Aliyekuwa mjumbe wa mkutano mkuu CHADEMA taifa kutoka wilaya ya Kigamboni Yericko Nyerere, ambaye leo ametangaza kuhamia Chama cha Ukombozi wa Umma(CHAUMMA) amesema kuwa wanahama na dhana ya ‘No Reforms, No Election’ aliyomaanisha Mwenyekiti wa zamani wa CHADEMA Freeman Mbowe.
Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam katika ofisi za CHAUMMA, Yericko amesema kuwa dhana ya ‘No Reforms, No Election’ aliyomaanisha mwenyekiti huyo wa zamani wa CHADEMA ililenga hasa kujipanga kuhakikisha wanadhibiti hujuma kwenye uchaguzi ikiwemo kwa kuunda vikundi vya vijana katika ngazi za kuanzia kata watakaoweza kudhibiti hujuma dhidi ya wagombea kwenye uchaguzi ikiwemo.
“Kwa nadharia ileile na kwa msimamo uleule ya kwamba ‘No Reforms, No Election’ tunaingia katika uchaguzi maana yake kwamba natangaza nitagombea ubunge jimbo la Kigamboni, amsema Yericko, “Agenda yetu ni ileile ya kuhakikisha hakuna mgombea anayeenguliwa ndani ya CHAUMMA,” amesema Yericko.
Amedai kuwa kwa sasa dhana ya ‘No Reforms, No Election’ ya CHADEMA imekosa uhalisia kwani haiwezekani kuzuia uchaguzi ambao upo kikatiba na chama hiko hakina mkakati wowote wa kutekeleza hilo.
Amemtuhumu Mwenyekiti wa sasa wa CHADEMA Tundu Lissu ambaye kwa sasa yupo mahabusu kwa kesi ya uhaini na uchochezi kuwa ndiye aliyekuja na tafsiri tofauti ya dhana ya ‘No Reforms, No Election’ alipochukua uongozi mwezi Januari kupelekea kukaribisha mashambulizi kutoka kwa dola.
Yericko ambaye amedai pia amekuwa mshauri wa kisiasa wa Mbowe wa muda mrefu, alikuwa mmoja wa vinara wa kampeni wa mwenyekiti huyo wa zamani wa CHADEMA kwenye uchaguzi wa kihistoria wa chama hiko uliofanyika Januari mwaka huu ambapo Tundu Lissu aliibuka mshindi.
Sambamba na Yericko Nyerere, aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Hai na mgombea udiwani Machame katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, James Mbowe naye ametangaza kuhamia CHAUMMA kwa kueleza kuwa uongozi wa sasa wa CHADEMA umekosa mwelekeo na chama hiko kipo hatua ya kuelekea kifo hakiwezi kuwa sawa tena.
“Hakuna jambo lolote linalofanyika, kwenye ngazi ya msingi kama nilivyosema, ngazi ya taifa, ngazi ya jimbo, wilaya hakuna kinachofanyika chochote. Shughuli pekee iliyopo ya CHADEMA leo ni kesi iliyopo Mahakama Kuu au kesi iliyopo Mahakama ya Kisutu ndio utawaona viongozi pale kupiga picha na kusinzia,” amesema James.
James amesema kuwa kwa kipindi chote wamekuwa wakivumilia matusi anayoshambuliwa Freeman Mbowe ambaye amekuwa kimya huku viongozi wa sasa wa CHADEMA wakiangalia bila kukemea, hivyo wameamua kujitenga na aina hiyo ya siasa.
Akizungumzia suala la ukimya wa Freeman Mbowe amesema kuwa ni sahihi kwani hata Mbowe alipochukua uenyekiti hawakuwahi kumlilia mwenyekiti mstaafu Edwin Mtei awe anazungumzia masuala ya CHADEMA wanapokutana na misukosuko.
“Wenye wajibu wa kuivusha hii taasisi sio viongozi wastaafu, ni wale waliopo madarakani,” amesema James.
James naye ametangaza kugombea ubunge jimbo la Hai kwa akisema kuwa kama mwanasiasa anawajibika kutafuta jukwaa kwa ajili ya kutimiza malengo na ndoto ambazo tayari alikuwa akijiandaa nazo kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.
“Mimi kama mwanasiasa wajibu wangu wa kwanza ni kuhakikisha napambana kwa gharama kuwawakilisha wale ambao natamani niwawakilishe,” amesema James.