Kuanza shule mpya ni jambo kubwa kwa watoto wetu, wawe na miaka mitatu au 18. Ni wakati unaoweza kujaa msisimko wa kukutana na walimu wapya, marafiki wapya na mazingira mapya, lakini, mara nyingi, pia kuna wasiwasi.
Kwa watoto, kila kitu kipya kinaweza kuonekana kikubwa na kisichojulikana. Kama wazazi, maandalizi tunayofanya nao yanaweza kuleta tofauti kubwa kati ya mtoto kuanza shule akiwa na hofu au kuanza akiwa na ujasiri.
Kwa watoto wetu wadogo wanaoanza shule ya awali au chekechea, huu mara nyingi ndiyo mwanzo wa safari yao ya kujitegemea mbali na nyumbani. Katika hatua hii, mambo mengi yatakuwa mapya kwao. Kabla ya siku ya kwanza, tunaweza kuwapeleka kutembelea shule waone darasa lao, uwanja wa michezo na hata choo watakachotumia.
Nyumbani, tunaweza kuanzisha mazoea rahisi ya kila asubuhi kama kuvaa sare, kula kifungua kinywa na kubeba begi dogo. Tunaweza pia kucheza “shule” pamoja, tukibadilishana nafasi kati ya mwalimu na mwanafunzi. Mwishowe, tuwatie moyo kwa kuwaambia kuwa ni sawa kuhisi hofu kidogo, na kwamba tutakuwepo kuwapokea mwisho wa siku, kama tulivyokubaliana.
Kwa watoto wetu wanaoanza shule ya msingi ya awali – darasa la kwanza hadi la tatu– tunahitaji kuwasaidia kujiamini katika masomo na pia kujua namna ya kuishi na kundi kubwa la wanafunzi. Ni muhimu kuelezea ratiba ya siku ya shule, watakoweka begi, muda wa mapumziko, na jinsi ya kumwendea mwalimu wanapohitaji msaada.
SOMA ZAIDI: Je, Mbinu Zote za Malezi Yaliyotulea Sisi Bado Zinafaa?
Tukiwa pamoja, tunaweza kupita njia ya kwenda shule ili wajue maeneo muhimu. Hata michezo midogo ya kusoma na kuhesabu nyumbani inaweza kuwasaidia kuanza wakiwa tayari. Tuwahakikishie kwamba kila mtu anaanza akiwa mgeni, na muda si mrefu watazoea.
Kadri wanavyosonga mbele katika shule ya msingi ya juu – darasa la nne hadi la saba – masomo yanakuwa magumu zaidi na marafiki wanakuwa na nafasi kubwa katika maisha yao. Hapa, tuwape nafasi ya kumiliki maandalizi yao wenyewe. Waandike majina yao kwenye vitabu, wapange mabegi yao, na wawe na eneo dogo la kujisomea nyumbani.
Tuzungumze nao kuhusu namna ya kuchagua marafiki wazuri tunaweza kuigiza mazungumzo au michezo ya kujiunga na wenzetu. Tuwakumbushe kwamba si lazima wajue kila kitu siku ya kwanza; kujifunza jinsi mambo yanavyofanyika ni sehemu ya safari.
Kuingia shule ya sekondari – kidato cha kwanza hadi cha sita – mara nyingi ni hatua kubwa zaidi na inahusisha kuanza maisha ya bweni kwa mara ya kwanza. Hapa, kujitegemea ni jambo la msingi.
Tuhusishe watoto wetu kwenye kupanga mizigo ili wajue kila kitu walichobeba na wavione kama mali yao binafsi. Tuwafundishe ujuzi wa maisha kama kufua nguo, kupanga matumizi ya fedha ndogo watakazopewa na kutunza mali zao. Tuwe na utaratibu wa mawasiliano ili wawe na uhakika wa lini watatupigia au tutawapigia.
SOMA ZAIDI: Tuwafundishe Watoto Wetu Urafiki Mzuri ni Upi
Tuzungumze nao pia kuhusu kujitunza kiafya kulala kwa wakati, kula vizuri, na kumtafuta mtu mwalimu wa kumsaidia atakapohitaji. Tuwakumbushe kwamba ni kawaida kukumbuka nyumbani, lakini kuendelea na ratiba na kulenga malengo kutawasaidia kuzoea haraka.
Pia, katika hatua hii ya elimu, masomo yanaongezeka na watu wapya wanakuwa wengi. Tuwasaidie kujiandaa kwa kuwafundisha kupanga muda wao, ratiba yenye masaa ya kusoma, kupumzika na kushiriki shughuli za ziada. Tuzungumze nao kuhusu kuchagua marafiki wanaowajenga na kuepuka vishawishi vibaya.
Ikiwezekana, tutembee nao shule mapema ili wajue maeneo muhimu kama madarasa, maabara na ofisi. Tuwahakikishie kwamba watakutana na watu wengi wapya, lakini sisi daima tutabaki kuwa ngome ya usalama kwao.
Katika kila hatua hizi zote, maandalizi ya kweli siyo tu kununua sare na vifaa vya shule. Ni kuwapa watoto wetu ujasiri, maarifa na mbinu za kushinda changamoto wanazoweza kupitia pamoja na mabadiliko ya mazingira ili mwanzo safari yao ya elimu iwe yenye furaha na mafanikio.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.