Akizungumza katika Kongamano la Umoja wa Maimamu Tanzania kuombea uchaguzi, lilofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee leo Agosti 24, 2025, Rais Samia ametahadharisha juu ya kupanda kwa joto la kisiasa wakati wa uchaguzi Tanzania.
“Kwa kawaida, kote duniani, kipindi cha uchaguzi hupandisha joto la kisiasa nchini…..linatokea kwa sababu wapo wanaotafuta kutumia kipindi hicho kama mwanya wa kuvuruga amani, na hawa wako nje ya nchi na ndani ya nchi,” alieleza Rais Samia.
“Nje ya nchi ni wale wanaohisi kwamba wakituvuruga yale wanayoyatamani kuyafanya ndani ya Tanzania tukivurugana, watapata mwanya wa kuingia na kuja kuyafanya yale wanayoyatamani,” alifafanua zaidi.
“Au labda watapata kubadilisha uongozi wa nchi, waje wale ambao hawakujengwa na misingi ile tuliyowekewa na wazee wetu waliotutangulia wakati wa uhuru. Waweke wao ambao wanaweza wakawaweka mawazo yao kichwani na wakaweza kuendeleza nchi kama wanavyofanya katika maeneo mengine,” aliongeza zaidi.
“Lakini wale wa ndani kuna wawili wanaotumika na hao wa nje, lakini kuna wale ambao wanahaha kwa uchu wa madaraka na ulwa, ameomba amekosa, [anajiuliza] kwa nini nikose. Kwa nini yule na sio mimi, hao nao ni wavunjifu wa amani.”
Rais Samia ameendelea kuwataka viongozi wa dini kuwajenga waumini wao ki-imani ili kuweza kujiepusha na vishawishi vya uvunjifu wa amani, hata hivyo Rais Samia ametahadharisha hata kwa viongozi wa dini wako wenye changamoto.
“Kinachonipa matumaini ni kwamba hapa nchini kwetu viongozi wa kidini,kijamii na kisiasa walio wengi wamekuwa mstari wa mbele kuhubiri umoja, amani na utulivu. Wachache sana ambao wanahubiri yasiyo, na pengine ukienda kwa undani sio viongozi sawa sawa wa dini, wamevaa huo mwamvuli, lakini wanafanya mengine.”