The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Panga la Wajumbe CCM Lilivyowashughulikia Wabunge, Naibu Mawaziri. Kazi Imebaki Vikao vya Mchujo Baada ya Kura ya Maoni

Katika wabunge walioangukia pua katika mchakato huo wa kura za maoni, wapo wabunge wakongwe waliokaa bungeni kwa zaidi ya miaka 20, lakini pia wapo wabunge ambao wamehudumu kwa kipindi cha muhula mmoja tu. Lakini kubwa zaidi ni zaidi ya Naibu Mawaziri saba wameangushwa na kuachwa mbali kwa kura kwenye majimbo yao.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Siku ya Jumatatu, Agosti 4, 2025 Chama Cha Mapinduzi(CCM) kiliendelea na mchakato wa ndani wa uteuzi wa wagombea watakaopeperusha bendera ya chama hiko kwenye uchaguzi mkuu kwa nafasi za ubunge wa jimbo, uwakilishi na udiwani ambapo wajumbe wa mkutano wa jimbo na kata walipata nafasi ya kupiga kura za maoni.

Katika kura za maoni za ubunge zilizopigwa katika majimbo mbalimbali nchini imeshuhudia zaidi ya waliokuwa wabunge 40 wa bunge lililoisha wakishindwa kufua dafu kwenye sanduku la kura za maoni zilizopigwa na wajumbe wa CCM ngazi ya jimbo husika.

Katika wabunge walioangukia pua katika mchakato huo wa kura za maoni, wapo wabunge wakongwe waliokaa bungeni kwa zaidi ya miaka 20, lakini pia wapo wabunge ambao wamehudumu kwa kipindi cha muhula mmoja tu. Lakini kubwa zaidi ni zaidi ya Naibu Mawaziri saba wameangushwa na kuachwa mbali kwa kura kwenye majimbo yao.

Naibu Mawaziri waanguka

Naibu mawaziri waliokutana na panga la wajumbe ni pamoja Alexander Mnyeti ambaye ni mbunge Misungwi mkoani Mwanza na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi. Kwenye kura za maoni Mnyeti meangushwa na Salvatory Luboja Sylvester aliyepata kura 9,680 dhidi ya kura 3,249 alizopata.

Geophrey Pinda aliyekuwa mbunge wa jimbo la Kavuu mkoani Katavi ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi ameangushwa kwenye kura za maoni na Laurent Luswetula aliyepata kura 1,564. Pinda ameshika nafasi ya tatu, kwani  nafasi ya pili ameshika Bi. Pudensia Kikwembe kura 1,065 huku Pinda akiambulia kura 1,032.

Jumanne Sagini aliyekuwa mbunge wa jimbo la Butiama mkoani Mara ambaye pia Naibu Waziri wa Katiba na Sheria ameangushwa kwenye kura za maoni na mpinzani wake Wilson Mahera aliyepata kura 4,295 dhidi ya kura 2,341 alizopata. Wilson Mahera aliyeshinda amewahi kuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Uchaguzi katika uchaguzi mkuu uliopita na badae kushika wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia anayeshughulikia elimu.

SOMA ZAIDI: CCM Yakamilisha  kura za Maoni ya Uchaguzi Viti Maalum Makundi Mbalimbali, Kivumbi  Majimboni Leo

Cosato Chumi aliyekuwa mbunge wa Mafinga Mjini mkoani Iringa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ameangushwa kwenye kura za maoni na Dickison Lutevele aliyepata kura 1,219 dhidi ya kura 376 alizopata.

Exaud Kigahe aliyekuwa mbunge wa Mufindi Kaskazini ambaye ni Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara naye ameangushwa kwenye kura za maoni na Luqman Merhab aliyepata kura 3,795 dhidi ya kura 488 alizopata Naibu Waziri huyo. 

Naibu Mawaziri wengine walioangushwa ni pamoja na Stanslaus Nyongo aliyekuwa mbunge wa Maswa Mashariki mkoani Simiyu na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji. Dastan Kitandula aliyekuwa mbunge wa jimbo la Mkinga mkoani Tanga na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii.

Wabunge walioanguka

Kwa upande wa wabunge yupo aliyekuwa mbunge wa jimbo la Nzega Vijijini mkoani Tabora Dkt. Hamisi Kigwangalla ambaye amekuwa mbunge  tangu mwaka 2010 na kuwahi kushika nyadhifa ya Naibu Waziri na Waziri wakati wa utawala wa awamu ya tano. Dkt Kigwangalla ameachwa nyuma ya Neto Kapalata aliyeshinda kura za maoni kwa 2,570 dhidi ya kura 1,715.

Vita Kawawa  wa jimbo la Namtumbo mkoani Ruvuma ameangushwa na Juma Zeberi Homera aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya. Homera ameongoza kwa kura 11,836 dhidi ya kura 852 alizopata Kawawa. Kawawa ambaye ni mtoto wa Waziri Mkuu wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rashid Mfaume Kawawa, amekuwa mbunge wa Namtumbo kwa miaka 20 tangu alipoingia bungeni mwaka 2005.

Jesca Msambatavangu  aliyekuwa mbunge wa jimbo la Iringa Mjini mkoani Iringa ambaye aliingia bungeni kwa mara ya kwanza 2020 ameshika nafasi ya nne kwenye sanduku la kura za maoni. Aliyeshinda Iringa Mjini ni Fadhili Ngajilo lura 1,899 akifuatiwa na Wakili Moses aliyepata kura 1,523, Mchungaji Peter Msigwa kura 477 huku Msambatavangu akiambulia kura 408.

Deo Kasenyenda Sanga aliyekuwa mbunge wa Makambako mkoani Njombe ameshindwa kwenye kura za maoni  na aliyekuwa Katibu Mkuu wa zamani wa CCM na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo aliyepata kura 6,151. Deo Sanga maarufu kama Jah People alishikilia jimbo hilo kwa miaka 15 aliachwa mbali kwa kupata kura 470.

SOMA ZAIDI: Panga la Kamati Kuu CCM Lawashukia Wabunge Zaidi ya 40. Hawataonekana Kwenye Kura za Maoni CCM

Dr. Charles Kimei  aliyekuwa mbunge wa jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro tangu mwaka 2020 ameangushwa kwenye kura za maoni na Enock Zadock Koola aliyepata kura 1,999 dhidi ya Kimei aliyepata kura 861. Dkt Kimei kabla ya kuwa mbunge alikuwa akihudumu katika sekta ya fedha kama mkurugenzi mtendaji wa moja ya benki kubwa ya biashara nchini Tanzania.

Charles Mwijage  wa jimbo la Muleba Kaskazini mkoani Kagera ambaye amekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa miaka 15 ameangushwa na Adonis Bitegeko. Mwijage amewahi kuwa Waziri katika Serikali ya awamu ya tanno.

Wengine walioangushwa ni Constantine Kanyasu jimbo la Geita Mjini,  Emmanuel Adamson Mwakasaka jimbo la Tabora Mjini, Jumanne Kishimba jimbo la Tabora Mjini, 

Hamida Abdallah jimbo la Lindi Mjini, Profesa Patrick Ndakidemi jimbo la Moshi vijijini, Issa Jumanne Mtemvu jimbo la Kibamba,  Stella Manyanya jimbo la Nyasa.

Dkt Medard Kalemani jimbo la Chato Kaskazini, Bonophase Butondo jimbo la Kishapu, Antipasto Mgungusi jimbo la Malinyi, Nicholas Ngasa jimbo la Igunga Mjini,  Hassan Mtenga jimbo la Mtwara Mjini, Innocent Bilakwate jimbo la Kyerwa na Tumaini Magesa  aliyekuwa mbunge wa Busanda akigombea jimbo la Katoro.

Matokeo hayo ya kura ya maoni yanasubiri uamuzi wa mwisho wa vikao vya juu vya CCM ikiwemo kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa(NEC)  kinachotarajia kufanya uteuzi Agosti 22, 2025 baada ya kupokea maoni ya kikao cha Kamati Kuu ya NEC inayotarajia kukaa Agosti 20, 2025.

Vikao hivyo vitatanguliwa na kikao cha Kamati ya siasa za majimbo vitakavyowajadili wagombea hao leo Agosti 6, 2025 na kupeleka mapendekezo yake kwenye kamati za siasa za wilaya, kisha kamati za siasa za mikoa ambazo nazo zitapeleka mapendekezo yake ngazi ya taifa.

Habari hii imechangiwa na waandishi wa The Chanzo Ibrahim Mgaza na Victoria Kavishe

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×