Development, zimeonesha kuwa watoto wenye marafiki wazuri wa karibu hujenga uwezo mkubwa wa kukabiliana na msongo wa mawazo, hubaki na hali bora ya afya ya akili, na mara nyingi huwa na matokeo mazuri zaidi shuleni.
SOMA ZAIDI: Kwa Nini Mtoto Wako Analia Sana?
Urafiki wa kweli huwa kama kizingiti dhidi ya dhoruba za maisha, hasa wakati wa migogoro ya kifamilia, mabadiliko ya shule, au hata pale mtoto anapokumbana na unyanyasaji.
Kwa lugha nyepesi, rafiki wa kweli humfanya mtoto ajisikie salama, na kupendwa kwa jinsi alivyo.
Watoto wengi wanapoambiwa wawe na marafiki, huwa hawapati mwongozo wa kutambua nani anafaa kuwa rafiki. Tunaweza kutumia hadithi, vipindi vya watoto, au tukio halisi walilopitia kuwasaidia kuona tofauti kati ya urafiki unaojenga na ule unaobomoa.
Maswali kama, “Unajisikiaje ukiwa na fulani?” au “Unajisikia huru kusema mawazo yako ukiwa naye?” yanawasaidia kufikiria kwa kina. Kwa njia hii, wanajifunza kusikiliza sauti yao ya ndani inayowaambia kama wako kwenye nafasi salama au la.
Tuwafundishe pia kutambua urafiki unaowaumiza. Siyo kila urafiki unaleta faraja. Wapo watoto wanaojikuta wakidhalilishwa na rafiki zao, wakilazimishwa kufanya mambo ambayo hawapendi, au wakitishiwa kuachwa nje ya kundi kama asipo fanya jambo flani. Aina hizi za tabia huweza kuwa na athari za muda mrefu kwenye hali ya mtoto ya kujiamini na uwezo wake wa kuweka mipaka.
SOMA ZAIDI: Tabia Kumi Ambazo Watoto Wetu Hujifunza Kutoka Kwetu
Ni muhimu watoto wetu wafahamu kwamba siyo jambo zuri kumcheka rafiki, kumlazimisha afanye mambo kinyume na matakwa yake, au kumwambia asiongee na watu wengine kwa sababu sisizo za msingi. Tunapaswa kuwaambia kwa uwazi kuwa urafiki wa kweli hauumizi moyo. Akianza kuhisi huzuni kila mara anapokutana na rafiki fulani, huenda hiyo si urafiki wa kweli.
Tuwasaidie kuwa marafiki wema bila kuwa watu wanao kubali kufanya kila kitu.
Watoto wengi hupenda kupendwa. Na mara nyingine, katika kutaka kukubalika, hujikuta wakijinyima ili tu wafurahishe wengine. Hii mara nyingi ndiyo mbegu ya “people pleasing” tabia ya kusema “ndiyo” kila wakati hata kama moyoni hawataki.
Tunapaswa kuwafundisha watoto kua watu wenye ukarimu lakini hiyo haimaanishi kusahau wao ni nani. Tunaweza kuwapa maneno ya kutumia wanapolazimishwa kufanya kitu ambacho hawataki kufanya, kama vile, ‘’Sitaki kufanya kitu hiko, kwasababu…….’’ “Sijisikii vizuri kufanya jambo hilo kwasababu….” Lugha za kusimamia hisia zao kwa heshima, ni silaha inayojenga uwezo wa kusema hapana kwa upendo.
Watoto wetu waelewe kuwa ni jambo la kawaida urafiki fulani kuisha. Watoto wengine hujilaumu, na wengine hupoteza imani kwa watu. Tuna jukumu la kuwaambia kuwa baadhi ya marafiki huja kwa muda na wengine hubaki kwa muda mrefu. Tunaweza kuwaambia kwa maneno rahisi, “Kuna baadhi ya watu mlioelewana na mlikua marafiki zamani, lakini sasa hamuongei tena hiyo ni sehemu ya maisha, na si kosa la mtu yeyote.”
SOMA ZAIDI: Je, Tunawafundisha Watoto Wetu Kuchagua Chakula Bora?
Pia, tuwape nafasi ya kufikiri wenyewe. Sio kila changamoto kati yao na marafiki zao linahitaji sisi kuingilia. Badala ya kutatua matatizo kwa niaba ya mtoto, tuwe washauri. Tuwe watu wa kusikiliza na kumuuliza, “Ungependa kusema nini?” au “Ungependa nkusaidieje?” Mtoto anayepata nafasi ya kufikiria suluhisho mwenyewe hujifunza kuwajibika na kujiamini.
Hivyo basi tuwakumbushe kuwa hawahitaji kubadilika ili wapendwe. Marafiki wa kweli watakubali utu wao, mapungufu yao, furaha yao, na mipaka yao. Urafiki wa kweli huleta nuru, si giza. Tuwaambie watoto wetu kwamba hawatakiwi kupambana kupendwa bali wanapaswa kupendwa kwa kuwa wao ni wao.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.