The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Tumewauliza Wakazi wa Dar Kama Wanadhani Wanafaidika na Mfumo wa Vyama Vingi. Haya Ndiyo Majibu Yao 

Wengi wanasema mfumo huo ni mzuri unaopaswa kubaki, wakitoa wito kwa kasoro zinazoukabili kurekebishwa ili uweze kunufaisha vizuri zaidi.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Wakazi wa jiji hili kuu la biashara nchini Tanzania wameuelezea mfumo wa vyama vingi vya siasa kama kitu kizuri cha kuwanacho kama nchi kwani unasaidia kuwapa wananchi fursa ya kuamua nani awe mwakilishi wao, lakini pia husaidia kuwachangamsha wale waliopo madarakani.

Wakazi hao walitoa maoni hayo wakati wa mazungumzo na The Chanzo ilipowatembelea kwenye maeneo yao ya kazi, wengi wao wakitamani mfumo huo uendelee kuwepo kutokana na faida zake, na zile kasoro zinazoukabili zirekebishwe kwa manufaa mapana ya umma. 

“Nanufaika, kwa sababu, ili nichague Rais ambaye nampenda, inabidi kila chama kisimamishe Rais, inabidi kila chama kisimamishe mbunge, inabidi kila chama kisimamishe diwani, nimchague Rais ninayempenda, nimchague mbunge ninayempenda, nimchague diwani ninayempenda,” alisema Mama Mudi kutoka Msasani.

“Kuliko ukisimamisha kwa kusema labda chama kimoja kimsimamishe mgombea mmoja, chama kingine kisimsimamishe, pale nakuwa mimi sina manufaa nao, kutokana na kila mwananchi anamchagua kiongozi ampendaye,” aliongeza mama huyo anayejishughulisha na biashara ya mamantilie.

Jumanne Husseni Bigo, mkazi wa Manzese anayejishughulisha na biashara ya uuzaji wa magezeti, anasema kwamba mfumo wa vyama vingi una manufaa makubwa kwa sababu unawaamsha wale waliopewa dhamana ya kuunda Serikali kwenye uchaguzi uliopita. 

SOMA ZAIDI: Wananchi Dar Waeleza Matamanio Yao Binafsi Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025

“Watu wa chama tawala hao,” anasema Bigo, “ambao kidogo walikuwa wao wanajiona wao ndio wako wamoja tu, lakini kwa sababu wako wengi imeleta changamoto.” 

Mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania ulirejeshwa mwaka 1992 baada ya Tanzania kufuata mfumo wa chama kimoja kwa miaka mingi. Watanzania walishiriki kwenye uchaguzi wa vyama vingi wa kwanza mwaka 1995, na uchaguzi wa mwisho ukiwa ni ule wa 2020.

Mnamo Oktoba 29, 2025, Watanzania watashiriki kwenye uchaguzi wa saba wa vyama vingi, wakitegemewa kwenda kuchagua Rais, wabunge na madiwani. 

Tangu kurejeshwa kwake, changamoto mbalimbali zinazohusiana na uchaguzi, ikiwemo vyombo vilivyokabidhiwa jukumu la kusimamiwa uchaguzi kudaiwa kupendelea chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM), zimekuwa zikiukabili mfumo wa vyama vingi nchini. 

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wananchi wamekuwa wakihoji faida za mfumo wa huo, hususan pale wagombea wa vyama vya upinzani wanaposhindwa kutangazwa, licha ya ushahidi kuonesha wameshinda kwenye chaguzi hizo.

SOMA ZAIDI: Wananchi Wachambua Usahihi Zawadi za Wagombea Kipindi cha Uchaguzi 

Hata hivyo, wananchi ambao The Chanzo imezungumza nao wameonesha kuwa na imani na mfumo huu wa vyama vingi, huku wakitaka kasoro hizo zirekebishwe ili mfumo huo uweze kuwasaidia ipasavyo.

Uhuru wa kuchagua

“Tunanufaika kwa sababu mfumo wa vyama vingi unatupa uhuru wa kuchagua chama tunachokitaka,” alisema mwananchi mmoja kutoka Msasani aliyejitambulisha kwa jina moja la Diana. “Mimi nitakachoangalia ni sera, nilipopendezewa sera ndiyo hapo, sisi tuachoangalia ni sera.”

Lucas Majumbi, mkazi wa Manzese, anaamini kwamba ushiriki wa vyama vingi katika chaguzi una faida nyingi. 

“Kwanza, kuleta hamasa kwenye viongozi waliopata uongozi kupitia labda chama cha CCM, au CUF, au CHADEMA au TLP,” alisema Majumbi. 

“Wanapokuwepo madarakani wengi huwa wanajisahau sana, hata kile ambacho unakuta wamekiahidi, hawezi kutekeleza,” aliongeza. “Lakini ukiwepo ushiriki wa vyama vingi katika uchaguzi inakuwa inawaletea changamoto.”

SOMA ZAIDI: Wananchi Dar Waeleza Sifa za Mwakilishi Wanayemtaka Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025

Kwa upande wake, Mohammedi Saidi kutoka Msasani, mfumo wa vyama vingi ni mzuri kwani unamsaidia mwananchi kupata kiongozi bora.

“Hata kiongozi mwingine tunayemchagua anakuwa anajituma kuleta maendeleo kutokana na ukweli kwamba anafahamu akiharibu hatutomchagua tena,” aliongeza Saidi. “Ndiyo maana vyama vingi, vinakuwepo.”

“Vyama vingi vinakupa uhuru wa kuchagua mtu unayempenda,” alisisitiza mwananchi huyo. “Kwamba, huyu kiongozi mimi anatufaa kutuongoza katika jimbo, au katika mtaa, au Rais, inakuwa inatunufaisha kwa namna hiyo.”

‘Tunateseka’

Walipoulizwa ni yepi matarajio yako kuhusu uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, wananchi wengi walisema wanatamani zoezi hilo lifanyike kwa amani, uhuru na haki, bila ya kuwepo kwa vurugu au sintofahamu yoyote. 

Wananchi walisema pia kwamba wanatamani yoyote atakayepata dhamana ya kuunda Serikali asiwashau wananchi wa chini ambao wamedai wanapitia hali ngumu za kimaisha.

SOMA ZAIDI: Kwa nini Mwaka wa Uchaguzi 2025 ni wa Kihistoria na Sababu za Hitaji la Muafaka wa Kitaifa Kabla ya Uchaguzi

“Waangalie namna ambavyo wananchi tunapata tabu,” alisema Hamisi Makabuli, mkazi wa Manzese. “Wanachi sisi tunapata tabu sana. Tuko katika mazingira ya hali ya chini sana.”

“Tunafannya kazi, lakini kipato vimekua vichache,” aliongeza Makabuli. “Kwa hiyo, tunaomba ambao watakuwa madarakani, wajaribu kutekeleza mambo yote yale ambayo wanatoa ahadi watekeleze ili maisha yawe bora kwa wananchi.”

Hija Selemani ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia hijaselemani9@gmail.com.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×