Kampuni ya kichina Zijin Mining imesaini mkataba na serikali ya Tanzania kuendesha eneo la mizigo la Bandari ya Kigoma na pia geti la Malindi katika bandari ya Dar es Salaam.
Hafla fupi ya kusaini makubaliano hayo ilifanyika katika hoteli ya Johari Rotana Jijini Dar es Salaam mnamo Agosti 05, 2025. Waliohudhuria katika hafla hiyo ni pamoja na Waziri wa uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Ludovick Nduhiye, na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Plasduce Mbossa. Wengine waliohudhuria ni Makamu wa Rais wa Kampuni ya Zijin Mining, Lin Hongying na Balozi wa China Tanzania, Chen Mingjian.
Zijin Mining ambayo inaendesha migodi mikubwa ndani ya DR Congo inaeleza hatua hii ni moja ya ubunifu wa kampuni hiyo kurahisha usafirishaji.
“Ili kukabiliana na changamoto hizi za usafirishaji, kampuni ya Zijin imepanga njia bora ya usafirishaji wa pamoja kwa kutumia maji na nchi kavu kupitia korido hii ya mashariki,” inasomeka taarifa ya Zijin Mining baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo.
“Bidhaa za madini zitapelekwa kwa barabara hadi Bandari ya Kalemie nchini DRC, kisha kusafirishwa kwa meli kuvuka ziwa hadi Bandari ya Kigoma nchini Tanzania,” taarifa hiyo inaendelea.
“Halafu yatasafirishwa kwa barabara moja kwa moja hadi geti la Malindi katika Bandari ya Dar es Salaam, kabla ya kuingia kwenye njia za usafirishaji wa kimataifa. Hii inaashiria ufunguzi wa korido kuu ya biashara inayounganisha Afrika ya Kati na Afrika Mashariki,” taarifa hiyo inaendelea.
Taarifa kutoka katika kampuni hiyo inaonesha kampuni hiyo itatakiwa kuboresha maeneo ya Bandari ya Kigoma na eneo la Malindi kwa kujenga yadi, karakana, na kuwekea vifaa vya kisasa vya kupakia na kupakua pamoja na mifumo ya kisasa kiteknologia ya usimamizi. Sehemu ya mkakati wa Zijin ni kuleta vyombo vyenye uwezo wa kusafirisha mizigo mikubwa katika ziwa Tanganyika.
“Zaidi ya hayo, ili kuboresha mnyororo mzima wa usafirishaji, Zijin inajenga meli kadhaa za kubeba mizigo zenye uwezo wa tani 2,000 nchini Tanzania, ambazo zinatarajiwa kukabidhiwa mwaka 2026,” taarifa ya Zijin inaeleza.
“Meli hizi hazitakuwa tu za kwanza za kisasa za kubeba mizigo mikubwa nchini Tanzania, bali pia zinachukuliwa na serikali ya Tanzania kama mafanikio ya kihistoria katika kuvutia uwekezaji na kuinua sekta ya uzalishaji wa ndani.”
Zijin inakuwa kampuni ya tatu kuingia makubalino na serikali ya Tanzania kati ya mwaka 2024 na 2025, kwa ajili ya kuendesha bandari.Kapuni zingine ni Pamoja na DP World inayoendesha bandari ya Dar es Salaam, yaan, gati namba 4 mpaka 7 na gati namba 0 mpaka 3. Na mkataba kati ya kampuni ya Adani kuendesha gati la kontena, yaani gati namba 8 mpaka 11.
Zijin ni moja ya kampuni kubwa binafsi kutoka China, moja ya mradi wake mkubwa ndani ya Afrika Mashariki na kati ni machimbo ya Kamoa-Kakula Copper Mine yaliyopo nchini DR Congo.
