Dar es Salaam. Mahakama Kuu haikua sahihi kutengua uamuzi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala uliowapa ushindi wasanii wa muziki Hamisi Mwinyijuma maarufu Mwana FA na mwenzake Ambwene Yesaya au AY dhidi ya kampuni ya simu ya MIC Tanzania Public Limited Company, sasa Honora Tanzania Public Limited Company.
Hii ni kwa mujibu wa hukumu ya Mahakama ya Rufani iliyosomwa leo Alhamisi, Agosti 7, 2025, na Jaji wa Mahakama ya Rufani Latifa Alhinai Mansoor jijini Dar es Salaam mbele ya mawakili waliokuwa wanawakilisha pande hizo mbili kwenye kesi hiyo iliyoanza mwaka 2012.
Kwenye uamuzi wake, Mahakama ya Wilaya ya Ilala iliiagiza kampuni ya MIC, sasa Honora, inayoendesha mtandao wa simu wa Tigo, kuwalipa Mwana FA na AY Shilingi 2,185,000,000 baada ya kukubaliana nao kwamba kampuni hiyo imekiuka hakimiliki yao kwa kutumia muziki wao kama mlio wa simu bila idhini yao, pamoja na maagizo mengine.
Hata hivyo, kampuni hiyo haikuridhishwa na uamuzi huo, ikakata rufaa Mahakama Kuu, ikidai kwamba Mahakama ya Wilaya ya Ilala haikuwa na nguvu ya kisheria ya kusikiliza shauri hilo, kwani kiwango cha fidia kinachohusika kinapita kile kilichowekwa kisheria, wakiuita uamuzi huo batili.
Kwenye Kesi ya Rufaa ya Madai Na. 112 ya mwaka 2019, Mahakama Kuu ilikubaliana na hoja za kampuni ya MIC, sasa Honora, na kutengeua uamuzi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, pamoja na kuweka pembeni amri ilizotoa, ikiwemo ile ya Mwana FA na AY kulipwa mabilioni hayo ya fedha na kampuni hiyo ya mitandao ya simu.
Uamuzi huu wa Mahakama Kuu, hata hivyo, haukuzingatia ule wa Mahakama Kuu wa mwaka 2011 ya kulipiga chini shauri hilo hilo lilipoletwa mbele yake kwa mara ya kwanza, ikieleza kwamba yenyewe haina nguvu za asili za kisheria za kusikiliza mashauri yanayohusiana na hakimiliki, uamuzi uliowapelekea Mwana FA na AY kupeleka shauri hilo Mahakama ya Wilaya ya Ilala walikopata ushindi.
Ni uamuzi wa Mahakama Kuu, kwenye Kesi ya Rufaa ya Madai Na. 112 ya mwaka 2019, wa kutengeua maamuzi ya Mahakama ya Wilaya ya Ilala uliowapeleka Mahakama ya Rufani Mwana FA na AY ambayo uamuzi wake wa hapo Alhamisi uliwapatia ushindi, ikisema uamuzi huo wa Mahakama Kuu haukua sahihi, ikiielekeza isikilize kesi upya kwa kuzingatia madai ya wasanii hao.
Hoja ya msingi ya Mahakama ya Rufani ni kwamba kwa sababu Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki ya Tanzania inaipa Mahakama ya Wilaya nguvu ya kisheria kusikiliza mashauri yote yanayohusiana na hakimiliki, haijalishi kiwango cha fedha kinachohusika, Sheria ya Mahakama za Mahakimu, inayotoa nguvu za kisheria kwa mahakama za awali kusikiliza mashauri ya aina fulani, haiwezi kutumiwa.
“Sheria inapotoa nguvu mahususi ya kisheria kwa mahakama fulani, nguvu hiyo mahususi hutengua masharti mengine ya kiujumla ya kisheria yanayohusiana na nguvu za mahakama kusikiliza mashauri ya aina fulani,” Mahakama ya Rufani inasema kwenye hukumu yake.
“Hii maana yake ni kwamba, kama sheria fulani inasema waziwazi kwamba mahakama itakuwa na nguvu ya kusikiliza shauri fulani mahususi, hiyo sheria mahususi ndiyo itakayokuwa inafanya kazi, na zile za masharti ya kiujumla kuhusu nguvu za mahakama kusikiliza mashauri fulani hazitafanya kazi,” inaeleza Mahakama ya Rufani.