The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Mashekhe, Maimamu, Tanzania Wamuunga Mkono Rais Samia Kuelekea Uchaguzi 2025. Wasisitiza Amani

Sehemu kubwa ya viongozi hao wa dini walionesha kupendezwa na utendaji wa Rais Samia kama sababu ya kummuunga mkono kuelekea uchaguzi unaokuja.

subscribe to our newsletter!

Wakiongea katika kongamano la Umoja wa Maimamu Tanzania (UMATA) kuombea uchaguzi Mkuu 2025, viongozi mbalimbali wa dini ya Kiislamu kutoka katika madhehebu na taasisi mbalimbali wameeleza kumuunga mkono Rais Samia kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.

Rais Samia Suluhu Hassan alikuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo lililofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee, mnamo Agosti 24, 2025. Ambapo Rais Samia aliweza kufanyiwa dua maalum na watoto alipowasili ukumbini hapo majira ya asubuhi.

“Sisi tunamuomba Allah Subhanahu wa Ta’ala aendelee kukupa idhaa na uendelee zaidi na zaidi. Dua bila juhudi ni uwendawazimu, pamoja na dua lazima tufanye juhudi,” alieleza Sheikh Arif Surya, Mwenyekiti wa Umoja wa Maimamu Tanzania, akiwa mmoja wa wazungumzaji wakuu kabla ya Rais Samia kutoa hotuba yake.

“Sisi kama UMATA, viongozi tunakuahidi safari yako yote utakayokwenda huko katika mikoa yako, basi sisi kama UMATA, kila utakapokuwa katika mkoa pale mahala sisi tutatafuta msikiti mkubwa tutafanya ibada ya itikafu kwa ajili ya kukuombea,” aliendelea zaidi, Sheikh Arif Surya, mbele ya mamia ya waumini waliofika.

Katika risala yao, UMATA walieleza malengo ya kongamano hilo yalikuwa ni kwanza kuwaandaa Watanzania katika kuilinda amani, kabla na baada ya uchaguzi. Pili kuzindua kampeni ya amani yetu, kwa mustakabali wetu. Kampeni hiyo ina lengo la kuwakumbusha Watanzania kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi, na kuwahimiza viongozi wa dini zote kuhubiri amani.

Akikazia katika hotuba yake kuhusu amani, Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Walid Alhad Omar amemuhakikishia Rais Samia Suluhu juu ya mshikamano uliopo katika kuilinda amani Tanzania.

“Fanya kazi yako kwa uhuru kabisa na bahati nzuri hawa sio wa Dar es Salaam tu, lakini ni wa mikoa 26. Dar es Salaam mimi nina misikiti 10,300 sasa sijui na mikoa mingine. Mashekhe wa mikoa wako hapa tungekuwa tumepata nafasi tungetoa takwimu ungeona namna gani inaombewa nchi hii amani,” alieleza Sheikh Walid Omar.

“Hakuna kitakachovuruga amani ya nchi hii kwa sababu hiyo. Matusi siku zote ni silaha ya mwenye kushindwa, ukimuona mtu unajadiliana naye akatoka kwenye hoja akaanza matusi, we endelea kupiga kazi ujue huyu ushammaliza,” aliongeza zaidi.

Sababu za kumuunga mkono

Sehemu kubwa ya viongozi hao wa dini walionesha kupendezwa na utendaji wa Rais Samia kama sababu ya kummuunga mkono kuelekea uchaguzi unaokuja.

“Mungu atujalie wote kuwa na nia na moyo wa kumuombea kwa dhati Mheshimiwa Rais wetu, aweze kutimiza jukumu lake,  na uchaguzi uende salama na kwa amani; na faraja kubwa kwetu Watanzania tuone mama yetu amepita kwa kishindo sana,” alieleza Murtaza Adamjee, mwakilishi kutoka dhehebu la Bohora.

“Tunaomba kwa Mwenyezi Mungu aweze kuleta amani katika nchi yetu, na Rais wetu apite kwa kishindo katika uchaguzi unaokuja,” aliongezea pia mwakilishi wa dhehebu la Ismaili Tanzania.

Amiri Mkuu wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taaisis za Kiislam Tanzania, Sheikh Mussa Kundecha alielezea maeneo kadha wa kadha ya kiutendaji katika serikali ya Rais Samia, yanayowafanya wanajumuia wa dini ya kiislamu kumuunga mkono, ikiwemo kuondoa hofu kwa wafanyabiashara, kuleta mtaala mpya unaofanya masomo ya dini kuwa rasmi na masuala ya kifedha.

“Kama Waisalamu tulikuwa na hofu kubwa, tulikuwa na sonona, takribani miaka kumi na mbili iliyopita palianzishwa dirisha la kwanza la mfumo wa fedha wa kiislamu, Alhamdulillah, likawa dirisha gumu dogo, halitutoshi kama Watanzania,” alieleza Sheikh Kundecha.

“Kupitia kwako, tumeshuhudia kwa macho yetu kufunguka mfumo wa fedha wa Kiislamu ambao unatuondoa kama Waislamu katika hofu ya riba, mtihani huo umetuondolea, tumekuwa na faraja kubwa,” aliongeza zaidi.

Jambo lingine alilolielezea Kundecha ni suala la mitaala: “Kupitia uongozi wako, tunashuhudia katika mtaala mpya na mtaala uliyoboreshwa sasa masomo ya dini ni rasmi. Kazi ni kwa Watanzania kuandaa misingi yote ya kuwapata walimu bora wanaoweza kufundisha lugha ya kiarabu, wanaoweza kufundisha maarifa ya kiislamu, na pia watapata ajira ya serikali ya kufanya kazi hiyo ambayo kwa kipindi chote tumekuwa tukifanya waislamu bila msaada wa aina yeyote.”

Akizungumzia kuhusu hali ya ujumla katika jamii, Kundecha amechambua kuwa kwa sasa tofauti na serikali iliyopita mambo yanaendeshwa kwa utulivu na hakuna hofu katika jamii.

“Katika kipindi kifupi ulichokipata umeweza kufanya haya, tunaamini, ukipata kipindi kingine tunaweza kupata makubwa na zaidi kuliko haya tuliyoyapata. Tunamuomba Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Ta’ala,  akupe nafasi hiyo nyingine tena kama alivyokupa hapa mwanzoni,” ameeleza Kundecha.

Mwakilishi wa Ofisi ya Mufti Mkuu Zanzibar, Sheikh Shaaban Batwashy ambaye ni Mkuu wa Divisheni ya Utatuzi wa Migogoro, alieleza kuwa utendaji mzuri katika serikali ya awamu ya sita umeweza kuifanya Tanzania kuwa nchi ya mfano duniani.

“Tanzania imekuwa ni kama lulu kwa nchi nyingine duniani,  na wewe Mheshimiwa Rais kwa hakika umefanya makubwa sana na uendelee kufanya makubwa sana kiasi ambacho yale matarajio yamevuka mpaka ule usawa wa mbingu yanakwenda juu zaidi. Tunakutakia heri na kukuombea dua na baraka za Mwenyezi Mungu. Ili uzidi kutuongoza zaidi katika muda uliobakia na muda unaokuja vile vile,” alieleza  Sheikh Shaaban Batwashy.

Dini inavyosema kuhusu wanawake kuwa viongozi

Moja ya mambo ambayo viongozi hao waliyafafanua ni suala la uongozi kwa wanawake kwa mujibu wa maandiko katika dini ya Kiislamu.

“Uislamu unasema mwizi akatwe mkono, sasa leo utamkata mwizi mkono serikali itakuacha? Kwa hivyo katika serikali ya kiislamu ndiyo mwanamke haongozi, serikali kama siyo ya kiislamu, mwanamke anaongoza,” alieleza  Sheikh Mirambo Yusuph Kamili katika hotuba yake akiwawakilisha Maimamu wa mikoani.

“Mheshimiwa Rais haya sisi tumeyazungumza katika mikoa mbalimbali, kuna kundi linaongozwa na Abdul Kambaya kupita mikoa, mimi walinikuta katika mkoa wa Tabora tukayazungumza haya, kisha tulienda nao Katavi tukayazungumza haya, wao walienda na kwingine. Tukiwezeshwa pia tutapita kuyaeleza haya maeneo yote. Na yapo katika vitabu sio ya kwetu,” aliendelea kufafanua zaidi.

Kiongozi wa wanawake katika umoja wa maimamu, Hajat Farhana naye alisisitiza juu ya umuhimu wa kuendelea kumuunga mkono Rais Samia.

“Wanawake umetupa heshima zaidi, kutufanyia vizuri katika nafasi yako ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na sisi wote wanawake wa UMATA tutaendelea kukufanyia dua, Allah akufanyie wepesi katika safari yako ya mitano mingine kwa manufaa ya Watanzania wote,” alieleza Farhana.

Katika kongamano hilo Rais Samia aliwataka viongozi wa dini kuendelea kuwajenga waumini wao ki-imani ili kudumisha amani nchi, akitaja kuwa uchu wa madaraka ni moja ya sababu inayoleta viashiria vya uvunjifu wa amani.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×