Dodoma. Baada ya kumkabidhi fomu mgombea wa Chama cha Mapinduzi, Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Jacobs Mwambegele amewakabidhi fomu wagombea wengine wawili wanaotegemea kuingia kwenye kinyang’anyiro cha Urais kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Wagombea waliokabidhiwa fomu ni pamoja na Hassan Kisabya Almas wa chama cha National Reconstruction Alliance (NRA) aliyefika pamoja na mgombea mwenza Hamis Ali Hassan.
Akizungumza na waandishi wa habari punde baada ya kuchukua fomu hiyo, Kisaby alisema kuwa NRA kina matumaini matatu kuelekea uchaguzi huo ambao licha ya kuhusisha wagombea Urais, pia utahusisha uchaguzi wa wabunge na madiwani.
Kisabya ameyataja matumaini hayo matatu kuwa ni Mungu, wananchi wanaowachagua na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, itakayotangaza matokeo. Mgombea huyo amesisitiza kwamba kipaumbele cha NRA ni amani, kwamba hawapo tayari kuharibu amani kwa ajili ya uchaguzi.
Wagombea wengine waliokabidhiwa fomu ni Kunje Ngombare Mwiru wa chama cha Alliance for Africa Farmers Party (AAFP), aliyefika pamoja na mgombea mwenza Chumu Abdallah Juma. Wagombea hao watatakiwa kutafuta wadhamini na kurudisha fomu hizo kwa ajili ya uteuzi wa Tume kama wamekidhi vigezo vyote.
Kwa mujibu wa taarifa ya Tume, hadi janaAgosti 08, 2025, Tume ilipokea barua kutoka katika vyama vya siasa kumi na nne (14) zikiainisha tarehe na muda ambao wanachama wa vyama vyao waliowapendekeza kugombea nafasi za Kiti cha Rais na Makamu wa Rais watafika ofisi za Tume zilizopo Njedengwa Jijini Dodoma kwa ajili ya kuchukua Fomu za Uteuzi.